Na
MWANDISHI WETU
NI
historia na msimamo mkali. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya Rais Dk. John
Magufuli kuisimamia kwa vitendo sera ya elimu bure kwa shule za msingi na
sekondari nchini.
Kutokana
na hali hiyo, wadau mbalimbali wa ndani zikiwamo taasisi za umma na sekta
binafsi zilitangaza kumuunga mkono, huku Serikali ya Uingereza ikivutiwa na
mpango huo.
Hatua
hiyo inatajwa kama njia ya mafanikio kwa Rais Dk. Magufuli ambaye Novemba 5,
mwaka huu anatimiza miaka miwili madarani, huku akitajwa kama shujaa
aliyedhamiria kuinua elimu kwa vitendo.
Kitendo
cha Rais kutamka hadharani kuwa serikali yake anayoiongoza haitawalipisha ada,
gharama za mitihani na michango mingineyo iliyokuwa inawakwaza wazazi na walezi
wa wanafunzi hasa wanyonge na masikini
kwa kueleza kutengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 18.7 kila mwezi kwa ajili ya
kugharamia mfumo na sera ya elimu bure hapa nchini.
Kadharika,
kuasisiwa huko kwa utaratibu huu wa elimu bure kumesababisha kuwepo kwa
mafanikio makubwa katika usajili na uandikishwaji wa wanafunzi wanaoanza darasa
la kwanza baada ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi waliofikisha umri wa
kwenda shule na kujiunga katika mikoa mbalimbali ya sehemu kubwa ya nchi
‘’kwetu
sisi hakika tumevuka malengo na matarajio, wakati rais anatuagiza kutekeleza
mfumo huu wa elimu bure hatukutarajia kama muitikio ungekuwa mkubwa kiasi hiki…kwa
kweli mfumo huu wa elimu bure umesababisha watu wengi zaidi wawaandikishe
watoto shule na hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kuwepo kwa watoto wasiojua
kusoma na kuandika katika siku zijazo’’. Alinukuliwa Mtela Mwampamba, Katibu tawala
wa wilaya ya Kisarawe.
Aidha
akizungumza na gazeti hili mkazi wa Morogoro kihonda Aziza Matiga Malinda
amempongeza Rais kwa msimamo wake wa kutoa elimu bure kwa kuzingatia ukweli
kwamba unasaidia kuondoa matabaka baina ya watanzania na watu wote wenye sifa
za kwenda shule sasa watakuwa wanakwenda shule bila kikwazo wala kizingiti cha
ada akitolea mfano yeye anavyoweza kuwasimamia watoto wake watatu kwenda
sekondari huku yeye gharama zake zikiwa ni utekelezaji wa majukumu mengine kama
mzazi na si ada wala michango ya shuleni.
‘’Unaona
mimi ninasomesha watoto watatu hapo, mmoja kidato cha pili na mwingine cha tatu
na mmoja darasa la sita, sasa kwa hali yangu hii ningeweza kweli kuwalipia ada
na michango mingine hawa watoto wote?..kwa kweli namshukuru sana Mungu kwa
kutuletea Rais huyu mwenye Huruma’’. Alisema Aziza
Madawati
Katika
kile kinachoonekana kufanikiwa kwa elimu bure kwa kipindi cha miaka miwili ya
uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, wakuu wa mikoa na wilaya wamefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kutimiza agizo la mkuu huyo wa nchi la kukabiliana na upungufu wa
madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha wanafunzi
wanasomea katika mazingira bora.
Mapema
mwaka jana, Rais Magufuli aliteua wakuu wapya wa mikoa na baada ya kuapishwa
aliwaambia vigezo atakavyotumia kuwapima ni pamoja na kushughulikia tatizo la
upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuimarisha
mazingira ya shule na kufanikisha sera ya kutoa elimu bure kuanzia elimu ya
awali hadi kidato cha nne.
Rais
aliwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana wawe
wamelimaliza tatizo la madawati katika shule zote.
Kwa
mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu wakati wa kuahirisha Bunge la 11, takwimu
zinaonesha hadi kufikia Juni 17, mwaka jana, tayari kulikuwa na madawati mapya
552,630 ambayo yamepatikana kwa njia ya michango mbalimbali na hivyo kufanya
shule za msingi kuwa na madawati 2,632,392 sawa na asilimia 77 ya mahitaji na
sekondari zikifikisha madawati 1,395,138 sawa na asilimia 93.
Takwimu
hizo zinaonesha kuwa katika shule za msingi bado yanahitajika madawati 792,949
sawa na asilimia 23 na sekondari madawati 112,785 sawa na asilimia saba.
Taarifa ya Waziri Mkuu inasema kuwa halmashauri 25 kutoka mikoa 13 zimeripotiwa
rasmi kukamilisha mahitaji ya madawati ya shule za msingi na halmashauri 46
kutoka mikoa 19 zimekamilisha madawati kwa shule za sekondari.
Katika
hotuba hiyo ya kuahirisha Bunge iliyotolewa siku 13 kabla ya Juni 30, mwaka
jana, ni wazi kuwa mikoa mingine imefanikiwa kukamilisha mradi huo kabla ya
tarehe iliyopangwa na rais.
Hadi
ilipofika Juni 30, mwaka jana, mikoa mbalimbali iliripoti kukamilisha mradi wa
madawati kwa shule za msingi na sekondari, ambapo Jiji la Arusha likiwa
limepitiliza lengo kwa kuwa na madawati ya ziada 180.
Hatua
hiyo iliungwa mkono na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za umma, mashirika na
sekta binafsi kwa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa kutekeleza sera ya
elimu bure kwa vitendo.
Mbali
na hilo, pia Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini naye aliunga mkono kazi hizo kwa
kutoa madawati 10,000 ambayo alimkabidhi Rais Dk. John Magufuli kama mkakati
wake wa kuinua elimu nchini.
Uchunguzi
uliofanywa na Jamvi la Habari umeonyesha kwamba hadi kufikia mwezi wa tisa
mwaka huu, lengo la upatikanaji wa madawati kwa shule zote hapa nchini lilikuwa
limetimia kwa wastani wa asilimia 92.5.
Maabara
Uhamasishwaji wa ujenzi wa Maabara za sayansi shuleni ulioonekana
kupokelewa kwa mikono miwili na kuanza kutekelezwa kwa kuwahusisha wananchi,
serikali, halimashauri na wadau wa maendeleo unaonyesha kuchagiza uimara wa
mfumo wa elimu nchini na kuzidi kummwagia sifa Rais Magufuli.
Tangu ameingia madarakani, Rais amekuwa akiwaagiza
wasaidizi wake hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule
unaenda sambamba na uwepo na maabara za sayansi kwa ajili ya wananfunzi
kujifunzia na madawati ili kufikia lengo la Tanzania ya viwanda.
Elimu ya Ufundi
Idara nyingine katika mfumo wa elimu inayopigiwa mstari wa
mfano ni uimarishaji wa elimu za ufundi katika maeneo mbalimbali hapa nchini
kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
Katika hotuba na nukuu mbalimbali za kielemu ambazo
anazitoa waziri wa elimu na watendaji wa wizara hiyo, ni pamoja na uchagizwaji na uboreshaji wa vyuo vya
ufundi kama vile Veta ambavyo kwa mujibu wa sera na mipango ya serikali ni
kwamba inahitajika kuwepo angalau chuo kimoja cha ufundi katika kila wilaya,
jambo ambalo limeonyesha kufanikiwa kwa kasi baada ya maeneo mengi nchini
kuendelea kujenga vyuo hivyo au kubadili matumizi ya baadhi ya shule ama
taasisi au majengo na kuyageuza kuwa vyuo vya elimu za ufundi.
Elimu ya Juu
Pamoja na maboresho mbalimbali yanayoonekana kufanyika
katika mfumo wa elimu hasa elimu ya msingi na sekondari,
Kadharika serikali ya awamu ya tano imeonyesha kuwepo kwa
mapinduzi makubwa baada ya Rais kuendelea kufanya mambo kadhaa kwa moyo na
upendo wa dhati.
Ujenzi wa mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar
es salaam katika eneo la barabara ya Sam Nujoma, kurudisha mfumo wa udahili wa
wanafunzi ambapo sasa mwanafunzi anaomba moja kwa moja katika chuo husika tena
kwa kulipa shilingi elfu kumi tu tofauti na hapo nyuma na kuimarishwa kwa
upatikanaji wa mikopo kwa wananfunzi wanaostahili tena kwa wakati kumefanya
wanafunzi wengi kumpongeza Rais Magufuli na kumtaka aendelee na moyo huo huo na
kwamba wao wataendelea kumuombea kwa Mungu.
‘’mimi nimeanza chuo mwaka jana hapa Udom, kwa kweli
sijawahi kupata tatizo lolote hasa kuhusiana na upatikanaji wa mkopo japo mimi
nilidahiliwa na TCU, ila napongeza zaidi mfumo wa udahili wa sasa’’. Anasema
Hanssy Kibiki mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma
Kadharika, akiongea na gazeti hili Johnson Maliyamungu ambaye
ni mwanafunzi mteule wa chuo kikuu cha Dar es salaam kampasi ya Mlimani
akisomea masuala ya uchumi na biashara anasema ‘’ unajua huko sekondari
tulikuwa tunajiandaa kujan chuo kikuu hasa hapa mlimani kugoma…akili zetu
zilijiandaa kisaikolojia kwamba huko chuoni tusipotimiziwa mahitaji yetu ni
mgomo tu, lakini kwa hii spidi ya serikali yetu wala hatuna sababu ya kugoma
tena, Mabweni yamejengwa, mikopo tunapatiwa kwa wakati na juzi tu hapa Rais
kasema ameshatoa bilioni 147 kwa ajili yetu, sasa yanini tugome?’’. Alinukuliwa
Malyamungu
Mimba
shuleni
Katika
kuonyesha kuwa hana utani na elimu kwa wananchi anaowaongoza na kwamba anataka
watanzania wote wanaostahili kusoma wasome bila kujihusisha na vitendo visivyo
vya kiuwanafunzi,
akiwa
katika ziara yake mkoani Pwani hivi karibuni, Rais Magufuli alitoa msimamo
mkali kuhusu wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni na kusema katika muda
wote atakaokuwa madarakani, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari
atakayepata ujauzito atakayeruhusiwa kuendelea na masomo katika shule za umma.
Akisisitiza
msimamo wake wa kukataa shule za umma kupokea wanafunzi wanaopata mimba wakiwa
katika masomo, rais aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO)
yanayowatetea kuanzisha shule kwa ajili yao.
“Nataka
niwaambie, katika utawala wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakayerudi
shuleni. Yapo mambo mengi ya kufanya, wanaweza kwenda Veta au wakajifunza
kushona, maisha yakaendelea,” alisema Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na
wananchi wa Bagamoyo wakati wa uzinduzi wa barabara ya Bagamoyo- Msata.
“Haiwezekani
Serikali ikawa inatenga Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure
halafu wanafunzi wanakwenda kufanya mambo ya ovyo. Hatuwezi kulipeleka Taifa
hili katika maadili ambayo hayapo. Hizi NGO zinapata fedha nyingi zikafungue
shule za wazazi, sisi tutazisajili lakini si watoto waliozaa warudi shule,”
alisema.
Uingereza
yakunwa
Sera
ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini imeigusa
Serikali ya Uingereza na hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania
katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo, ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano
uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Agosti
mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Dk. Augustine Mahiga, alieleza hayo alipokuwa akizungumzia ziara ya Waziri wa
Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola
na Idara ya Ushirikiano katika Maendeleo ya Kimataifa.
Balozi
Mahiga alisema Uingereza ni ya pili miongoni mwa wahisani wanaotoa misaada ya
kimaendeleo ikiifuatiwa na Benki ya Dunia (WB).
“Serikali
ya Uingereza ni moja ya nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini katika biashara,
viwanda na sekta binafsi. Pamoja na kuwa zipo nchi nyingi zaidi
tunazoshirikiana nazo kibiashara, Uingereza ni miongoni mwa nchi tano
zinazowekeza zaidi nchini,” alisema Balozi Mahiga.
Aliongeza
kuwa mbali na ushirikiano uliopo baina ya Serikali za nchi hizo mbili,
Uingereza imeendelea kushirikiana na baadhi ya Mashirika yasiyokuwa ya
Kiserikali (NGO’s), Sekta ya Afya, Elimu na mahusiano baina ya watu na watu.
Kwa
upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anyeshughulikia Masuala ya
Afrika, Jumuiya ya Madola na Idara ya Ushirikiano katika Maendeleo ya
Kimataifa, Rory Stewart, amesema amefurahi kuja Tanzania na kupata fursa ya
kutembelea baadhi ya shule Dar es Salaam na pia amefurahia Sera ya Elimu bure
inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Mgufuli.
Waziri
Stewart alisema kutokana na kuridhishwa na Sera hiyo, Serikali ya Uingereza
itatoa msaada wa pauni milioni 140 za Uingereza kwa lengo la kusaidia
katika sekta ya elimu ili kuboresha miundombinu muhimu katika sekta hiyo.
“Nimeridhishwa
na Sera ya Serikali ya Elimu bure na kutokana na mwitikio mkubwa wa wazazi
kuwapeleka watoto shule hali inayopelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya
wanafunzi, tumeona nasi tushiriki katika kuboresha sekta hiyo,” alisema
Waziri Stewart.