Ni katika Mkutano wao mkuu wa
Kidemokrasia kukutanisha wanachama, wananchi na viongozi
Zitto Kabwe Aunguruma, Azungumzia
Uchumi, Kilimo na Demokrasia
Na . Ibrahim Malinda
Zitto Zuberi Kabwe, Kiongozi wa
chama cha ACT WAZALENDO juzi aliwaongoza wanachama wa chama hicho katika
kuazimisha mkutano wao mkuu wa kidemokrasia wa tatu tangu kuanzishwa kwa chama
hicho mkutano uliofanyika mkoani mwanza katika ukumbi wa hotel ya Monarch
iliyopo jijini humo.
Ifuatayo ni hotuba iliyosomwa na
kiongozi huyo wa chama ambaye pia ni mbunge wa jimbo la kigoma mjini.
Ndugu
Watanzania.
Ndugu Wanachama wa Chama cha ACT
Wazalendo na washiriki wa Mkutano wetu wa mwaka wa Kidemokrasia hapa Mwanza.
Nawasalimu kwa salaam za kizalendo
na kuwakaribisha katika Mkutano wetu wa mwaka 2017. Huu ni Mkutano wetu wa pili
wa Kidemokrasia Kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu. Agosti mwaka jana tulikuwa
Dar es salaam katika Mkutano wa Kwanza wa Kidemokrasia, ambapo tulizungumzia
kwa undani juu ya suala la Katiba mpya.
Mwaka huu mwezi Machi tulikuwa na
Mkutano Mkuu wa kidemokrasia maalumu jijini Arusha kuadhimisha miaka 50 ya
Azimio la Arusha, kujadili Ujamaa pamoja na umuhimu wa Azimio la Tabora la
chama chetu linalohuisha Azimio la Arusha. Leo tupo hapa Mwanza katika Mkutano
wa Pili wa Kidemokrasia kuzungumzia umuhimu wa Uhuru wa Fikra, Mawazo na
Misingi ya Demokrasia.
Nina furaha kubwa kwamba pamoja na
upya wa chama chetu tumeweza kuendeleza bila kukosa utekelezaji wa Katiba yetu
kwamba kila mwaka wanachama wawe na nafasi ya kukutana na viongozi wa chama na
wananchi wengine kujadili hali ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Tusiache utamaduni huu kwani ni utamaduni unaoimarisha zaidi Chama na kuweka
karibu Viongozi wa Chama na na wanachama; Chama na wananchi; Chama na wadau
wake mbalimbali.
Mkutano huu wa Demokrasia ni
utaratibu unaotoa fursa ya moja kwa moja kwa wanachama kutuhoji Viongozi wao,
na kushauri juu ya namna njema ya kuendesha siasa zetu. Ni ishara ya kilele cha
Demokrasia ya chama chetu. Nawapongeza Sana wanachama na wananchi wote mlioweza
kushiriki nasi leo. Nawatakia mjadala wa kina na wenye manufaa Kwa nchi yetu na
bara la Afrika.
Mwaka 2015 wakati wa uzinduzi wa
Azimio la Tabora tulizungumza kwenye hotuba ya Tabora kuhusu changamoto ambazo
nchi yetu ilikuwa nazo na inawezekana bado inazo . Katika Hotuba ile ambayo
imechapishwa kwenye andiko la Azimio la Tabora tulianisha, nanukuu
"Wananchi wa Tabora, ndugu Watanzania nchi yetu inakabiliana na changamoto
kubwa nne;
- Uchumi usiozalisha ajira na
kutoondoa umasikini
- Huduma duni za jamii hususan
Elimu, Afya na Maji
- Rushwa na Ufisadi
- Nyufa katika Taifa kutokana na
hisia za udini na ukabila kuanza kushamiri". Mwisho wa kunukuu.
Leo Mwaka 2017, tukitazama nyuma
utaona kuwa hatukuwa na wasiwasi kuhusu Demokrasia na hasa uhuru wa mawazo na
Uhuru wa kufikiri tofauti. Hatukuwa na wasiwasi kuhusu Uhuru wa kukosoa
Viongozi na kutoa maono mbadala.
Miaka 2 baadaye huwezi kuandika
changamoto za Tanzania bila ya kutaja ufinyu wa demokrasia. Hii ni ishara kuwa
tunarudi nyuma. Bahati mbaya ni kwamba baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa ili
kupata Maendeleo ni lazima kuminya Uhuru wa watu. Tunakosea sana, chama chetu
kinaamini kinyume chake.
Demokrasia ni sehemu ya utanzania
wetu. Tulianza na demokrasia ya vyama vingi - tukajaribu demokrasia ya chama
kimoja na kurejea na demokrasia ya vyama vingi. Hivyo nchi yetu ina uzoefu wa
kutosha wa mifumo yote. Historia yetu ni somo tosha la kutufanya tusirudie
makosa ya kuamini katika utawala wa kiimla na utawala wa mtu mmoja.
Wazalendo wenzangu, Katika Ufumaji
wa Taifa (StateCraft) - ni muhimu kutambua utofauti wa kihistoria, kinyakati na
kimuktadha. Huwezi Leo ukasema kuwa Demokrasia Ndio imeturudisha nyuma na hivyo
kutaka kujaribu kuiga mifumo ya nchi nyengine ambazo tunaona zimepiga hatua za
kimaendeleo. China, Singapore, Ethiopia na Rwanda kama mfano wa kuigwa? Hapana.
Kuna mazuri ya kujifunza na kuchukua lakini sio kila kitu kwani modeli za
Maendeleo za nchi hizo zinatokana na historia za maisha yao Kama Taifa na kama
watu wanaounda Taifa hilo.
Nchi zote hizi nilizotaja Kwa mfano
zina historia na muktadha tofauti na Tanzania. Mifumo yao imejengwa kwa mujibu
wa historia zao, muktadha, na uhalisia wa mataifa yao, kisiasa, kijamii,
kiutamaduni na hata kijiografia. Singapore ilijengwa katika muktadha wa vita
vya baridi, ambapo mataifa ya kibepari yalilazimika kuibeba kiuchumi ili
kuepusha ushawishi wa kiitikadi wa Uchina na Urusi. Ethiopia ilijengwa baada ya
kuanguka kwa dola la nchi hiyo na ushindi wa Chama cha Ukombozi cha TPLF, kundi
la Meles Zenawi ambaye alipata nafasi ya kuijenga upya nchi hiyo. Rwanda
ilijengwa kupya baada ya mauaji ya kimbari yaliyosababisha kuanguka kwa dola na
taasisi zote za utawala. Wakaanza upya.
Wazalendo, Tanzania ni tofauti. Tuna
historia endelevu. Tuna dola na taasisi za kihistoria ikiwemo taasisi za
kidemorasia kama vyama vingi na 'bureaucracy' zilizokomaa. Tuna utamaduni na
desturi za utaifa zilizosukwa na kuenziwa kwa weledi mkubwa wa Mwalimu Nyerere
na viongozi waliofuata kwa kupitia Azimio la Arusha.
Tuna historia ya kuthamini misingi
ya demokrasia tangia kupata uhuru wetu. Demokrasia imejengeka kwenye mioyo,
fikra na matamanio ya wananchi. Hatuwezi kuanza upya na hatuhitaji kufanya
hivyo.
Hatua yoyote ya kurejesha nyuma
mchakato wa mfumo wa kidemokrasia zitapelekea athari kubwa za kiuchumi, kisiasa
na kijamii. Ni sawasawa na ile hadithi ya jini lililotoka katika kibuyu chake.
Unapotaka kulazimisha kulirudisha utaishia kuvunja kibuyu.
Wazalendo, tayari tumeanza kuona
madhara hasi ya kuminywa Kwa demokrasia. Kwanza mshikamano uliokuwa umeanza
kujengeka ndani ya nchi bila kujali vyama umeanza kumomonyoka. Kamatakamata ya
Viongozi wa wananchi badala ya kujenga Taifa inabomoa bomoa nyuzi zinazosuka
Utaifa wetu, kujenga chuki na hata kupelekea shughuli za Uchumi kuanza
kuporomoka.
Ukuaji wa sekta ya wananchi wengi,
yaani Kilimo cha Mazao ulikuwa 1.4% tu mwaka 2016 kutoka ukuaji wa 2.2% mwaka
2015 na 4% miaka ya kabla ya hapo. Ukichukua kasi ya ukuaji wa idadi ya watu
Tanzania ya 2.8% kwa mwaka, maana yake ni kwamba Mwaka 2016 Watanzania
tuliongezeka maradufu ya kuongezeka kwa uwezo wetu wa kujilisha. Ina maana
mwaka 2016 Watanzania wengi zaidi walidumbukia kwenye umasikini kuliko mwaka
2015.
Wakati Serikali inaimba Viwanda,
mauzo ya bidhaa zitokanazo na Viwanda kwenda nje ya nchi yetu yameshuka sana.
Mwaka unaoishia Mei, 2016 Tanzania iliuza nje bidhaa za Viwanda za thamani ya
Dola 1.5 bilioni. Mwaka mmoja baadaye yaani mwaka unaoishia Mei, 2017 Tanzania
imeuza nje bidhaa za Viwanda za thamani ya Dola 0.8 bilioni tu. Anguko la mauzo
Nje la takribani Dola 700 milioni sawa na thamani ya Ndege 23 za Bombadier
Q400.
Uagizaji wa bidhaa za chakula kutoka
nje umeongezeka kwa 14% ndani ya mwaka mmoja wa Mei 2016 mpaka Mei 2017 ambapo
Tanzania ilitumia Dola 480 milioni kuagiza vyakula kama Sukari, nafaka na
mafuta ya Mawese. Tumekuwa tegemezi zaidi, tunauza bidhaa kidogo zaidi nje ya
nchi, na tunanunua bidhaa zaidi kutoka nje.
Mauzo ya Nje ya zao la Pamba mwaka
2016 yalikuwa Dola 52 milioni. Mwaka 2017 Mei mauzo yameshuka mpaka Dola 42
milioni. Uagizaji wa bidhaa za kuzalisha bidhaa (capital goods) umeporomoka kwa
25% ndani ya mwaka mmoja kati ya Mei 2016 na Mei 2017. Hali hiyo ya mdororo wa
uchumi iko karibia katika sekta zote za uchumi wa nchi yetu.
Takwimu hizi chache zinaonyesha kuwa
hali ya nchi yetu sio imara na kuna hatari kwamba Watanzania wengi sana
wakadumbukia kwenye umasikini zaidi.
Mwaka huu ndio tumeshuhudia
uminywaji zaidi wa demokrasia na umeendana na kushuka Kwa viashiria vyote vya
uchumi. Demokrasia sio adui wa Maendeleo. Demokrasia ni chachu ya Maendeleo.
Sisi ACT Wazalendo hatukubaliani na hali hii. Tunaamini kinachopaswa kufanywa
ni kusadifu na sio kuikandamiza demokrasia yetu.
Hilo linapaswa kufanyika katika
mfumo unaojenga muafaka wa kitaifa na sio mgawanyiko wa taifa kama
inavyoelekea. Na njia thabiti na sahihi ya mchakato huo ni kupata katiba mpya
itakayokuwa na ushiriki na ridhaa ya watanzania kwa ujumla wao. Tuthubutu
kuenda mbele zaidi na sio kurudi nyuma!
Wazalendo, Yote hayo niliyoyaeleza
yanaonyesha Utamaduni wetu wa kisiasa wa kuonana ni Watanzania bila kujali
itikadi za vyama vyetu nao umetikiswa, sisi si wamoja tena. Msingi wa utamaduni
wetu wa kisiasa hujengwa zaidi kwa mahusiano, matamko na matendo ya viongozi
mbalimbali wa nchi.
Mahusiano, matamko na matendo yetu
viongozi katika nyakati hizi yanaashiria mpasuko tu na yanamomonyoa msingi wa
amani uliojengwa. Kauli za vitisho na vitendo vya bughdha kwa wote
wanaotofautiana mtazamo na watawala ndio vimeshamiri. Yote hayo yameleta athari
kwenye uchumi wetu, yamezuia kupatikana kwa sauti mbadala ya kuleta marekebisho
ya kisera.
Hali hii inaliathiri Taifa, hatua
zifuatazo zichukuliwe kulinda demokrasia yetu na kusukuma mbele Maendeleo yetu:
1. Kwanza ni kwa Viongozi wenzangu,
hasa wale wa chama tawala. Ni muhimu Viongozi tuepuke kugawa watu kwa misingi
ya vyama vya siasa, makabila, kanda na hata dini. Ni muhimu tuache vitisho kwa
wote wanaotumia uhuru wao wa kutoa mawazo mbadala nchini. Ni muhimu tuimarishe
uhuru wetu wa kidemokrasia. Tukishindwa kufanya hayo, uhasama utazidi, mpasuko
utapanuka, wananchi wetu watapoteza matumaini ya kuwa nchi hii ni moja na kila
raia anayo haki (bila kujali tofauti zote za kisiasa, kiuchumi, kidini na
kikabila), na mwishowe nchi hii itapasuka vipande vipande, uchumi wetu kudorora
zaidi na amani yetu kutoweka.
Vyama vya upinzani vinaongoza
Halmashauri zaidi ya 35 nchini, kuzuia mikutano ya hadhara ni uvunjifu wa
katiba lakini pia ni kuondoa uwajibishaji kwa tunaoongoza halmashauri hizo
kutoka kwa CCM ambao ni wapinzani wetu katika maeneo hayo.
Maeneo kama Kigoma Ujiji
tunakoongoza ACT Wazalendo, Arusha Mjini, Mbeya, Iringa nk wananchi wanakosa
sauti mbadala, wanakosa uwajibikaji na fursa ya kupatikana kwa mawazo mbadala
yanayoweza kuendeleza halmashauri hizo. Hali hiyo ni hivyo hivyo kwenye
halmashauri nyengine zinazoongozwa na chama tawala.
2. Kwa wananchi wenzangu, ni muhimu
sana kuendelea kupaza sauti kupinga kubanwa kwa Demokrasia, hatupaswi kabisa
kukaa kimya, huu ni wajibu wetu wa Kizalendo, hatupaswi kuwaachia nchi wahisani
jambo hili. Ndio maana kikao chetu hiki ni muhimu sana, maana kinatupa fursa ya
kujadili tusiyokubaliana mtazamo, kujenga muafaka juu ya tunayoridhiana na
kushirikiana katika yale tunayokubaliana, ndio ujenzi wa Utaifa, ndio
Utanzania. Tunahitaji kuhuisha na kuimarisha utamaduni huu kama tunataka nchi
yetu iendelee kuwa ya amani. Tusiache kupaza sauti juu ya Udikteta.
Njia zetu za kupinga udikteta ni
lazima zilinde amani yetu, hali hii ya kuwa na viongozi wabaya si jambo jipya
duniani, walikuwepo kina Mobutu, Bokassa, Iddi Amin Dada nk, leo hawapo, wakati
tukipinga udikteta ni muhimu kuhakikisha amani ya nchi yetu inabaki, Tanzania
yetu inabaki.
3. Kwa wazalendo, wanachama wenzangu
wa chama cha ACT Wazalendo, tunao wajibu wa kushiriki kujenga Demokrasia ya
nchi yetu kwa kupinga Udikteta nchini, lakini wajibu huo ni lazima uambatane na
kujihusisha na masuala ya watu. Ni lazima tuendelee kujenga chama chetu hata
katika kipindi hiki kigumu, ujenzi huo haupaswi kufanyika mahakamani au jela,
ni lazima tukakijenge kwa watu.
Ni lazima tuendelee kuwasemee
wananchi, ni lazima tujihusishe na masuala ya watu, ni lazima katika sehemu
tunazoongoza tuonyeshe utofauti na wengine, sera nzuri tunazozinadi
tuzitekeleze katika maeneo tunayoyaongoza.
Wazalendo, Demokrasia ni hazina na
sio laana. Inatupa nafasi ya kujuana na kuthaminiana. Inatupa uwezo wa kutambua
mafanikio na mapungufu yetu. Inatoa nafasi kwa mawazo mbadala. Inatuamsha ili
tujisahihishe.
Changamoto tuliyonayo sio mfumo wa
kidemokrasia bali ni ukosefu wa wanademokrasia. Sio misingi ya demokrasia bali
ni ukosefu wa taasisi imara za kidemokrasia. Sio gharama za mahitaji ya
kidemokrasia bali kutambua tija ya siasa za kidemorasia.
Demokrasia hujenga haki. Haki huzaa
amani. Amani huwezesha maendeleo. Tuijenge Demokrasia yetu ili tulete maendeleo
ya nchi yetu.
Nataka niwaache na nukuu ya
mwanaharakati wa kijamaa wa karne 20,Rosa Luxembourg ambaye alisema 'uhuru
kihalisia ni uhuru wa mtu anayefikiri tofauti'.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Mwanza
Agosti 26, 2017
No comments:
Post a Comment