WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Sunday, August 27, 2017

USALAMA ASILIMIA 100 KIBITI

Viongozi na wananchi waliolazimika kukimbia Kibiti baada ya kuwapo na matukio ya kila mara ya kuuawa kwa wenzao huku wahalifu wa unyama huo wakiwa hawafahamiki, wameendelea kurejea katika maeneo yao baada ya hali ya usalama kuendelea kuimarika siku baada ya siku imefahamika.

kuimarika huko kwa hali ya usalama katika siku za hivi karibuni kulikotokana na operesheni mbalimbali zinazoendelea kufanywa na vyombo vya kulinda usalama wa raia na mali zao kumewapa imani wengi wao ambao sasa wameanza kurejea, ingawa imefahamika kuwa kasi ya kurudi kwa baadhi yao imekuwa ni ya kuvizia, kuashiria kuwa wapo ambao bado wamejawa na wasiwasi.

Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Alvela Ndabagoye, alisema kuwa baada ya ombi lake la wiki iliyopita la kuwataka viongozi na watendaji kurejea kazini ili waendelee kutoa huduma kwa wananchi, sasa hali imekuwa ya kutia moyo kwa sababu wengi wameitikia wito huo na kurejea.

"Tumefanikiwa kuwarejesha (watendaji) wote 16 ambao walikimbia ofisi zao kutokana na kuwapo na matukio ya mauaji, hali sasa imekuwa nzuri kwa wananchi kutokana na kuendelea kupata huduma kutoka kwa watendaji hao,'' alisema.

Aliongeza kuwa, watendaji hao walimwelewa na wakakubali kurudi katika vituo vyao vya kazi na hivi sasa wanaendelea kutoa huduma kama kawaida.

Mkurugenzi huyo alisema pamoja na kurejea kazini, bado baadhi ya watendaji wana wasiwasi kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa muda mfupi na kurejea nyumbani.

Alisema pamoja changamoto za kiusalama zilizokuwapo katika wilaya hiyo, watumishi wa kada zingine waliendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Wiki iliyopita katika kikao cha robo mwaka cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Kibiti na kuhudhuriwa na madiwani, wakuu wa idara pamoja na wananchi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Milongo Sanga aliwaondoa hofu watendaji wa vijiji na kuwataka warejee ofisini kwao ili kuendelea kutoa huduma kwa jamii kutokana na hali ya kiusalama kuimarika.

"Tunawaomba wenyeviti wa vijiji warudi kazini kuendelea na utoaji wa huduma kwa wananchi kwani kwa sasa hali ya Kibiti imeimarika na hakuna matatizo yoyote," alisema Sanga.
Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, zilikumbwa na mauji mfululizo ya kikatili lakini hivi karibuni, jeshi la polisi lilitangaza kuwa usalama umeimarika na sasa wananchi wanapaswa kuendelea na shughuli zao bila hofu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alitangaza vilevile kuwa Polisi imewaua watu 13 wanaohusishwa na mauaji hayo wakati wakiwa katika harakati za kuwadhibiti.

Katika tukio mojawapo la mauaji yanayoendelea eneo hilo, askari polisi wanane waliokuwa kwenye gari wakitoka lindo waliuawa kwa risasi Aprili 13 mwaka huu walipofika eneo la Mkengeni. Kata ya Mjawa Wilaya ya Kibiti.

Katika tukio hilo, majambazi hao walipora bunduki saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.

Katika tukio hilo askari mmoja alijeruhiwa na baadaye polisi walitangaza kuua wahalifu wanne waliodaiwa kuwa majambazi baada ya kubaini maficho ya muda katika majibizano ya risasi.

Zawadi ya Sh. milioni 10 ilitangazwa na IGP Sirro kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.

Kabla ya kutangazwa kwa zawadi hiyo ya IGP, Polisi mkoani Pwani ilikuwa imetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa mwananchi yeyote ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 wa mauaji ambao ilidaiwa hujihusisha na mtandao wa mauaji hayo.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Sanga Lyanga, aliwaambia waandishi wa habari Mei 22, kuwa jeshi hilo limepata picha za baadhi ya watuhumiwa na fununu za mahali wanapopenda kutembelea mara kwa mara.

Kamishina Lyanga aliwataja watuhumiwa hao pamoja na mwanzilishi wa mtandao huo wa mauwaji kuwa ni Abdulshakur Ngande Makeo, Faraja Ismail Nangalava, Anaf Rashid Kapera, Said Ngunde na Omary Abdallah Matibwa.

Wengine ni Shabani Kinyangula. Haji Utaule, Ally Utaule, Hassan Upinda,Rashid Salim Mtulula,Sheikh Hassan nasr Mzuzuri na hassani Njame.

Mfululizo wa mauji hayo ulianza Mei mwaka jana katika tukio la kupigwa risasi kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Nyambungu, Saidi Mbwana.
Kadharika, hivi karibuni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, amewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama wilaya ya Kibiti na Rufiji ipo shwari. Aidha amesema jeshi la polisi linaendelea na oparesheni mbalimbali za kuwasaka wahalifu wanaochafua mkoa na taifa.
Aliyasema hayo, kufuatia habari zinazoendelea kusemwa na kuandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu mambo yanayoendelea kwenye wilaya hizo. Mhandisi Ndikilo, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi waliopo kwenye oparesheni hiyo na kuacha kukimbia miji yao kama wanajiamini sio wahalifu.

"Kumekua na taarifa zinazoendelea kuandikwa suala ambalo mkoa haujawahi kutoa taarifa zaidi ya tukio la mauaji ya vifo nane iliyotokea april 13 na kukemea usafiri wa pikipiki ifikapo saa 12 jioni " alisema. Alibainisha kwamba, endapo kutakuwa na tukio ama jambo litakalojitokeza serikali ya mkoa, wilaya, jeshi la polisi litatolea ufafanuzi.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama ambae pia ni mkuu wa mkoa huo, alieleza, kuwa sasa vyombo vya dola vinawasaka watu waliojihusisha na mauaji ya wenyeviti wa vijiji, vitongoji na polisi . "Jeshi la polisi ama serikali haiwezi kumwonea mtu yoyote kwani inafanywa kwa kuzingatia sheria"alisema.

Mhandisi Ndikilo alisema jeshi la polisi linafanya kazi yake kwa weledi na kazi yake kubwa ni kulinda amani ya wananchi na mali zao. “Nawaombeni wananchi msiwe na hofu juu ya operesheni hiyo na hakuna haja ya kukimbia makazi yao kwani kuna taarifa kuwa kuna watu wamehama kwenye nyumba zao na kukimbia,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa watu wanaokimbia wanatia mashaka, hawana sababu ya kukimbia nyumba zao na familia zao kwani wanaotafutwa ni wahalifu na si raia wema. Mhandisi Ndikilo, alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili viweze kufanya kazi zake ipasavyo.
Aliwatoa hofu watu wote wanaofanya shughuli zao kwenye wilaya hizo kutokuwa na wasiwasi kwani ulinzi umeimarishwa

No comments:

Post a Comment