Ibara ya 117 ya katiba ya CUF ndio
mwiba kwake,
Inaelekeza kiongozi anayetaka
kujiuzulu lazima akubaliwe na mamlaka iliyomchagua
Yeye na Mtatiro walimpuuza Lipumba,
Sasa wanahaha kujinusuru
Mipango kumuangushia lawama msajili
wa vyama ,serikali yazidi kugognga mwamba
Kila mahali waambiwa fuateni katiba
yenu.
Na Ibrahim Malinda.
KUKWAMA kwa majaribio kadhaa ya Katibu Mkuu wa chama
cha wananchi( CUF) Maalim Seif Sharif Hamad dhidi ya Mwenyekiti wake Profesa
Ibrahim Lipumba na viongozi wake waandamizi aliowateua na wengine kuteuliwa na
vyombo vya maamuzi vya chama hicho kunatokana na katiba ya chama hicho, imezidi
kubainika.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama
hicho, Maalim Seif alipata pigo baada ya kukwama kwa jaribio lake la kuwavua uanachama wanachama
kadhaa wa chama hicho akiwemo Magdalena Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF
Bara na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la
Kaliua, Mkoani Tabora sambamba na Maftah Nachuma ambaye ni mbunge wa Mtwara Mjini.
Sambamba na jaribio hilo kukwama,
wiki chache zilizopita Wakala wa Usajili, Ufilisi na Uthamini(RITA) iliridhia
usajili wa wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini baada ya kuisha kwa muda wa bodi
ya awali ya udhamini wa chama hicho.
Jambo hilo linathibitisha kumuondoa
Maalim Seif katika nafasi ya kushinda imani ya wananchama wa CUF baada ya
kuenea kwa tetesi kwamba bodi mpya ya wadhamini imeunda na wanachama
wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Lipumba.
Kitendo cha kutambuliwa kwa bodi
mpya ya wadhamini wa CUF, kinatoa taswira kuwa kuna uwezekano wa kufutwa kwa
mashtaka yote yaliyofunguliwa na bodi ya awali ya udhamini, bodi ambayo kwa
mujibu wa katiba ya chama hicho, ndio imepewa mamlaka ya kushtaki na kushtakiwa
kwa niaba ya chama cha CUF.
Aidha maung’uniko ya muda mrefu ya
katibu mkuu huyo wa chama hicho kuwa kurudi kwenye kiti kwa mwenyekiti wake
Lipumba kunatokana na kubebwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini
inayoongozwa na jaji Fransis Mutungi yameonekana kukosa mashiko.
Hali hiyo, inatokana na Lipumba
baada ya kujua kwamba katiba ya chama hicho inamruhusu kutengua uamuzi wake
kutokana na kutokukubaliwa kwa ombi lake na mamlaka iliyomchagua.
Taarifa zaidi zinasema kwamba
kuzembea kwa katibu mkuu huyo kuchukua uamuzi wa kuitisha mkutano mkuu wa chama
hicho haraka mara tu baada ya kupokea barua ya Lipumba ya kujiuzulu ambapo mkutano huo ungepiga kura ya siri ya
kuridhia ombi hilo na hatimaye Lipumba kuwa ameondoka rasmi kwa kufuata matakwa
ya katiba ndiko kumesababisha mtanziko unaendelea hivi sasa.
‘’Katiba ilimtaka katibu mkuu
kuitisha mkutano mkuu maalum kwa ajili ya kujadili na kupiga kura juu ya barua
ya Profesa lakini Maalim hakuitisha, hiyo hata ule mkutano wa Agosti 21 pale
ubungo plaza haukuwa na lengo la kujadili barua ya Profesa bali ni kuchagua tu
Mwenyekiti ambapo kina Taslima walikuwa wanagombea, lakini tulipokataa kwa
nguvu ndio ikachomekwa hiyo agenda na hata hivyo hatukufikia hatua ya kupiga
kura’’. Anasema mjumbe mmoja wa mkutano mkuu wa chama hicho kutokea viwani
Zanzibar tunayemuhifadhi jina lake kwa sasa.
Kwa kifupi Ibara ya 117(2) ya katiba ya CUF inataka ili
kiongozi ahesabike amejiuzulu ni lazima mamlaka iliyomchagua ikubali ombi lake,
ambapo kwa Profesa Lipumba mamlaka hiyo ni Mkutano mkuu wa chama hicho ambao
haujaridhia ombi hilo . Hata hivyo Maalim Seif na timu yake wanaukwepa ukweli
huo wa katiba yao na kueneza propaganda dhidi ya Msajili na Serikali.
Ibara hiyo ya 117 kifungu kidogo cha (2) inasomeka kama ifuatavyo ‘’Kiongozi
atajiuzulu kwa kuandika barua na kuweka saini yake kwa katibu wa mamlaka
iliyomchagua au kumteua na kiongozi huyo atahesabiwa kuwa amejiuzulu
ikifika tarehe aliyoiainisha katika barua yake kuwa atajiuzulu pindipo
akikubaliwa na mamlaka iliyomchagua au iliyomteua, au kama hakuainisha
tarehe ya kujiuzulu kwake basi atahesabiwa amejiuzulu mara baada ya katibu wa
mamlaka iliyomteua au kumchagua kupokea barua hiyo na mamlaka iliyomchagua
au kumteua kukubali ’’.
Hivi karibuni gazeti hili liliripoti
kuwa hali ya mambo inazidi kwenda kombo kwa upande wa Maalim Seif katika
mgogoro wa kiuongozi unaoendelea baina yake na mwenyekiti wa Taifa wa Lipumba.
Kitendo cha Mwenyekiti wa Chama
hicho, Profesa Lipumba kuwavua uanachama wabunge nane na madiwani wawili wa
viti maalum kitendo kilichoonyesha kufuata taratibu zote za kisheria na katiba
ya ndani ya chama hicho na hatimaye kubarikiwa na ofisi ya Bunge, Tume ya taifa
ya Uchaguzi na msajili wa vyama vya siasa.
Taarifa zaidi inaelezwa kinaelezwa
kumpagawisha Katibu Mkuu huyo na timu yake kiasi cha kuamua na yeye kuwavua
uanachama wanachama wengine kadhaa akiwemo mbunge na Naibu Katibu Mkuu
anayekaimu majukumu ya Katibu Mkuu wa chama hicho kwa sasa kutokana na
kutokufika ofisini kwa Maalim Seif tangu mwezi Septemba, 2016.
Mmoja wa wanaharakati wa siasa
nchini, Joseph Zabron, alisema huu ndio wakati wa Maalim Seif kukaa mezani na
Profesa Lipumba kuyamaliza mambo yote kwa kuwa chama imara ni maelewano na si
kuanza kutoa shutuma kwa vyombo vya dola.
“Hili suala ukilitizama kwa umakini
si Msajili wa Vyama, Bunge wala Tume au Mahakama unaweza ukasema inaingilia CUF
zaidi ya Katiba yao wenyewe na ndio maana wao wenyewe wamekwenda mahakamani
kukatia rufaa maamuzi ya msajili, lakini maamuzi halali hayakatiwi
rufaa,’’alisema.
Kadhalika, wakati hayo yanaendelea
hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama hicho alifanikiwa kusajili upya bodi ya
wadhamini wa chama hicho baada ya ile ya awali kumaliza muda wake wa mujibu wa
sheria jambo ambalo limezidisha pigo kwa timu ya maalim seif kwa sababu bodi ya
wadhamini ya chama chochote cha siasa huwa moja tu inayosajiliwa na RITA na kwa
mujibu wa katiba ya CUF bodi hiyo ndio mamlaka pekee inayoruhusiwa kufanya
usimamizi wa jumla wa chama hicho ikiwemo kushtaki na kushtakiwa jambo
linalohatarisha uwepo na uhalali wa kesi zilizofunguliwa na bodi ya awali dhidi
ya Msajili wa vyama na Lipumba juu ya masuala kadhaa.
Aidha, kukwama huko kwa maalim Seif
katika kile anachokiita mapambano ya kukinusuru chama hicho, kunamfanya sasa abadili
mawazo na kujiandaa kuhamia chama kingine kikubwa cha upinzani hapa nchini
chenye ngome yake kuu Tanzania bara.
Taarifa zaidi zinaonyesha kwamba
mpaka sasa maalim na watu wake wameshakubali kuwa kisheria hawawezi kumshinda
Prof. Lipumba na kwamba wamebakiwa na njia mbili pekee ama wahame kuhamia chama
hicho kikubwa cha upinzani Tanzania bara ama waanzishe chama chao wenyewe
kipya.
Mjadala unaoendelea hivi sasa baina
ya wadau muhimu wa timu ya maalim Seif ni kwamba iwapo uamuzi utakuwa ni kuwa
wanahama, je watahama na vyeo vyao walivyokuwa navyo wakiwa CUF kama hicho cha
Katibu mkuu na vya baadhi ya vya wakurugenzi au watahamia na kuwa wanachama wa
kawaida jambo ambalo wanahisi litawapunguzia nguvu ya kufanikisha agenda yao ya
kuendelea kudai maslahi yao ya kisiasa yanayotokana nauchaguzi mkuu uliopita.
Taarifa hizo pia zinaeleza kuwa
mpaka sasa majadiliano ya kina ya namna gani Maalim na timu yake watahamia
chama hicho yameshaanza na yanaratibiwa vizuri na wanasiasa kadhaa mashughuli
hapa nchini wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wenye vinasaba na chama
hicho.
Ikiwa mwanasiasa huyo atahama chama
hicho na kujiunga chama kingine kama njia ya kufikia lengo lake la kisiasa,
kitakuwa ni kielelezo mahsusi cha kudhibitiwa na Prof. Lipumba katika kuijua na
kuifahamu katiba ya chama hicho na pia ndio utakuwa mwisho wa ushirikiano wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.
Alipotafutwa na gazeti hili msajili
wa vyama vya siasa Jaji Fransis Mutungi, ameendelea kusisitiza kwamba ofisi
yake itaendelea kufanya kazi za kuvisimamia vyama vyote vya siasa vilivyopo
hapa nchini kama sheria iliyoviasisi inavyosema na kuongeza kuwa kinachoendelea
ndani ya Cuf ni matokeo ya utekelezaji wa katiba ya chama hicho ambacho
wameitunga wenyewe.
‘’mimi ofisini kwangu ninasajili
vyama baada ya kuzipitia katiba zao na kujiridhisha kuwa hazikiuki masharti ya
sheria za nchi, nikizipokea na kujiridhisha siongezi wala kupunguza kitu
chochote zaidi ya kuzisajili, na kama ujuavyo katiba ikishapitishwa
kinachofuata ni kutekelezwa tu’’. Alisema Msajili Mutungi
‘’kwa hiyo Lugha nyepesi kabisa
kuitumia ni kwamba mchawi wa Cuf si Mutungi wala nani, Mchawi wa Cuf ni katiba
yao wenyewe, waifate katiba yao inavyoelekeza nina imani hakuna malalamiko
yatakayotokea, lakini kama wataendelea kufanya mambo kwa hisia na utashi
binafsi, basi haya wataendelea kulalamikiana daima’’. Aliongeza mtaalamu huyo
wa maswala ya sheria.
No comments:
Post a Comment