WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Friday, August 4, 2017

BILIONI 600 ZAMPELEKA NEYMAR PARIS St-GERMAIN

Neymar: Paris St-Germain wamnunua nyota wa Barcelona kwa rekodi ya dunia ya euro 222m

Neymar

Paris St-Germain wamekamilisha kumnunua mshambuliaji wa Brazil, Neymar, kwa ada iliyoweka rekodi mpya ya ununuzi wa mchezaji ya euro 222m (£200m) kutoka Barcelona.
Ununuzi huo wa mchezaji huyo wa miaka 25 umevunja rekodi ya awali iliyowekwa Paul Pogba aliporejea Manchester United kutoka Juventus kwa £89m Agosti 2016.

Atakuwa analipwa euro 45m (£40.7m) kwa mwaka - euro 865,000 (£782,000) kila wiki - kabla ya kutozwa ushuru katika mkataba wake wa kwanza wa miaka mitano. Hiyo ni jumla ya £400m.
Neymar amesema amejiunga na "mojawapo ya klabu zenye ndoto kuu zaidi Ulaya".
"Ndoto kuu ya Paris St-Germain ilinivutia kujiunga na klabu hiyo, pamoja na kujitoleza kwao na nguvu zinazotokana na hili," amesema.

"Najihisi niko tayari kuanza kazi. Kuanzia leo, nitafanya kila niwezalo kuwasaidia wachezaji wenzangu wapya."

Klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Ufaransa imepanga kuwa na kikao na wanahabari mwendo wa saa 12:30 BST Ijumaa (saa nane unusu Afrika Mashariki).
Neymar baadaye atatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa PSG Jumamosi wakati wa mechi yao ya kwanza kabisa ya msimu mpya, ambayo itakuwa nyumbani uwanja wa Parc des Princes dhidi ya Amiens.
Neymar alikuwa amefika kituo cha mazooezi cha Barcelona Jumatano akiandamana na babake na mwakilishi wake na kufahamisha klabu hiyo ya Uhispania kwamba angetaka kuondoka.
Alipewa ruhusa na meneja wa Barca Ernesto Valverde kwenda "kupanga mustakabali wake".
Nchini Uhispania, kifungu cha kumwachilia mchezaji kutoka kwa mkataba wake kinaweza tu kufunguliwa kwa mchezaji kulipa pesa yeye binafsi.

Neymar alipofika na pesa Alhamisi kulipa hata hivyo, maafisa wa La Liga walikataa malipo hayo.
Kulitokea majibizano kati ya maafisa wa La Liga na wasimamizi wa Ligue 1.
La Liga wanaamini PSG huenda wanakiuka sheria za uchezaji haki kifedha (FFP) kwa kumnunua mchezaji huyo wa Brazil.

Baada ya kushindwa kulipa pesa hizo kwa La Liga, wawakilishi wa Neymar walilipa euro 222m (£200m) katika afisi za Barca badala yake.
Neymar alijiunga na Barca mwaka 2013 na akashinda mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

PSG wameorodheshwa wa 11 kwa thamani duniani na Forbes lakini ni mara yao ya kwanza kwao kuvunja rekodi ya dunia katika kumnunua mchezaji.

Neymar ni nani?

  • Alizaliwa Mogi das Cruzes, viungani mwa Sao Paulo, 5 Februari 1992
  • Alianza uchezaji wake Santos kwa kutia saini mkataba wa kulipwa Januari 2009
  • Amesalia kuwa mfungaji mabao mengi zaidi Santos baada ya enzi ya Pele ambapo aliwafungia mabao138 mechi 229.
  • Alihusishwa na kuhamia Real Madrid, Chelsea na Manchester United kabla ya kuchukuliwa na Barcelona Juni 2013 akiwa na miaka 21.
  • Alichezea Barca mechi yake ya kwanza dhidi ya Levante Agosti 2013 na akawafungia mabao 105 na kusaidia ufungaji wa mengine 80 katika mechi 186 alizochezea klabu hiyo ya Catalona.
  • Alichezea timu ya taifa mara ya kwanza akiwa na miaka18 na amefunga mabao 52 katika mechi 77 alizochezea Brazil

Thursday, August 3, 2017

Wanyarwanda wanapiga kura kuchagua Rais wao Leo

https://ichef.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/15B44/production/_97200988_1ef3c25d-0299-49b4-a74a-543ba0b4061f.jpg
Raia nchini Rwanda wanamchagua kiongozi mkuu wa Rwanda katika uchaguzi mkuu Ijumaa, ambao unatarajiwa na wengi kumuongezea muhula mwingine madarakani rais Paul Kagame.
Frank Habineza wa chama cha Green Party na Philippe Mpayimana, ambaye ni mgombea huru pia wanawania urais katika uchaguzi huu.
Lakini wapinzani hao wote hawatarajiwi kumpa ushindani mkubwa Kagame ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000.
Kuna hisia tofuati kuhusu utawala wake Kagame nje ya nchi hiyo.
Lakini uungwaji mkono mkubwa anaopata ndani ya Rwanda, unamhakikishia ushindi mkubwa katika uchaguzi huu.
Ameutaja uchaguzi huo kama mpangilio usio budi kufanyika.
Anasifiwa kwa kukuza uchumi wa taifa hilo.
Lakini wakosoaji wanamshutumu kwa kukandamiza upinzani na kuzuiwa uhuru wa kisiasa nchini.
Wagombea wengine wanasema wafuasi wao wamenyanyaswa lakini chama tawala kina kana tuhuma hizo.
Katiba ya Rwanda ilikarabatiwa mnamo mwaka 2015, na kumpa rais Kagame nafasi ya kushinda muhula mwingine wa miaka 7 na mihula mingine miwili ya ziada ya miaka mitano kila mmoja.
Kwa hivyo, ana nafasi ya kusalia madarakani hadi mwaka 2034.

MAALIM SEIF AKWAMA

·         Afukuza wabunge, Ashindwa
·         Katiba Cuf yambeba Lipumba
·         Msajili wa Vyama akaza Uzi, Amtaka Afate Utaratibu

Na Mwandishi Wetu.

Ni dhahiri sasa hali ya mambo inazidi kwenda kombo kwa upande wa katibu mkuu wa Chama cha wananchi Cuf Maalim Seif Sharif Hamad katika mgogoro wa kiuongozi unaoendelea baina yake na mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba, Jamvi la Habari linaweza kuthibisha.

Kitendo cha mwenyekiti wa chama hicho Prof. Lipumba kuwavua uanachama wabunge nane na madiwani wawili wa viti maalum kitendo kilichoonyesha kufuata taratibu zote za kisheria na katiba ya ndani ya chama hicho na hatimaye kubarikiwa na ofisi ya Bunge, Tume ya taifa ya Uchaguzi na msajili wa vyama vya siasa, kinaelezwa kumpagawisha katibu mkuu huyo na timu yake kiasi cha kuamua nayeye kuwavua uanachama wanachama wengine kadhaa akiwemo mbunge na naibu katibu mkuu anayekaimu majukumu ya katibu mkuu wa chama hicho kwa sasa kutokana nan kutokufika ofisini kwa Maalim Seif tangu mwezi septemba mwaka 2016 Magdalena sakaya na Maftah Nachuma ambaye pia ni mbunge wa mtwara mjini.

Katika barua yake kwa msajili wa vyama vya siasa, katibu mkuu huyo amemueleza msajili  huyo kuwa baraza kuu la uongozi la taifa lililokutana visiwani Zanzibar hivi karibuni kuwa wajumbe 43 kati ya 45 waliokutana visiwani humo wameridhia kuvuliwa kwao uanachama na kwamba anamfamisha msajili juu ya jambo hilo.

Katika kile kinachoitwa kufuata sheria na katiba ya chama hicho, msajili amemjibu kwa kumkumbusha kuwa yeye kama mlezi na mtunza kumbukumbu wa shughuli zote za vyama vyote vya siasa nchini, anafahamu kwamba ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho imekaimishwa kwa Magdalena sakaya na kwamba  ofisi yake inahitaji kupokea kwanza taarifa ya kutenguliwa kwa azimio hilo lililomuweka madarakani sakaya.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili inazo zinasema kuwa kwa sasa kambi ya maalim seif imeshakata tama juu ya mgogoro huo baada ya kujitathmini na kujigundua kwamba katiba ya chama chao inampa nguvu mwenyekiti wa chama hicho Prof.Lipumba na hivyo kujilaumu kila kukicha.

‘’unajua mwanzoni Maalim na Julius (Mtatiro) hawakujua kwamba Prof angekuwa na nguvu kiasi hiki, ndio maana wakampuuza, lakini laity kama wangejua namna ya ushindani wanaokuja kukabiliana nao hasa wa kikatiba nadhani hali isingekuwa kama ilivyo hivi sasa’’. Alinukuliwa Saidi Makame wa Darajani Zanzibar
‘’tatizo Prof. analindwa na ibara ya 117 ya chama, sasa kila maalim na wenzetu kadhaa tukijaribu kutafuta namna ya kumpiku, linapokuja swala la kisheria na mahakamani ama kwa msajili huyu bwana anatushinda tu’’. Aliongeza mwanachama huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar
Kadhalika, wakati hayo yanaendelea hivi karibuni mwenyekiti wa chama hicho alifanikiwa kusajili upya bodi ya wadhamini wa chama hicho baada ya ile ya awali kumaliza muda wake wa mujibu wa sheria jambo ambalo limezidisha pigo kwa timu ya maalim seif kwa sababu bodi ya wadhamini ya chama chochote cha siasa huwa moja tu inayosajiliwa na RITA na kwa mujibu wa katiba ya CUF bodi hiyo ndio mamlaka pekee inayoruhusiwa kufanya usimamizi wa jumla wa chama hicho ikiwemo kushtaki na kushtakiwa jambo linalohatarisha uwepo na uhalali wa kesi zilizofunguliwa na bodi ya awali dhidi ya Msajili wa vyama na Lipumba juu ya masuala kadhaa.

Aidha, kukwama huko kwa maalim Seif katika kile anachokiita mapambano ya kukinusuru chama hicho, kunamfanya sasa abadili mawazo na kujiandaa kuhamia chama kingine kikubwa cha upinzani hapa nchini chenye ngome yake kuu Tanzania bara.

Taarifa zaidi zinaonyesha kwamba mpaka sasa maalim na watu wake wameshakubali kuwa kisheria hawawezi kumshinda Prof. Lipumba na kwamba wamebakiwa na njia mbili pekee ama wahame kuhamia chama hicho kikubwa cha upinzani Tanzania bara ama waanzishe chama chao wenyewe kipya.

Mjadala unaoendelea hivi sasa baina ya wadau muhimu wa timu ya maalim Seif ni kwamba iwapo uamuzi utakuwa ni kuwa wanahama, je watahama na vyeo vyao walivyokuwa navyo wakiwa CUF kama hicho cha Katibu mkuu na vya baadhi ya vya wakurugenzi au watahamia na kuwa wanachama wa kawaida jambo ambalo wanahisi litawapunguzia nguvu ya kufanikisha agenda yao ya kuendelea kudai maslahi yao ya kisiasa yanayotokana nauchaguzi mkuu uliopita.

Taarifa hizo pia zinaeleza kuwa mpaka sasa majadiliano ya kina ya namna gani Maalim na timu yake watahamia chama hicho yameshaanza na yanaratibiwa vizuri na wanasiasa kadhaa mashughuli hapa nchini wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wenye vinasaba na chama hicho.

Ikiwa mwanasiasa huyo atahama chama hicho na kujiunga chama kingine kama njia ya kufikia lengo lake la kisiasa, kitakuwa ni kielelezo mahsusi cha kudhibitiwa na Prof. Lipumba katika kuijua na kuifahamu katiba ya chama hicho na pia ndio utakuwa mwisho wa ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

Alipotafutwa na gazeti hili msajili wa vyama vya siasa Jaji Fransis Mutungi, ameendelea kusisitiza kwamba ofisi yake itaendelea kufanya kazi za kuvisimamia vyama vyote vya siasa vilivyopo hapa nchini kama sheria iliyoviasisi inavyosema na kuongeza kuwa kinachoendelea ndani ya Cuf ni matokeo ya utekelezaji wa katiba ya chama hicho ambacho wameitunga wenyewe.

‘’mimi ofisini kwangu ninasajili vyama baada ya kuzipitia katiba zao na kujiridhisha kuwa hazikiuki masharti ya sheria za nchi, nikizipokea na kujiridhisha siongezi wala kupunguza kitu chochote zaidi ya kuzisajili, na kama ujuavyo katiba ikishapitishwa kinachofuata ni kutekelezwa tu’’. Alisema Msajili Mutungi

‘’kwa hiyo Lugha nyepesi kabisa kuitumia ni kwamba mchawi wa Cuf si Mutungi wala nani, Mchawi wa Cuf ni katiba yao wenyewe, waifate katiba yao inavyoelekeza nina imani hakuna malalamiko yatakayotokea, lakini kama wataendelea kufanya mambo kwa hisia na utashi binafsi, basi haya wataendelea kulalamikiana daima’’. Aliongeza mtaalamu huyo wa maswala ya sheria

Wednesday, August 2, 2017

HABIBU MCHANGE : TUMWAMINI NANI, CHADEMA AU ZITTO KABWE

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjWoB6pXyiTI5hN11Z86w-g110eWfHggGcwxRd44E5k3HS78-sH12cGy0YkZOhhy2f9wyqmWSFa5K-l_PilvdVcKfqUmkMAlsSaof0l8tYBQIyrAp9ZWoWQbjfU1wISvxP_pIPjnpiy9Es/s1600/bomola.jpg Habibu Mchange.
Na. Habibu Mchange

Kwa kipindi cha siku kadhaa sasa tumekuwa tukishuhudia maneno makali kutoka kwa wanachama na viongozi wa Chama cha CHADEMA kwenda kwa kiongozi wa chama cha ACT WAZALENDO ndugu Zitto Kabwe.

Njia mbalimbali zimetumika kufikisha mashambulizi hayo huku mitandao ya kijamii ikishika hatamu sambamba na makala za magazetini wakimuita Zitto kabwe ni Msaliti, wengine Kinyonga na wengine Mamluki huku Leo nikisoma makala nyingine ikimuita Zitto Kabwe ni Uyoga kwamba uyoga unaweza kutumiwa kama chakula na kadharika sumu.

Licha ya wanachama na viongozi hawa kujisahau pengine kuwa Zitto sio mwanachama wa chama chao na kwamba yeye ni mwanachama wa chama kingine kinachojitegemea chenye Sera, katiba na miongozo yake, lakini ni Dhahiri Viongozi na wanachama wa CHADEMA hawawezi kumsahau Zitto Kabwe.

Kama kuna jambo CHADEMA na viongozi wake nahisi linawauma na kuwanyima usingizi, basi kuendelea kuwepo kwa mwanasiasa huyu waliyemfukuza chama chao kwa matusi na kejeli nyingi mwaka 2015 mwanzoni.

Naam, ukisoma makala na maandiko yanayomshambulia Zitto kisa tu kakosoa kauli ya mwanasheria wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu kuhusu kutaka nchi inyimwe misaada na ushirikiano wa kimataifa, hauna utakachojifunza dhidi ya Chuki dhahiri za wanachadema kwa Zitto.

Kwa Lugha nyepesi tu unaweza ukasema CHADEMA na wafuasi wake wanatamani sana Madini yanayotemwa na Zitto Kabwe wa ACT WAZALENDO yangekuwa yanatemwa Hata kwa asilimia 20 na mmoja kati ya wabunge wao, ndio maana Hata Zitto afanye jema lipi, CHADEMA wao wataacha kulijadili alilolifanya watamvaa Zitto, huu ni udhaifu wa kiwango kikubwa sana.

CHADEMA wameumia sana Zitto kumsifia Rais Dkt Magufuli pale Jukwaani Kigoma, imewauma kwa sababu Hawakujua kuwa Zitto hakumsifia tu Rais Magufuli, Bali pia Zitto amempongeza kwa dhati kiongozi wa nchi anayepeleka mbele maendeleo ya wana kigoma.

Wamekasirika kwanini Zitto aliwahi kuukosoa utawala wa Rais Magufuli hapo nyuma halafu juzi eti amempongeza na kuona kwamba Zitto ni kigeugeu, walitamani Zitto aendelee kukosoa tu na kupinga hata maeneo dhahiri, ama wamesahau kwamba chama alichopo Zitto kwa sasa sio kazi yake kupinga kila kitu, na ndio maana wameamua kujitanabaisha na Slogan ya Taifa kwanza wakimaanisha kuwa wao maslahi ya nchi kwao ni kitu cha msingi kuliko chochote.

Wamesahau kwamba moja kati ya vichagizo vya Zitto na chama chake ni Kuupinga ujinga popote ulipo bila kujali chama cha anayefanya huo ujinga?. Ni vigumu sana kumuelewa Zitto kama haujui mpaka unaingia kwenye chama cha siasa unataka nini zaidi ya kupinga.

TUWAAMINI CHADEMA?...

Kwa msingi wa hoja zao kuwa Zitto ni kigeugeu na kwamba haaminiki Leo anaweza akapinga jambo na kesho akageuka, nadhani CHADEMA ndio wanaongoza kwa kuwa na sifa hiyo.

Kama hiyo ndio Hoja, basi Kwa sasa, CHADEMA ndio chama ambacho hakipaswi na hakiwezi kuaminiwa Mara 1000 zaidi kulinganisha na Zitto alivyo.

Nitatoa mifano Michache.

Mwaka 2013/2014, Freeman Mbowe akiwa kiongozi wa upinzani na mbunge wa Hai, aliwaongoza wabunge wenzake kupinga bajeti ya wizara ya Ujenzi iliyokuwa ikiongozwa na Dkt. Magufuli, mbowe aliipinga bajeti hiyo na kupiga kura ya hapana pale Bungeni, na kusema hawezi kuunga mkono serikali ya CCM.

Mungu si Athumani, mwaka huo huo Dkt Magufuli akaenda jimboni kwa Mbowe Hai, kisha au kabla alikwenda jimboni Rombo kwa Joseph Selasini, huwezi amini aisee,

Sifa alizozipolomosha Mbowe kwa Magufuli na Kikwete (aliyekuwa Rais) hazifikii hata Robo ya zile alizozitoa Zitto Kigoma, ndio maana ilimbidi mpaka Magufuli achukue link ya YouTube na kwenda nayo Bungeni katika bajeti iliyofata na kuwaambia wabunge na watanzani jinsi serikali ya CCM inavyochapa kazi kiasi cha kusifiwa hadharani na Freeman Mbowe. - NANI Tumuamini sasa, CHADEMA au Zitto?.

Naongeza, Kabla ya tarehe 15-09-2007, msamiati wa neno FISADI haukuwa maarufu hapa nchini Tanzania.

Unamjua aliyeuibua sawa sawa?.

Ni CHADEMA kupitia Tundu Lissu,

Ndio, Tundu Lissu akiwa Mwanachadema na mwanasheria machachali, tarehe 15-00-2007 pale viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es salaam, akishirikiana na Mbowe, na viongozi wengine wa upinzani akiwemo Dkt. Slaa, Maalim Seif , Mbatia na Wengine. Lissu alisoma Orodha ya Watanzania kumi na moja wanaolifilisi Taifa hili la Tanzania, tena akasema watu hawa hawanastaha ya kuitwa jina lingine zaidi ya MAFISADI, Lissu akasoma Orodha ya Mafisadi akisindikizwa na vifungu kibao vya Sheria.

Katika Timu ya watu 11 waliotajwa na Lissu kama mafisadi wanaoliumiza Taifa mtu NAMBA 9 aliyetajwa na Lissu na CHADEMA ni *EDWARD LOWASSA* Kwamba kwa mujibu wa Lissu na CHADEMA LOWASSA ni miongoni mwa Wafilisi 11 wa nchi hii, Leo LOWASSA yuko wapi, na Lissu yuko wapi na anasemaje?. - Tuwaamini CHADEMA ?.

Naongeza, Mwaka 2011/2012 kule Arumeru palikuwa na Uchaguzi wa Marudio, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA ambaye pia ni Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema, alisimama Jukwaani na Kuwashukuru wananchi kuwa walimzomea Mzee LOWASSA. Nitayarejea baadhi ya maneno yake

*"Jana mmemzomea LOWASSA, ni Heshima kubwa kwa Mungu Kumzomea Mwizi, LOWASSA ni FISADI*" Huyo ni God bless lema wa CHADEMA , Leo LOWASSA yuko wapi na Lema yuko wapi?, anasema nini?..- TUWAAMINI CHADEMA?.

Niongeze?... Msigwa alimtukana LOWASSA, akasema atakayemnadi na kumshabikia LOWASSA akapimwe akili yake, nani alimnadi LOWASSA 2015, ni Zitto au Msigwa?. - Tuwaamini CHADEMA ?

Mwaka 2010 katika kampeni za Uchaguzi mkuu Moja kati ya Sera za CHADEMA ilikuwa ni kurudisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kugeuzwa maghala, CHADEMA wakasema watavirudidha kwa wananchi, Mbowe akasema lazima virudi, Leo mwaka 2017 Mbowe yule yule anasema serikali imekosea kutoa tamko la kuvirudisha viwanda vile vile walivuotaka kuvirudisha wao mwaka 2010. Tuwaamini CHADEMA?...

Mwaka 2010 mpaka 2013 mwanzoni, CUF waliitwa CCM B na CHADEMA, Nccr wakaitwa Washirika wa CCM, miezi michache mbele CCM B na washirika wa CCM wakaungana wakaitwa UKAWA. tuimini CHADEMA?

Mifano iko mingi mingi mingi sana.

USHAURI

nawashauri viongozi na wanachama wa CHADEMA waachane na Zitto, wajenge CHADEMA yao, wamuache Zitto na ugeu geu wake na chama chake, watu makini wanafahamu kwamba CHADEMA ni kikundi cha watu wasaka madaraka tu na sio chama cha siasa.

Chama makini chochote cha siasa hakivunji wala kukiuka misingi yake iliyojiwekea,

Chama makini cha siasa hakiwezi badili Gia angani, lakini kikundi cha wasaka madaraka kinaweza Fanya lolote lile ilimradi tu kipate madaraka.

Wamuache Magufuli afanye kazi ya kuleta maendeleo aliyoahidi, maendeleo hayana chama, maendeleo hayana dini maendeleo hayana Kabila.

Kama Zitto alimpinga Magufuli Jana, sio kigezo cha kpongeza Leo kama amefanya vizuri na wala sio kizingizi cha kutokumkosoa kesho akifanya vibaya, hiyo ndio huitwa siasa ya masuala.

Ndio maana LOWASSA hamsimangi Lissu aliyemwita Fisadi namba Tisa hapa nchini,

Ndio maana LOWASSA hamsimangi Lema aliyekesha akimtukana katika mikutano ya kisiasa

Ndio maana LOWASSA hamsimangi msigwa, hamsimangi Mbowe aliyemkejeli kuwa ni dhaifu na baadae kumpokea wala hamsimangi yeyote, anafanya siasa zenye kukipigania anachokiamini atakipata ama anataraji kukipata.

Vijana, viongozi na wanachama wa CHADEMA kuhangaika na kina Zitto, Kitila mkumbo na Anna Mgwira ni kujidharirisha kwa kuonyesha kiwango kidogo cha uelewa wa masuala ya siasa.

Nawapongeza sana baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA wanaojikita kila uchao kuhangaika kutafuta suluhu ya changamoto za wananchi wao kama MEYA Boniface Jacob, John Mnyika, David Silinde Mwita Waitara nakadharika.

Muhimu kujua ni kwamba Zama zimebadilika, siasa zimebadilika, siasa za Leo si sawa na siasa za miaka mitano iliyopita.

Siasa za Leo zinahitaji wanasiasa wanaoleta majawabu kwa wananchi wao kuliko kutukanana kila uchao. Mmeshatukanana imetosha sasa wapeni majawabu wananchi.

Ndimi,
Habibu Mchange
0762178678
Mwananchi wa kawaida.

Friday, July 21, 2017

HIVI NDIVYO MORINYO ALIVYOMZIDI GUADIOLA

Manchester United imejipatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wa jadi Manchester City katika debi ya kwanza ugenini huku ziara za 2017 zinazofadhiliwa na Aon zikiendelea kuipatia ushindi the red Devils.
 Romelu Lukaku na Marcus Rashford wakisherehekea ushindi wa mabao yao
 Romelu Lukaku na Marcus Rashford wakisherehekea ushindi wa mabao yao

Romelu Lukaku na Marcus Rashford waliisaidia United katika mabao yote mawili yaliofungwa katika kipindi cha kwanza.

Kikosi hicho cha Jose Mourinho kilianza kwa mashambulizi huku Anders Herrera akianzisha juhudi hizo mapema, huku mashambulio mengine yakitoka nje ya eneo la hatari ,United wakimjaribu kipa mpya wa City Ederson.

David De Gea alilazimika kuwa macho katika upande mwengine huku Raheem Sterling akishambulia mara mbili , kabla ya Chris Smalling kuzuia mashambulizi mawili yaliofanywa na Patrick Roberts na Sterling.

United hatahivyo ilifanikiwa dakika nane kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza baada ya Lukaku kupata pasi muruwa kutoka kwa Paul Pogba na kucheka na wavu.
Dakika mbili baadaye Marcus Rashford aliifungia United bao la pili akifunga baada ya kazi nzuri kutoka kwa Henrikh Mkhitaryan

BREAKING NEWS:- Msemaji wa mawakili wa Trump ajiuzulu

Rais TrumpRais Trump 
Msemaji wa mawakili wa rais Donald Trump amejiuzulu, kulingana na vyombo vya habari.
Mark Corallo alikuwa msemaji wa Marc Kasowitz ambaye anamtetea Trump katika uchunguzi kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani na kumsaidia rais huyo kupata ushindi.
Ripoti zinasema kuwa bwana Corallo alitofautiana na mipango ya mawakili wa Trump kuwadharau na hata kupunguza uwezo wa maafisa wanaoongoza uchunguzi huo.

Hakujakuwa na tamko lolote kutoka kwake ama hata mawakili hao wa Trump.
Bwana Corallo ni mwandani wa wakili wa idara ya haki Robert Mueller ambaye anaongoza uchunguzi huo dhidi ya Urusi na amemsifu hadharani kulingana na mtandao wa politico.
Afisa huyo amekatishwa tamaa na operesheni za mawakili hao mbali na kambi pinzani zilizopo, ripoti hiyo imeongezea.

Bwana Mueller amewaajiri watu maarufu kujiunga na kundi lake, ambalo linachunguza iwapo kulikuwa na ushirikiano wowote kutoka kwa kundi la Trump ambao Urusi na rais Trump amekana kuwepo.

UTALII : Taifa la Tanzania latajwa kuwa eneo bora la Safari Afrika

Safari katika mbunga ya Serengeti nchini Tanzania 
Safari katika mbunga ya Serengeti nchini Tanzania


Taifa la Tanzania limetajwa kuwa kivutio kizuri cha safari za watalii barani Afrika kulingana na mtandao wa SafaricBookings.com ambao ndio mtandao mkubwa wa ukuzaji wa safari za Afrika.
Mtandao huo ulifanya tathmini ya zaidi ya wataalam 2500 na wale walioshiriki katika safari hizo kabla ya kutangaza kuwa Tanzania ndio eneo bora la safari mwaka 2017.

Tathmini hizo ziliandikwa na watalii walioenda safari pamoja na wataalam bingwa wa Afrika.
Mtandao huo unasema kuwa uchanganuzi huo pia ulibaini kwamba Tanzania ilipata umaarufu wake kutokana na idadi ya wanyama mbali mbali.

Watu maarufu katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakizuru taifa hilo wakitembelea maeneo tofauti ya vivutio vya utalii nchini Tanzania.

Watu hao ni mwanamuziki maarufu Usher Raymond, aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Manchester United na Real Madrid David Beckham, aliyekuwa mchezaji wa Liverpool Mamadou Sakho , mchezaji wa Everton Morgan Schneiderlin na nyota wa filamu kutoka Marekani Will Smith na Harrison Ford.

Walitembelea mbuga za Serengeti na mlima kilimanjaro.
Mtandao huo uliitaja Zambia kuwa taifa lenye kivutio kizuri cha misitu huku wataalam wote wakikubaliana kwamba mazingira ya misitu nchini humo mi mazuri zaidi.
Vilevile Zambia pia ilitajwa kuwa taifa lenye maisha bora ya ndege.
Namibia na Kenya zilitajwa kuwa bora katika mandhari mazuri pamoja na ndege waliopo mtawalia.