WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Tuesday, November 7, 2017

Siri kifo balozi wa Libya zaanza kuvuja

Siri kifo balozi wa Libya zaanza kuvuja

Na. Mwandishi Wetu,
Ikiwa ni siku moja tu imepita tangu gazeti hili kuandika juu ya kuibuka upya kwa utata unaohitaji kutolewa ufafanuzi na vyombo vya dola na kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha aliyekuwa balozi wa Libya nchini Tanzania Ismail Nwairat aliyefariki kwa kujipiga risasi, siri zaidi juu ya kifo hicho zimeanza kuvuja na kulifikia gazeti hili.

Mmoja wa wasaidizi wa ofisi ya balozi hiyo ambaye ameomba jina lake lisiandikwe kwa sasa amesema analifahamu vyema tukio hilo kuanzia mwanzo mpaka mwisho na anajua kila kilichotokea mpaka kupelekea kifo cha bosi wake na kwamba atashukuru sana kama uchunguzi utaitishwa nayeye atajitolea kutoa ushahidi wote wa jambo zima.

‘’kwanza niwapongeze hawa walioliibua hili jambo, ukweli ni kwamba hata sisi pale ofisini linatuumiza kichwa sana, japo miaka mitatu imepita lakini hakuna anayeijua kesho yake, hivyo ninaungana na hawa wanaoiomba serikali kufanya uchunguzi ili jambo hili likamilike na ukweli ujulikane’’. Anasema mtumishi huyo

‘’hata sisi mwanzo naada ya tukio tulidhani ni vyama kama uchunguzi wa kina ungefanyika na kila mwenye taarifa ama fununu angeitwa kutoa maelezo ya kina, lakini badala yake nguvu kubwa ilipelekwa kwenye kusafirisha mwili na kuuzika na huku nyuma kupuuza umuhimu wa kuweka sawa kumbukumbu’’. Aliongeza

Taarifa za ziada zilizopo mezani mwa gazeti hili zinaonyesha kuwa ikiwa vyombo vya ulinzi na usalama vutaamua kufanya uchunguzi wa kina juu ya jambo hilo basi watu kadhaa wapo tayari kutoa ushirikiano wa kueleza siri iliyojificha juu ya tukio hilo la kihistoria la kwanza na la aina yake kuwahi kufanywa hapa nchini la balozi kujitoa uhai wake

‘’unajua mpaka sasa kila mtu anasema lake huko nje, wapo wanaoamini kuwa marehemu alijipiga risasi, na wapo wasioamini kwenye hilo na wote wana hoja zao na mitazamo yao, kuliko mimi kukuambia upande upi ni mkweli kati ya wanao amini na wasio amini, wacha tusubiri uchunguzi wa kina ufanyika na tutatoa ushahidi wa kile tunachokifahamu Insha Allah’’. Aliongeza tena

Jana gazeti hili liliandika kuwa mwanaharakati  Philipo Mwakibinga ambaye ni Mratibu wa taasisi ya watetezi wa rasilimali wasio na mipaka maarufu WARAMI ambae pia amepata kuwa Rais katika serikali ya wanafunzi chuo kikuu cha Dodoma UDOM ameibuka na kuibua maswala mazito yanayohusiana na diplomasia ya kimataifa na uchunguzi wa kipolisi kuhusiana na kifo cha aliyekuwa balozi wa Libya nchini Tanzania Ismail Nwairat ambaye taarifa zilitolewa zikisema kuwa amejiua kwa kujipiga risasi akiwa ofisini kwake jijini Dar es salaam tarehe 2 juni 2014.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mwakibinga ameitaka serikali kupitia jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na kuondoa utata unaoonekana kuvikabili vichwa vya wananchi wengi wa Libya waliopo hapa nchini ambao yeye anafahamiana nao

‘’mimi nina marafiki zangu kadhaa wa ki Libya, tangu kutokea kwa tukio lile mpaka leo kila siku wanasononeka kuhusiana na kifo cha balozi wao, na mimi wananitumia kama sample ya mwananchi ambae taifa langu limeshindwa kulinda uhai wa mwana diplomasia wao’’. Anasema Mwakibinga

‘’wanasema haiwaingii akilini na hata mimi hainiingii akilini mtu mzima mwenye hadhi ya kuwa balozi ajipige risasi akiwa ofisini kwake mchana kweupe…kwa maslahi mapana ya taifa langu na heshima yake kimataifa naviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina juu ya swala hili’’. Aliongeza mwanaharakati huyo

Marehemu balozi Ismail Nwairat ambaye alikuwa anakaimu nafasi hiyo aliripotiwa kupoteza uhai wake kwa kujipiga risasi ofisini kwake.
Balozi huyo ambaye alikuwa anasifika kwa kutoficha msimamo wake wa kupingana na serikali iliyoondolewa madarakani ya hayati Kanal Muamar Gadafi kwa mapinduzi ya umma kwa kuiita ya kidikteta isiyojali wala kuheshimu haki za binaadam, kifo chake kilizua sintofahamu miongoni mwa wadau wengi wa masuala ya kidiplomasia ya kimataifa.

Taarifa ya kifo cha balozi huyo kufariki zilisema kuwa balozi huyo alijipiga risasi ya kifuani upande wa kushoto akiwa ofisini kwake.
Taarifa iliyotolewa na  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilisema kuwa,  ilipokea taarifa kutoka kwenye Ubalozi huo kuwa aliyekuwa Kaimu Balozi wa Libya,  Ismail Nwairat amefariki dunia  kwa kujipiga risasi.

Hata hivyo ubalozi wa Libya ulisema  kuwa,  kifo hicho kilitokea majira ya saa 7 mchana ofisini kwa Kaimu Balozi huyo katika jengo la Ubalozi wa Libya. Na ilitaarifiwa kuwa  Nwairat alijifungia ofisini na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto.

“Maafisa ubalozi walivunja mlango waliposikia mlipuko wa bunduki na kumkuta Kaimu Balozi Nwairat ameanguka chini, walimkimbiza hospitali ya AMI Oysterbay ambako alitangazwa kuwa alikwisha kufariki na Polisi walithibitisha kifo hicho” ilisema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment