Na. Ibrahim Malinda
Wakati jana Rais wa Jamhuro ya
Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ametimiza miaka miwili tangu
aapishwe kuwa Rais wan chi, sekta ya maji imekuwa ni miongoni mwa sekta
zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa sana na kupigiwa mfano.
Uzinduzi wa miradi mikubwa ya maji
kama ule wa ruvu chini, mradi wa kutoa maji ziwa Victoria na kuyapeleka mikoa
ya jirani, mradi wa maji kigoma, mradi wa misungwi , mradi mkubwa wa maji wa
lindi na mingineyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya serikali hii ya awamu
ya tano.
Jiji la Dar es salaam kwa sasa
sehemu kubwa yake imekuwa ikipata huduma ya maji ya bomba hata kwenye maeneo
yaliyosemwa kuwa korofi na malalamiko ya upatikanaji wa maji kuwa makubwa
lakini sasa imekuwa tofauti.
‘’kwa kweli sasa hivi hawa DAWASCO
waje watengeneze mabomba tu ili maji yasiendelee kumwagika maana maji yamekuwa
mengi mno’’. Anasema mkazi wa tabata Mariam Abdalaah
‘’huku tabata hapo nyuma ilikuwa
ukitaka kuhamia unaambiwa kuhusu shida ya maji, na mara chache yalikuwa
yanatoka kwa kuvizia pengine hata mara moja kwa mwezi, lakini kwa sasa
tunajionea wenyewe yanavyotiririka. Tunawapongeza sana kwa hatua hii muhimu,
maji ni uhai bwana’’. Aliongeza
Aidha, utaratibu wa serikali kuwagia
maji wananchi kwa kulipa kidogo kidogo (yaani mkopo) kumeonyesha uwepo wa
mapinduzi makubwa na utayari wa kipekee wa serikali kuhakikisha huduma hii
muhimu inawafikia wananchi wote bila kujali vipato vyao.
Mwanabaraka Habibu ni miongoni mwa
wanufaika wa utaratibu huu na anasema umemfanya ajisikie mwenye furaha sana kwa
kuwa na uhakika wa maji safi na salama
‘’hata sijui niseme nini, yaani
nimefungiwa bomba hilo hapo na nalipa taratibu taratibu mpaka deni liishe,
mambo ya kudamka alfajir kuwahi foleni tumesha sahau kwa sasa. Mungu atupe nini
tena?’’ alinukuliwa
Hivi karibuni katibu mkuu wa wizara
ya maji na numwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo ameandika makala maalum
inayofafanua na kuelekeza masuala mbalimbali kuhusiana na mafanikio, mipango na
matarajio ya wizara hiyo katika kuhakikisha watanzania wanapata maji safi na
salama.
Miaka Miwili ya JPM:
Kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika katika sekta ya maji
Kitila Mkumbo
Wataalam
maendeleo duniani wanakubaliana kwamba maji ndicho kiungo na kichocheo kikubwa
cha maendeleo katika dunia ya leo. Bila maji hakuna maendeleo. Bila maji hakuna
maisha. Ndiyo maana hata wataalam wa anga wanatumia uwepo wa maji kama mojawapo
ya vielelezo vya uwezekano wa kuwepo maisha katika sayari zingine. Maji ni
bidhaa ya pekee duniani yenye uhitaji kwa wote kwa wakati wote. Upekee wa maji unatokana na
ukweli kwamba bidhaa hii haina mbadala. Ukikosa kuni za kupikia utatumia majiko
ya umeme, mkaa, gesi, mafuta ya taa, au umemejua. Ukikosa umeme utatumia mwanga
wa jua; utawasha koroboi na unaweza kuamua kulala gizani.
Upo uhusiano mkubwa baina ya ukosekanaji wa maji na kiwango cha
maendeleo. Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa moja ya kiashiria cha nchi zilizo
nyuma kimaendeleo ni tatizo la upatikanaji wa maji kwa watu wake. Ni kwa sababu
hii Rais John Pombe Magufuli alitamka wazi wakati akifungua rasmi Bunge jipya
la Jamhuri wa Muunghano wa Tanzania kuwa “Tunataka
tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini
kama wananchi hawapati maji safi na salama”.
Lakini
kama hakuna maji utaoga nini? Utapikia nini ili chakula kiive? Utafulia nini
nguo chafu? Utakunywa nini ili uweze kukata kiu ya maji mwilini? Kama hakuna
maji, pasina shaka kabisa, ndoto ya nchi ya viwanda itayeyuka! Ujenzi
utasimama! Hoteli na nyumba za kulala wageni zitafungwa! Wafanyakazi hawataweza
kwenda kazini, wanafunzi hawatakwenda shuleni! Hakuna mbadala wa maji!
Ni
kwa sababu ya upekee wa maji, nchi zote duniani huiweka sekta ya maji kama
kipaumbele mojawapo kikubwa katika mipango ya maendeleo. Hivyo ndiyo ilivyo pia
kwa Tanzania ambapo sekta ya maji ni moja ya vipaumbele kumi (10) vya kitaifa
katika mpango wa miaka mitano wa maendeleo.
Mwezi
huu wa Novemba 2017, Rais Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametimiza miaka
miwili (2) tangu alipoapa na kukubali kuongoza Tanzania. Katika makala hii
ninaainisha mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika miaka miwili ya
uongozi wa Rais Magufuli katika sekta ya maji.
Maendeleo
katika sekta ya maji hupimwa kwa vigezo vikubwa vitatu. Mosi, tunaangalia
uwepo, utunzaji, uendelezaji na ukuzaji wa rasilimali ya maji. Pili,
tunaangalia uwezo na kasi ya usambazaji wa raslimali ya maji kwa matumizi
mbalimbali, kama vile matumzi ya nyumbani, viwandani, mashambani na kwa ajili
ya kutunza mazingira. Tatu, tunaangalia uwezo na kasi ya uondoaji wa majitaka,
kwa kuzingatia kuwa takribani asilimia 80 ya maji yanayotumika majumbani
hugeuka kuwa majitaka yanayostahili kuondolewa na kuhifadhiwa katika namna
ambayo haileti madhara ya kiafya kwa binadamu na mazingira.
Prof. Kitila Mkumbo, Katibu mkuu wizara ya maji na umwagiliaji.
Kwa
lengo la makala hii, nitajikita katika mafanikio yaliyopatikana na changamoto
zilizojitokeza katika usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu,
yaani usambazaji wa maji safi na salama ya kunywa. Hata hivyo, itoshe tu kusema
kwa sasa kuwa, tofauti na imani kuwa tuna maji mengi chini na juu ya ardhi,
ukweli ni kuwa katika miaka 50 iliyopita, raslimali hii imekuwa ikipungua
ukilinganisha na kasi ya ongezeko la idadi ya watu.
Kwa
mfano, wakati mwaka 1962 Tanzania ilikuwa na wastani wa kiasi cha maji mita za
ujazo 7,862 (sawa na mapipa 39,310 ) kwa mtu mmoja kwa mwaka, kiwango hiki
kimeshuka hadi mita za ujazo 1,621 (sawa na mapipa 8105) ilipofika mwaka 2014. Kiwango hiki ni kidogo
na kinaiweka Tanzania kuwa moja ya nchi inayokabiliwa na uhaba wa maji duniani.
Upungufu huu umetokana na sababu mbalimbali, nyingi zikiwa ni matokeo ya
shughuli zetu wenyewe kama vile kuharibu vyanzo vya maji, kukata misitu na
teknolojia ndogo ya kuhifadhi maji. Sababu zingine ni zile ambazo kwa kiasi
kikubwa kipo nje ya uwezo wetu kama vile mabadiliko ya tabianchi. Hii
inamaanisha kuwa tuna kazi kubwa kama taifa ya kufanya katika kuhuisha, kulinda
na kuendeleza vyanzo mbalimbali za maji. Ni kwa sababu hii, serikali, kwa
kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, inatekeleza mipango mbalimbali ya
kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji.
Njia moja ya
kuboresha upatikanaji wa maji hata machache yaliyopo ni kuimarisha mfumo wa
usambazaji ili maji yaliyopo yaweze kukidhi haja ya matumizi yetu. Mfumo wa
usambazaji wa maji katika nchi yetu umegawanywa katika makundi makubwa manne,
ambayo ni Dar es Salaam, miji mikuu ya mikoa, miji midogo na makao makuu ya
wilaya na vijijini. Katika sehemu zinazofuata za makala hii ninaainisha hatua
mbalimbali ambazo serikali imechukua na mafanikio yaliyopatikana katika
kusambaza maji kwa maeneo haya.
Usambazaji wa maji Dar es Salaam
Hatua nne muhimu zimechukuliwa na
zinaendelea kuchukuliwa katika kupanua miundo mbinu ya usambazaji wa maji
katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Kibaha na Bagamoyo. Hatua ya
kwanza ilikuwa ni ukarabati na upanuzi wa mitambo ya kuzalisha maji katika Mto
Ruvu. Mto huu ndio chanzo kikuu cha maji kwa Jiji la Dar es Salaam na miji ya
Kibaha na Bagamoyo ukichangia kwa asilimia 98. Katika miaka ya mwanzo ya 1990
kuelekea miaka ya 2000 uwezo wa mitambo hii kuzalisha maji ulipungua sana ukilinganisha
na mahitaji. Mitambo hii ilikuwa inazalisha lita milioni 300 (mapipa milioni
1.5) kwa siku wakati mahitaji halisi yalikuwa ni lita milioni zaidi ya 500
(mapipa milioni 2.5).
Kwa kutambua hili, serikali, kwa
kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, iliwekeza shilingi bilioni 443 kwa
ajili ya kupanua mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. Kazi imekamilika mapema
mwaka huu na mitambo ya Ruvu Juu ilizinduliwa rasmi na Mhe Rais Dkt John
Magufuli mwezi Juni 2017. Kufuatia hatua hii, uzalishaji wa maji wa mitambo hii
sasa umeongezeka hadi kufukia lita milioni 502 kwa siku wakati mahitaji halisi ni
lita milioni 544.
Hatua ya pili ni uchimbaji wa visima
20 katika maeneo ya Kimbiji na Mpera kwa gharama ya shilingi bilioni 18. Visima
hivi kwa pamoja vitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 260 kwa siku, na
hivyo kufikisha jumla ya lita milioni 760 kwa siku kwa Jiji la Dar es Salaam.
Uzalishaji huu utatosheleza mahitaji ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya
Kibaha na Bagamoyo angalau hadi mwaka 2030. Uchimbaji wa visima 19 ulikamilika Oktoba
2017. Serikali tayari imeanza mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuweka
miundombinu ya usambazaji. Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni pamoja na
Kigamboni, Keko, Chamazi, Mbagala, Kongowe, Ukonga, Gongolamboto, Pugu,
Chanika, n.k. Zinahitajika jumla ya shilingi bilioni 465 kwa ajili ya kuwekeza
katika miundombinu ya usambazaji katika maeneo haya.
Hatua ya tatu ni kuwekeza katika
miundombinu ya kusambaza maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini. Miundombinu hii ni
pamoja na usimikaji wa mabomba na ujenzi wa matanki makubwa ya kuhifadhi maji
katika maeneo ya Kimara, Mbezi na Makongo. Miundombinu hii itagharimu jumla ya
shilingi biloni 290 na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kukamilika kwa mradi huu kutamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji katika
maeneo ya Mbezi Beach, Kinyerezi, Kimara, Kiluvya, Tegeta, Bagamoyo,
Changanyikeni, Wazo, Bunju, Salasala, Goba, n.k. Baadhi ya wakazi wa maeneo
haya tayari wameanza kupata maji ya uhakika kwa zaidi ya masaa 20 kwa siku na
hali hii itaendelea kuboreka na kuimarika kabisa ifikapo mwishoni mwa mwaka
huu.
Hatua ya nne ni ujenzi wa Bwawa la
Kidunda lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Katika miaka ya hivi
karibuni Mto Ruvu umeanza kupungua maji hasa nyakati za kiangazi. Hali hii
inatishia uhakika wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine
yanayohudumiwa na mitambo ya Ruvu Juu na Chini. Hali inatarajiwa kuwa mbaya
zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kasi kubwa ya ongezeko la watu
katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa kutambua hili, serikali imewekeza katika
mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kwa lengo la kuwa na chanzo cha uhakika wa
maji kutiririka katika Mto Ruvu na kuondoa kabisa tatizo la kupungua kwa uwezo
wa uzalishaji kwa kutumia Mto Ruvu. Gharama za mradi huu ni takribani shilingi
bilioni 483. Hadi sasa, kati ya hatua tano za ujenzi wa mabwawa, tumekamilisha
hatua tatu ambazo ni upembuzi wa awali, upembuzi yakinifu na usanifu. Aidha,
tumelipa jumla ya shilingi bilioni 7 kwa wananchi waliopisha ujenzi wa mradi
huu. Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya wadau wa
maendeleo ili kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa bwawa hili.
Kutokana na hatua mbalimbali
zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kupanua na kuimarisha miundombinu
ya usambazaji katika Jiji la Dar es Salaama, hali ya upatikanaji wa maji
imeboreka kutoka asilimia 55 mwaka 2015 hadi aslimia 75 mwezi Septemba 2017. Tunatarajia
kuwa hali ya upatikanaji wa maji itaboreka zaidi na kufikia asilimia 86 ifikapo
Juni 2018.
Usambazaji wa maji katika miji
mikuu, miji midogo na halmashauri za wilaya
Serikali inatekeleza miradi
mbalimbali katika ngazi ya miji mikuu ya mikoa na miji midogo 25. Miradi hii
yote ina gharama ya zaidi ya shilingi trilioni 2.73 na ilipiwa na serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Baadhi ya miradi inayotekelezwa
ni pamoja na mradi wa kuchukua maji kutoka Ziwa Viktoria na kupeleka katika
miji ya Busega, Bariadi, Legangambili, Maswa, na Mwanhuzi, Isaka, Kagongwa,
Mwadui, Kishapu, Kolandoto na Maganzo. Miradi yote kwa pamoja inagharimu jumla
ya shilingi bilioni 763.
Mwezi Aprili mwaka huu, serikali
ilisaini mikataba mitatu na wakandarasi watakaojenga mradi mkubwa wa maji unaotoa
maji kutoka Ziwa Viktoria na kupeleka katika miji ya Tabora, Nzega, Uyui,
Igunga, Tinde, na Sikonge. Mradi huu utagharimu jumla ya shilingi bilioni 600. Upo
mradi mwingine unaotumia pia chanzo hiki cha Ziwa Victoria kwenda Miji ya
Kagogwa na Isaka. Mradi huu unagharimu jumla ya Shilingi bilioni 24.72.
Miradi mingine imekamilika na/au
inaendelea kutekelezwa katika miji mbalimbali ikiwemo: Mwanza, Bukoba, Musoma,
Sengerema, Geita, Nansio, Kigoma, Sumbawanga, Lindi, Mtwara, Babati, Arusha,
Morogoro, Mwanga, Same, Korogwe, Tanga, Mugumu, Longido, Simanjiro, Dodoma na
Singida.
Aidha, serikali ipo mbioni kuanza
kutekeleza mradi wa maji wa dola milioni 500 (zaidi ya shilingi trilioni 1)
ikiwa ni mkopo nafuu kutoka serikali ya India kupitia Benki ya Exim-India.
Mradi huu utatekelezwa katika miji 17, ikiwemo mji mmoja wa Zanzibar. Miji
itakayofaidika na mradi kwa upande wa Tanzania Bara ni Muheza, Wanging’ombe, Makambako,
Kayanga, Songea, Geita, Kilwamasoko, Tanga (HTM), Njombe, Mugumu, Chunya,
Sikonge, Makonde, Manyoni, Kasulu and Rujewa.
Kwa hiyo, kwa ujumla wake, serikali
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imewekeza zaidi ya shilingi
trilioni 3.73 katika miradi ya maji inayotekelezwa katika miji mikuu ya mikoa,
miji mikuu ya wilaya na miji midogo. Kutokana na miradi inayoendelea
kutekelezwa, tunatarajia hali ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya mijini
iboreke kutoka chini ya asilimia 60 mwaka 2015 hadi asilimia 75 ifikapo Juni
2018 na kufikia wastani wa asilimia 95 ifikapo 2020.
Kwa upande wa Vijijini, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau wengine wa Maendeleo inaendelea kutekeleza miradi
mbalimbali kama sehemu ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP). Jumla ya miradi 1,810
ilipangwa kutekelezwa maeneo ya vijijini tangu mwaka 2013, na kati ya hii,
miradi 1,444 imekamilika, na miradi 366 ipo katika hatua mbalimbali za
utekelezaji.
Katika kipindi cha miaka miwili ya
utekelezaji wa awamu ya tano ya Serikali, jumla ya miradi 388 imeendelea kutekelezwa vijijini na kiasi cha shilingi 274,887,164,606.86 zimetumika kwa ajili
ya miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa.
Kwa ujumla, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau wa Maendeleo, kupitia miradi mbalimbali iliyokamilika na inayoendelea,
tayari imejenga vituo vya kuchotea maji vijijini 121,369, ukilinganisha na lengo la kujenga vituo 155,934 ifikapo mwaka 2020. Kama vituo
hivi vyote vingefanya kazi vyote vingekuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi milioni
30.3 sawa na asilimia 79. Hata
hivyo, ni vituo 83,331 pekee
vinavyofanya kazi vikiwa na uwezo wa kuhudumia watu milioni 20.8, sawa na asilimia
55. Hivyo, moja ya changamoto ya miradi ya maji vijijini ni kuhakikisha
kuwa miradi inafanya kazi muda wote, na hili ni jukumu la Watumiaji pamoja na Uongozi
katika ngazi ya Vijiji na Halmashauri. Serikali inachukua hatua mbalimbali
kuimarisha usimamizi wa miradi iliyokamilika Vijijini. Lengo ni kuhakikisha
kuwa ifikapo mwaka 2020, angalau asilimia 85 ya wananchi vijijini wawe wanapata
huduma ya maji.
Hitimisho
Katika miaka miwili ya uongozi wa
Rais John Pombe Magufuli, serikali imeendelea kutekeleza na kuibua miradi mipya
mbalimbali ya maji. Jumla ya miradi mikubwa mitano inatekelezwa Jijini Dar es
Salaam, miradi zaidi ya 50 katika miji mbalimbali na miradi zaidi ya 1,800
vijijini.
Kukamilika kwa miradi inayoendelea kutekelezwa
kutaongeza kasi ya usambazaji maji kwa wananchi. Lengo la serikali ni
kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, angalau asilimia 85 ya wakaazi wa vijijini
na asilimia 95 ya wakaazi wa mijini wawe wanapata maji safi, salama na ya
uhakika. Kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo, sisi
watendaji katika serikali ya Rais Magufuli tunafanya kazi kwa bidii kubwa
kuhakikisha kuwa lengo hili linatimia. Kasi ya utekelezaji wa miradi katika
miaka miwili ya Rais Magufuli inaonesha pasi na shaka kuwa tutafikia malengo
haya.
Mwandishi wa Makala haya ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment