WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Sunday, August 20, 2017

TUHUMA NDEGE BOMBADIER KUZUILIWA: LISSU APUUZWA

 Aumbuliwa kwa matamshi yake ya nyuma

Akumbushwa alivyomkashifu Lowassa na kisha kumsifia

Wanasiasa uchwara watumika kumkwamisha JPM nje ya nchi

Serikali yasisitiza kila kitu kiko sawa, ndege kutua nchini

Na Mwandishi Wetu.

Kitendo cha Mwanasiasa na Mbunge wa Ikungi kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chama hicho Tundu Lissu kuishambulia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na hivi karibuni kuihusisha na kile alichokiita kukwama kwa ndege zilizonunuliwa na serikali ya Tanzania nchini Canada kimemfanya mbunge huyo kupuuzwa na watu makini huku akihusishwa na kufilisika kisiasa.

Akiongea na Gazeti hili Kaimu Mkurugenzi wa muungano wa Taasisi zinazojihusisha na masuala ya utetezi wa Rasilimali, Haki na Utawala wa Sheria uoutwa ULINGO WA KATIBA Bwana Ally Bushiri amesema hakutarajia kuona kama maneno anayoyasikia yangeweza kutamkwa na mwanasiasa huyo aliyejipambanisha kama mtetezi wa wanyonge na mzalendo.

‘’huwezi kujiita Mzalendo ama mtetezi wa wanyonge halafu ushiriki kuihujumu serikali, hata kama inaongozwa na kiongozi usiyempenda kiasi gani, haiwezekani’’. Alisema Bushiri

‘’kila siku Lissu anaibuka na kashfa mpya, na kashfa zote ni kumchafua Rais tu, hata kama anajiandaa kugombea Urais 2020 lakini si kwa mtindo huu….Lissu lazima afahamu kwamba Waziri yeyote yule hapa Tanzania, Afrika na Duniani hana Mamlaka ya Kusaini Mkataba wa kizabuni kama ujenzi, na ndio maana kunakuwa na mamlaka za manunuzi ambazo ni huru na haziingiliwi na taasisi yoyote, na ndio maana Lowassa alipojaribu kuingilia kwenye zabuni ya Richmond alikwenda na Maji’’. Alisisitiza bwana Ally.

Aidha mkurugenzi huyo ameongeza kuwa haikuwa rahisi na isingewezekana kwa kile alichokisema Lissu kuwa Rais Magufuli alipokuwa waziri aliweza kuvunja mkataba na kampuni moja ya kigeni jambo ambalo kisheria waziri hana mamlaka ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba yeye si sehemu ya mkataba wa ujenzi ambayo kwa barabara kubwa hapa nchini husimamiwa na Wakala wa Barabara nchini maarufu kama TANROADS.

‘’Lissu angeweza kusema kuwa sisi kama nchi tunadaiwa, na mmoja kati ya wadeni wetu amekosa uvumilivu ameamua kuchukua hatua kali zaidi, wala haina maana ya ziada kusema tunadaiwa deni lililosababishwa na Fulani, serikali haifanyagi kazi namna hiyo dunia nzima, labda wao Chadema kama ndivyo wanavyoongozana hivyo’’. Alisisitiza

Bushiri aliongeza kuwa Tanzania kwa mujibu wa taarifa za kifedha mpaka sasa inadaiwa zaidi ya Trilioni 40 na kwamba haijaanza kukopa leo wala jana na kamwe haiwezi kuacha kukopa kesho wala kesho kutwa kwa kuwa inafuata taratibu zote za kisheria na kifedha.

‘’Mwalimu Nyerere alikopa na akadaiwa, Mzee Mwinyi naye kakopa, Rais Mkapa alikopa na akadaiwa, Mzee Kikwete naye Kadharika, na wote hawa walikopa na kulipa na kukopa na hata Magufuli amekopa na atalipa na atakopa, sasa shida iko wapi?...Mbona Marekani wanadaiwa, Uingereza Wanadaiwa..nchi zote unazozijua kubwa kwa ndogo hapa uniani zinadaiwa. Alisisitiza

Aidha bwana Bushiri amewataka watanzania kutomkubalia na kumuamini Lissu kwa haraka bila kupima jambo analowaambia kutokana na ukweli kwamba mwanasiasa huyo hachelewi kugeuka na kubadili msimamo wake bila kujali jana amesema nini.

‘’Lissu sio wa kumuamini sana. Leo anaweza kusema hivi kesho vile, ni mjanja mjanja, ndio maana mwaka 2007 Lissu alituambia watanzania tumchukie Lowassa kwa kuwa ni FISADI  lakini mwaka 2015 akatuambia tumchague Lowassa kuwa Rais wa Tanzania vinginevyo tuthibitishe UFISADI wa Lowassa…hivyo anaweza siku moja akatuambia tuthibitishe haya anayoyaropoka leo…ili umuamini Lissu inakubidi uwe na akili kama zake ’’. amenukuliwa Bushiri

Hivi karibuni  serikali imetoa tamko na kueleza kuwa baadhi ya wanasiasa wapo katika mkakati wa kuhujumu mipango ya maendeleo na usalama wa nchi ambao wameshiriki kuchochea kuwekwa zuio la ndege mpya ya kuwasili nchini.

Jamvi la Habari limepata taarifa ya serikali iliyosema kuwa licha ya uwepo wa zuio hilo, hatua  za kidiplomasia  na za  kisheria  zimeanza  kuchukuliwa  ili kulimaliza na ndege hiyo itawasili nchini.

Zuio hilo la mahakama linalodaiwa kuwekwa na kampuni moja ya ujenzi nchini Canada, ikiidai serikali fedha kufuatia kuvunjwa mkataba wa ujenzi wa moja ya barabara iliyokuwa ikijengwa nchini.

Hatua hiyo iliyochochewa na wanasiasa wanaoendeleza hujuma   dhidi ya maendeleo ya nchi, imesababisha ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400, kuzuiwa nchini Canada.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa , Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaiadizi wa Idara ya Habari-Maelezo, Zamaradi Kawawa, alisema serikali inawaomba  Watanzania  kutokuwa  na wasiwasi kuhusu suala hilo.

Alisema serikali ilikuwa na fununu kwamba kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wanaendeleza juhudi za kuhujumu jitihada za Rais Dk. John Magufuli, za kuwaletea Watanzania  hasa wanyonge maendeleo.

“Walikwenda  kufungua madai  kuwa, serikali  inadaiwa  na kwamba ndege  hiyo  ishikiliwe, watu hawa hawana  uhalali wowote  wa kufanya hivyo,  na ni matapeli  ambao wamesukumwa  na baadhi ya viongozi  wa kisiasa  wasioitakia mema  nchi.''alisema

Aliongeza kuwa “Kwa kuwa serikali ilishapata  fununu  kwamba kuna  baadhi ya  viongozi  wa chama  cha siasa  wanampango  huo, sasa  watu hao wamejiridhisha  hadharani,  kwamba wao  ndio wako nyuma  ya pazia  la  kuhujumu  jitihada  za serikali  kwa maslahi yao ya kisiasa,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Zamaradi alisema serikali ya  Dk. Magufuli itawahakikishia  Watanzania  kuwa, ndege  itakuja na wanaokwamisha  jitihada hizo  watapanda ndege hizo na ndugu zao  na wafuasi wao.

Zamaradi alibainisha kuwa, kundi hilo limekuwa likichochea wafadhili wasitishe misaada nchini, wakidhani kufanya hivyo ni kukomoa serikali.

Aliongeza kuwa pia serikali inafununu kwamba watu hao wanaohujumu jitihada za kimaendeleo, wanahujumu hata hali ya usalama wa raia, hivyo inaendelea kufuatilia kwa makini.

“Tunachojifunza kama serikali, hivi misaada isipotolewa anayekomolewa ni Rais Dk. Magufuli?. Au ni Watanzania wanyonge ambao wangekosa dawa, huduma za maji na umeme.

Aliongeza “Lakutia faraja ni kwamba pamoja na jitihada hizo, washirika wa maendeleo wameongeza kasi ya ushirikiano na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Magufuli,”.

Alisema yeyote mwenye uchungu na nchi yake angepambana ili jambo linalohusu maslahi ya taifa, likiwemo la kununua ndege lisikamwe na kama kuna mkwamo, ashiriki kukwamua badala ya kushabikia.

Kauli ya Kaimu Mkurugezi huyo wa Maelezo, imefanana na kauli mbalimbali za wananchi, walioeleza kuwa Lissu amekuwa akipotosha mambo mengi, na umefika wakati wa kuchukuliwa hatua kali za  kisheria.

Jacob Agustino, ambaye ni mkazi Temeke Mtongani, alisema huyu mtu anapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa hasa kutokana na kujifanya anajua sheria na mwisho wa siku anafanya mambo mengi ya ovyo.

Alisema kuna wakati alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Tanzania yote ijue kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ni fisadia namba moja nchini na badala ya siku amekuwa mstari wa mbele katika kumsifia na kumfanya aonekane ni mtu safi.

"Watanzania tuweni makini, serikali inafanya kazi nzuri chini ya Rais Dk. John Magufuli,ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila linalofanywa linafanywa kwa maslahi ya umma,''alisema.

Hivyo, alisema kila mwananchi mpenda maslahi anapaswa kuwa pamoja na Rais Dk. Magufuli kwa kuwa katika kipindi kifupi ameipa hadhi nchi kuwa na ndege zake zenyewe na hatimaye kuwa na mafanikio katika usafiri wa anga.

No comments:

Post a Comment