DKT. KIGWANGALLA AMWAGA CHECHE, AFUTA UTARATIBU WA
UTOAJI WA VIBALI VYA UWINDAJI WA KITALII, AAPA KUTOYUMBISHWA NA RUSHWA
NA FITNA
NA HAMZA TEMBA - WMU - DODOMA
.............................. .............................. .......................
Katika
kile alichoeleza kuwa ni kuimarisha sekta ya maliasili na utalii iweze
kutoa mchango unaostahili kwa jamii na taifa kwa ujumla, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesitisha utaratibu wa
kuhuisha upya vibali vyote vya makampuni ya uwindaji wa kitalii ambavyo
vilitolewa mwaka huu mwezi Januari ili kupisha utaratibu mpya wa utoaji
wa vibali hivyo kwa njia ya mnada.
Dk.
Kigwangalla ametangaza uamuzi huo jana mjini Dodoma katika mkutano
alioutisha wa wadau wa sekta ya maliasili na utalii ambao ulilenga
kukusanya maoni, kero na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili
sekta hiyo muhimu nchini kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi wa haraka.
“Kwa
mamlaka niliyopewa na sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009,
nimeamua bila kushawishiwa na mtu yeyote yule wala kushauriwa na mtu
yeyote yule zaidi ya kusikiliza tu ushauri wa kitaalamu na ushuari wa
ndugu yangu Mhe. Naibu Waziri, lakini sasa hivi ninavyotamka haya
sijamshirikisha mtu yeyote yule, nimeamua kwa mamlaka yangu, nasitisha
vibali vyote vya uwindaji wa makampuni ambavyo vilitolewa mwaka huu
mwezi Januari kwa maana ya ‘kurenew’ (kuhuisha).
“Nasitisha
ili kupisha mchakato wa kutengeneza taratibu mpya za kuendesha ugawaji
wa vitalu kwa njia ya mnada, tunataka twende kwenye ‘auction’ (mnada) ya
vitalu, na auction (mnada) iwe ya wazi, iwe na faida kubwa zaidi, na
natoa siku sitini utaratibu huo uwe umekamilika ili tuweze kuendesha
‘auction’ (mnada) kabla ya muda wa kuanza kwa awamu ya miaka mitano
ambayo ni january 2018 mpaka 2022.
“Kwahiyo
ndani ya siku sitini, wataalam mkae mniletee utaratibu wa namna bora
zaidi ya uwazi inayotoa haki ya kugawa vitalu lakini pia yenye faida
kubwa zaidi kama tunavyoelekezwa na mpango wa taifa wa miaka mitano
kwamba ni lazima vitalu vyote vifanyiwe ‘auction’ (mnada)”. alisema Dk.
Kigwangalla.
Alisema
utaratibu huo hautahusisha vitalu vilivyopo kwenye maeneo yenye migogoro
ya ardhi kwa sasa mpaka pale migogoro hiyo itakapomalizika.
“Ni
mwiko kugawa vitalu kwenye maeneo yenye mgogoro, kuna maeneo kama
vitalu vilivyopo Loliondo, kuna mgogoro, ni mwiko kugawa vitalu, kuna
maeneo kama Lake Natron kuna mgogoro, mwiko kugawa vitalu, mpaka tutatue
migogoro kwanza, Kama kuna mtu alipewa kibali huko nyuma ajue hicho
kibali cha renewal kimekufa leo na mimi ndio nimekiua” alisema Dk.
Kigwangalla.
Kuhusu
uwindaji wa Wenyeji kwenye maeneo ya wazi uliosimamishwa kwa muda wa
miaka miwili sasa, Dk. Kigwangalla alitoa muda wa siku sitini kwa
watendaji wa wizara yake kukamilisha masharti mapya ya uendeshaji wa
biashara hiyo na kuyawasilisha kwake aweze kuyasaini ili kufungulia
biashara hiyo.
“Natoa
siku sitini, wataalam wetu mnaohusika na utoaji wa vibali vya uwindaji
wa wenyeji mkamilishe masharti mapya mniletee nisaini tutoe vibali,
hatuwezi kuzuia wenyeji wanufaike na rasilimali ambazo ziko huko
vijijini alafu tukaruhusu makampuni ya watu kutoka nje kuja kuwinda
wakaondoka na nyama, ni lazima tutoe haki kwa wazawa kama wapo
wanaovunja masharti sisi tudhibiti na tusimamie sheria” alisema Dk.
Kigwangalla.
Wakati huo
huo, Waziri Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Mej. Jen. Gaudence Milanzi kuwasiliana na Msajili wa Hazina kwa
ajili ya kuanza mchakato wa kuzirudisha serikalini hoteli za kitalii
kumi zilizobinafsishwa miaka 1990 kufuatia kushindwa kutimiza masharti
ya mkataba wa uendeshaji.
“Niagize
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii uwasiliane na mamlaka ambayo ina
dhamana ya kushikilia mali zilizokuwa za Serikali ambazo ziliuzwa kwa
maana ya msajili wa hazina, umueleze nimetoa agizo kwamba hizi hoteli
zote ambazo zimekiuka masharti na hivyo kuathiri utendaji wa sekta ya
utalii nchini na hivyo kuathiri uchumi mpana wa taifa letu, zichukuliwe
na zirudi kuwa mali ya serikali ili serikali ipate fursa ya kuzitangaza
upya na kutafuta waendeshaji wapya watakaoweza kuendesha hoteli hizi
kwa tija na ufanisi kwa maana ya kukuza sekta ya utalii ambayo
inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.
“Nimetoa
agizo hoteli hizi 10 ambazo zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya
mauziano, mchakato wa kuzirudisha Serikalini uanze mara moja na
ukamilike ndani ya siku sitini.
Alisema
kumekuwepo na changamoto kubwa ya uhaba wa vyumba katika sekta ya
utalii hali iliyosababishwa na ubinafsishaji wa hoteli 17 za Serikali
uliofanywa miaka 1990 kwa nia njema ya kuimarisha usimamizi na
uendeshaji wa hoteli hizo kupitia sekta binafsi lengo ambalo
halikufikiwa kwa baadhi ya hoteli hizo.
“Baada
ya kufanya uchunguzi katika hoteli zote 17 tulizouza ni saba tu
zinafanya vizuri, hoteli zinazofanya vizuri na zimekidhi masharti yote
ambayo yalikuwepo kwenye ile mikataba ni Kilimanjaro Hotel, Kunduchi
Beach Hotel, Mt. Meru Hotel, New Africa Hotel, New Safari Hotel, Mafia
Highland Hotel na Hotel 77.
“Hoteli
10 zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya mauziano na mwaka
ulioisha Serikali ilifanya uchunguzi kwenye hoteli nyingine nne kati ya
hizo 10 ambazo ni Robo Wildlife Lodge, Seronera Wildlife Lodge,
Ngorongoro Wildlife Lodge na Lake Manyara Hotel, na zote zilionesha zipo
chini ya kiwango na hazikidhi mahitaji.
“Kwa
kuwa watu hawa wamekiuka masharti ya ubinafsishaji kama walivyopewa
wakati wananunua hizo hoteli ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuvunja
hii mikataba kuzichukua hizi hoteli na kuzibinafsisha kwa watu wengine
watakaoweza kuziendesha kwa faida lakini pia kuziendesha kwa tija zaidi”
alisema Dk. Kigwangalla.
Awali
akijibu baadhi ya hoja za wadau wa mkutano huo kuhusu wizara yake kuwa
na vishawishi vingi vya rushwa na fitna ambazo husababisha viongozi
wengi kutodumu kwenye nafasi zao, Dk. Kigwangalla alisema kamwe
hatoruhusu hali hiyo ijitokeze kwa kuwa hata aliyemteua anamjua vizuri
kuwa ni muarobaini wa changamoto hizo.
“Mimi
nipo hapa kwenye hiki kiti, na nitakuwepo kama sababu ni hiyo ya
maslahi, Mimi sihongeki, sinunuliki, na sishawishiki, najua hata
aliyeniweka hapa ananijua vizuri, kwahiyo alivyoniweka hapa alishajua
hii ni dawa, muarobaini.
“Watu
wote humu ndani tuna njaa, lakini njaa yangu nabaki nayo mwenyewe, bora
nife kwa heshima zangu kuliko kuaibika na kudharaulika kwa kuchukua
rushwa ama kwa kutokutenda haki ama kwa kumuonea mtu.
“Hilo
nina uhakika nalo, kwa maana ya rushwa, maslahi ya kibiashara hapana,
hutonikuta mimi huko, na kama kuna mdau mmoja anadhani kuna siku
anafkiria anaweza kuja kuongea na mimi kwa maslahi binafsi akaweka mbele
mazingira ya rushwa, sana sana ataona nimemuaga na kikao chetu
kimeishia hapo, kwahiyo ukija kwangu njoo na ishu ambayo ipo straight
maslahi ya umma yapo ndani yake utaraibu wa kisheria upo”. Alisema Dk.
Kigwangalla.
Miongoni mwa
maagizo mengine aliyoyatoa kwenye kikao hicho kwa watendaji wa wizara
yake ni kuandaa taratibu za kuanzishwa kwa mwezi maalumu wa kuadhimisha
utamaduni wa Mtanzania (Tanzania Heritage Month), Makumbusho ya Marais
wa Tanzania (Presidential Museum) na Utalii wa Mabasi kwa Miji ya Dar es
Salaam na Arusha (Dar Bus Tour/ Arusha Bus Tour) ili kurahisisha utoaji
wa huduma kwa watalii katika miji hiyo.
Katika
mkutano huo wadau wa maliasii na utalii walipata fursa ya kutoa maoni,
mapendekezo ushauri na kero mbalimbali wanazokumbana nazo katika sekta
hiyo ambazo ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na Waziri
Kigwangalla. Miongoni mwa ushauri na mapendekezo waliyotoa ni pamoja na
kuanzishwa kwa mamlaka moja inayosimamia rasilimali za misitu nchini na
kufunguliwa kwa biashara ya kusafirisha viumbe hai nje ya nchi.
Mkutano
huo wa siku moja ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili
ambao ni Naibu Waziri, Mhe. Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Mej. Jen.
Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, Wakurugenzi wa
Idara na Wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.
Wengine
ni wadau zaidi ya 200 kutoka sekta mbalimbali ya maliasili na utalii
ambao ni wawakilishi kutoka vikundi, taasisi, vyama na vyombo mbalimbali
vinavyoshughulika na utoaji wa huduma katika sekta ya utalii,
wanyamapori, misitu na nyuki pamoja na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment