WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Monday, October 30, 2017

NI HISTORIA MIAKA MIWILI YA JPM NA ELIMU

Na MWANDISHI WETU

NI historia na msimamo mkali. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya Rais Dk. John Magufuli kuisimamia kwa vitendo sera ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wa ndani zikiwamo taasisi za umma na sekta binafsi zilitangaza kumuunga mkono, huku Serikali ya Uingereza ikivutiwa na mpango huo.
Hatua hiyo inatajwa kama njia ya mafanikio kwa Rais Dk. Magufuli ambaye Novemba 5, mwaka huu anatimiza miaka miwili madarani, huku akitajwa kama shujaa aliyedhamiria kuinua elimu kwa vitendo.

Kitendo cha Rais kutamka hadharani kuwa serikali yake anayoiongoza haitawalipisha ada, gharama za mitihani na michango mingineyo iliyokuwa inawakwaza wazazi na walezi wa wanafunzi  hasa wanyonge na masikini kwa kueleza kutengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 18.7 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia mfumo na sera ya elimu bure hapa nchini.

Kadharika, kuasisiwa huko kwa utaratibu huu wa elimu bure kumesababisha kuwepo kwa mafanikio makubwa katika usajili na uandikishwaji wa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza baada ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi waliofikisha umri wa kwenda shule na kujiunga katika mikoa mbalimbali ya sehemu kubwa ya nchi

‘’kwetu sisi hakika tumevuka malengo na matarajio, wakati rais anatuagiza kutekeleza mfumo huu wa elimu bure hatukutarajia kama muitikio ungekuwa mkubwa kiasi hiki…kwa kweli mfumo huu wa elimu bure umesababisha watu wengi zaidi wawaandikishe watoto shule na hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kuwepo kwa watoto wasiojua kusoma na kuandika katika siku zijazo’’. Alinukuliwa Mtela Mwampamba, Katibu tawala wa wilaya ya Kisarawe.

Aidha akizungumza na gazeti hili mkazi wa Morogoro kihonda Aziza Matiga Malinda amempongeza Rais kwa msimamo wake wa kutoa elimu bure kwa kuzingatia ukweli kwamba unasaidia kuondoa matabaka baina ya watanzania na watu wote wenye sifa za kwenda shule sasa watakuwa wanakwenda shule bila kikwazo wala kizingiti cha ada akitolea mfano yeye anavyoweza kuwasimamia watoto wake watatu kwenda sekondari huku yeye gharama zake zikiwa ni utekelezaji wa majukumu mengine kama mzazi na si ada wala michango ya shuleni.

‘’Unaona mimi ninasomesha watoto watatu hapo, mmoja kidato cha pili na mwingine cha tatu na mmoja darasa la sita, sasa kwa hali yangu hii ningeweza kweli kuwalipia ada na michango mingine hawa watoto wote?..kwa kweli namshukuru sana Mungu kwa kutuletea Rais huyu mwenye Huruma’’. Alisema Aziza

Madawati

Katika kile kinachoonekana kufanikiwa kwa elimu bure kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, wakuu wa mikoa na wilaya wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutimiza agizo la mkuu huyo wa nchi la kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha wanafunzi wanasomea katika mazingira bora.

Mapema mwaka jana, Rais Magufuli aliteua wakuu wapya wa mikoa na baada ya kuapishwa aliwaambia vigezo atakavyotumia kuwapima ni pamoja na kushughulikia tatizo la upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuimarisha mazingira ya shule na kufanikisha sera ya kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.

Rais aliwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana wawe wamelimaliza tatizo la madawati katika shule zote.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu wakati wa kuahirisha Bunge la 11, takwimu zinaonesha hadi kufikia Juni 17, mwaka jana, tayari kulikuwa na madawati mapya 552,630 ambayo yamepatikana kwa njia ya michango mbalimbali na hivyo kufanya shule za msingi kuwa na madawati 2,632,392 sawa na asilimia 77 ya mahitaji na sekondari zikifikisha madawati 1,395,138 sawa na asilimia 93.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa katika shule za msingi bado yanahitajika madawati 792,949 sawa na asilimia 23 na sekondari madawati 112,785 sawa na asilimia saba. Taarifa ya Waziri Mkuu inasema kuwa halmashauri 25 kutoka mikoa 13 zimeripotiwa rasmi kukamilisha mahitaji ya madawati ya shule za msingi na halmashauri 46 kutoka mikoa 19 zimekamilisha madawati kwa shule za sekondari.

Katika hotuba hiyo ya kuahirisha Bunge iliyotolewa siku 13 kabla ya Juni 30, mwaka jana, ni wazi kuwa mikoa mingine imefanikiwa kukamilisha mradi huo kabla ya tarehe iliyopangwa na rais.

Hadi ilipofika Juni 30, mwaka jana, mikoa mbalimbali iliripoti kukamilisha mradi wa madawati kwa shule za msingi na sekondari, ambapo Jiji la Arusha likiwa limepitiliza lengo kwa kuwa na madawati ya ziada 180.

Hatua hiyo iliungwa mkono na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za umma, mashirika na sekta binafsi kwa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa kutekeleza sera ya elimu bure kwa vitendo.

Mbali na hilo, pia Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini naye aliunga mkono kazi hizo kwa kutoa madawati 10,000 ambayo alimkabidhi Rais Dk. John Magufuli kama mkakati wake wa kuinua elimu nchini.

Uchunguzi uliofanywa na Jamvi la Habari umeonyesha kwamba hadi kufikia mwezi wa tisa mwaka huu, lengo la upatikanaji wa madawati kwa shule zote hapa nchini lilikuwa limetimia kwa wastani wa asilimia 92.5.

Maabara

Uhamasishwaji wa ujenzi wa Maabara za sayansi shuleni ulioonekana kupokelewa kwa mikono miwili na kuanza kutekelezwa kwa kuwahusisha wananchi, serikali, halimashauri na wadau wa maendeleo unaonyesha kuchagiza uimara wa mfumo wa elimu nchini na kuzidi kummwagia sifa Rais Magufuli.

Tangu ameingia madarakani, Rais amekuwa akiwaagiza wasaidizi wake hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule unaenda sambamba na uwepo na maabara za sayansi kwa ajili ya wananfunzi kujifunzia na madawati ili kufikia lengo la Tanzania ya viwanda.

Elimu ya Ufundi
Idara nyingine katika mfumo wa elimu inayopigiwa mstari wa mfano ni uimarishaji wa elimu za ufundi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.

Katika hotuba na nukuu mbalimbali za kielemu ambazo anazitoa waziri wa elimu na watendaji wa wizara hiyo, ni pamoja  na uchagizwaji na uboreshaji wa vyuo vya ufundi kama vile Veta ambavyo kwa mujibu wa sera na mipango ya serikali ni kwamba inahitajika kuwepo angalau chuo kimoja cha ufundi katika kila wilaya, jambo ambalo limeonyesha kufanikiwa kwa kasi baada ya maeneo mengi nchini kuendelea kujenga vyuo hivyo au kubadili matumizi ya baadhi ya shule ama taasisi au majengo na kuyageuza kuwa vyuo vya elimu za ufundi.

Elimu ya Juu
Pamoja na maboresho mbalimbali yanayoonekana kufanyika katika mfumo wa elimu hasa elimu ya msingi na sekondari,
Kadharika serikali ya awamu ya tano imeonyesha kuwepo kwa mapinduzi makubwa baada ya Rais kuendelea kufanya mambo kadhaa kwa moyo na upendo wa dhati.

Ujenzi wa mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam katika eneo la barabara ya Sam Nujoma, kurudisha mfumo wa udahili wa wanafunzi ambapo sasa mwanafunzi anaomba moja kwa moja katika chuo husika tena kwa kulipa shilingi elfu kumi tu tofauti na hapo nyuma na kuimarishwa kwa upatikanaji wa mikopo kwa wananfunzi wanaostahili tena kwa wakati kumefanya wanafunzi wengi kumpongeza Rais Magufuli na kumtaka aendelee na moyo huo huo na kwamba wao wataendelea kumuombea kwa Mungu.

‘’mimi nimeanza chuo mwaka jana hapa Udom, kwa kweli sijawahi kupata tatizo lolote hasa kuhusiana na upatikanaji wa mkopo japo mimi nilidahiliwa na TCU, ila napongeza zaidi mfumo wa udahili wa sasa’’. Anasema Hanssy Kibiki mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma

Kadharika, akiongea na gazeti hili Johnson Maliyamungu ambaye ni mwanafunzi mteule wa chuo kikuu cha Dar es salaam kampasi ya Mlimani akisomea masuala ya uchumi na biashara anasema ‘’ unajua huko sekondari tulikuwa tunajiandaa kujan chuo kikuu hasa hapa mlimani kugoma…akili zetu zilijiandaa kisaikolojia kwamba huko chuoni tusipotimiziwa mahitaji yetu ni mgomo tu, lakini kwa hii spidi ya serikali yetu wala hatuna sababu ya kugoma tena, Mabweni yamejengwa, mikopo tunapatiwa kwa wakati na juzi tu hapa Rais kasema ameshatoa bilioni 147 kwa ajili yetu, sasa yanini tugome?’’. Alinukuliwa Malyamungu

Mimba shuleni
Katika kuonyesha kuwa hana utani na elimu kwa wananchi anaowaongoza na kwamba anataka watanzania wote wanaostahili kusoma wasome bila kujihusisha na vitendo visivyo vya kiuwanafunzi,
akiwa katika ziara yake mkoani Pwani hivi karibuni, Rais Magufuli alitoa msimamo mkali kuhusu wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni na kusema katika muda wote atakaokuwa madarakani, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari atakayepata ujauzito atakayeruhusiwa kuendelea na masomo katika shule za umma. 

Akisisitiza msimamo wake wa kukataa shule za umma kupokea wanafunzi wanaopata mimba wakiwa katika masomo, rais aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yanayowatetea kuanzisha shule kwa ajili yao.

“Nataka niwaambie, katika utawala wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakayerudi shuleni. Yapo mambo mengi ya kufanya, wanaweza kwenda Veta au wakajifunza kushona, maisha yakaendelea,” alisema Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi wa Bagamoyo wakati wa uzinduzi wa barabara ya Bagamoyo- Msata. 

“Haiwezekani Serikali ikawa inatenga Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure halafu wanafunzi wanakwenda kufanya mambo ya ovyo. Hatuwezi kulipeleka Taifa hili katika maadili ambayo hayapo. Hizi NGO zinapata fedha nyingi zikafungue shule za wazazi, sisi tutazisajili lakini si watoto waliozaa warudi shule,” alisema. 

Uingereza yakunwa
Sera ya elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini imeigusa Serikali ya Uingereza na hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo, ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Agosti mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alieleza hayo alipokuwa akizungumzia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Idara ya Ushirikiano katika Maendeleo ya Kimataifa.

Balozi Mahiga alisema Uingereza ni ya pili miongoni mwa wahisani wanaotoa misaada ya kimaendeleo ikiifuatiwa na Benki ya Dunia (WB).

 “Serikali ya Uingereza ni moja ya nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini katika biashara, viwanda na  sekta binafsi. Pamoja na kuwa zipo nchi nyingi zaidi tunazoshirikiana nazo kibiashara, Uingereza ni miongoni mwa nchi tano zinazowekeza zaidi nchini,” alisema Balozi Mahiga.

Aliongeza kuwa mbali na ushirikiano uliopo baina ya Serikali za nchi hizo mbili, Uingereza imeendelea kushirikiana na baadhi ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s), Sekta ya Afya, Elimu na mahusiano baina ya watu na watu.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anyeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Idara ya Ushirikiano katika Maendeleo ya Kimataifa, Rory Stewart, amesema amefurahi kuja Tanzania na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya shule Dar es Salaam na pia amefurahia Sera ya Elimu bure inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Mgufuli.

Waziri Stewart alisema kutokana na kuridhishwa na Sera hiyo, Serikali ya Uingereza itatoa msaada wa pauni milioni  140 za Uingereza kwa lengo la kusaidia katika sekta ya elimu ili kuboresha miundombinu muhimu katika sekta hiyo.

“Nimeridhishwa na Sera ya Serikali ya Elimu bure na kutokana na mwitikio mkubwa wa wazazi kuwapeleka watoto shule hali inayopelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi, tumeona nasi tushiriki katika kuboresha sekta hiyo,”  alisema Waziri Stewart.

No comments:

Post a Comment