·
Katika kila watu 10 , 7 kati yao wanalalamika njaa
·
Kampuni zafunga Ofisi, zapunguza wafanyakazi
·
Vijana sasa wageukia Kilimo, Ufugaji
·
Serikali yasisitiza hali ni shwari
Na. mwandishi wetu,
Mabadiliko makubwa ya kimfumo wa utawala katika serikali ya
awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli yanayoendana na
kubana matumizi, kurudisha nidhamu serikalini, kufuta na kuondoa wafanyakazi
hewa na kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda yenye uchumi wa kati
yanaonyesha kuambatana na maumivu makali kwa wananchi wa kada mbalimbali
yanayotokana na kinachoitwa kukaukiwa fedha mifukoni kunakotokana na kubanwa
matumizi huko.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti unaonyesha kwamba, tangu
mkakati wa kubana matumizi ushike kasi, hali ya maisha ya watu mmoja mmoja
imekuwa ikibadilika kwa kasi kubwa huku nidhamu ya fedha ikionekana kutamalaki
tofauti na hapo awali.
Sambamba na malalamiko hayo, taarifa zinaonyesha kupungua
ama kudorora kwa mzunguko wa fedha katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani jijini
Dar es salaam kunakotokana na watu wengi wenye kipato kikubwa kijihami na
kuamua kubana matumizi huku wakisikilizia hali ya uchumi kutengemaa, sambamba
na kubana huko matumizi kwa kutokutumia pesa na kuiondoa katika mzunguko, pia
wafanyabiashara wengi waliokuwa wametoa ajira kwa vijana na watu wazima
wamepunguza idadi ya wafanyakazi kati ya asilimia 40 mpaka 60 ya wafanyakazi
waliokuwa wamewaajiri ili kuendana na mabadiliko hayo ya kiuchumi.
Mmoja wa wamiliki wa kampuni inayojihusisha na huduma za
hoteli hapa nchini ambaye ameombwa jina lake lisitajwe Gazetini, amesema
kampuni yake haina namna zaidi ya
kupunguza wafanyakazi na kuitaka serikali iangalie upya na haraka njia bora ya
kubadili mfumo wa kiuchumi bila kuathiri shughuli na maisha ya kila siku ya
wananchi wake.
‘’kwa sasa ninaedesha kampuni kwa hasara kubwa, tena hasara
imekuwa ikiongezeka kila siku tangu mwezi wa tatu, kiasi kwamba hata
wafanyakazi ninawalipa Mishahara kutoka kwenye vyanzo vingine vya mapato
ambavyo navyo vimekata kwa sasa, hivyo hakuna jinsi ndio maana nimeamua
kuwapunguza tu ndugu yangu’’. Alisema
‘’wewe mwenyewe fikiria, tunalipa Ankara za maji, umeme,
usafi na mishahara kwa gharama kubwa sana tofauti na tunachokipata, hali hii
inatuumiza sana’’. Aliongeza
Utafiti zaidi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa
katika kila watu 10 waliohojiwa juu ya hali ya sasa ya kimaisha na kiuchumi,
watu saba kati yao wamekuwa wakilalamika mabadiliko haya kuwakuta kabla ya wao
kujiandaa na kwamba wanalia njaa.
‘’kwa hali hii, bora nichukue zangu malipo yangu ya pensheni
nikajiajiri kwa kilimo aisee, nikifuga zangu kuku wa nyama na mayai hata wa
milioni tatu naamini ipo siku watanilip tu’’. Alisema Godwin Mnyembela wa
kinyerezi Dar es salaam.
Mwengine aliyepata kuzungumza na gazeti hili bwana Gilbert
Mgube amesema kuwa kwa hali hii inavyokwenda inawahitaji vijana kutuliza akili
zaidi kuliko kupapatika na sehemu sahihi ya kutulizia akili wakati wa kuangalia
namna bora zaidi ya kuendana na kasi hii ni kilimo.
‘’wapo wanaolalamika kuhusu kilimo kutokulipa, lakini sio
sawa na kutokupata kabisa, uzurinwa kilimo hakikukati moja kwa moja, utakosa
kikubwa lakini kidogo utapata, na ikiwa utazingatia matakwa ya ukulima wa
kisasa haiwezi kukukata kabisa na lazima ikulipe, japo changamoto ya soko imezidi
kuwa kubwa kwa sasa, lakini hakuna kukata tamaa’’. Alisema Mgube
Hivi karibuni kumeripotiwa kufanyiwa mabadiliko kwa
makampuni kadhaa ya hoteli na kufungwa, kuuzwa ama kubadili matumizi ili
kuendana na hali ya sasa ya ubanaji wa matumizi.
Hoteli maarufu jijini arusha za Snow Crest na Mount Meru
zilizokuwa zikisifika kwa ubora na uendeshaji wake sasa zimetangazwa kuuzwa
huku jijini Dar es Salaam hotel maarufu ya land mark iliyopo ubungo riverside
ikibadili matumizi kutoka kuwa hotel mpaka hostel kwa ajili ya wanafunzi wa
vyuo vikuu.
Hali hii inakuja huku kukiwa na taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti
yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho
ya mwaka 2015 (Oktoba - Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato
la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016)
kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii
inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6
umepungua kwa 4%.
Taarifa hizo zinaonyesha kuwa Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi
masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015
mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya
kipindi kisichozidi miezi sita, sambamba na hayo, Ukuaji wa sekta ya ujenzi
katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii
katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya
takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
Taarifa hizo
zinaonyesha zaidi kuwa Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka
kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya
kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporomoka kwa 7%.
Taarifa hizi za
kushuka kwa uchumi zinaenda sambamba na malalamiko ya kupungua kwa shehena ya
mizigo katika bandari ya Dar es salaam kunakodaiwa kutokana na kuongezeka kwa
gharama za tozo za kodi tofauti na hapo awali.
Tofauti na malalamiko hayo ya kupungua kwa mizigo
kunakodaiwa na serikali kupitia mamlaka ya mapato nchini Tra kupandisha tozo hizo, taarifa
iliyosambazwa na viongozi wa Tra mitandaoni inawaondoa hofu watanzania na
kwamba kodi sio sababu ya mizigo kupungua.
Taarifa hiyo inakiri kuwa ni ukweli uliowazi kuwa kwa kiasi
fulani mizigo imepungua kwa wastani wa asilimia 9-30 kutegemea na nchi,
ambapo mizigo mingi iliyokuwa inapita
bandari ya Dar kwa kisingizio inaenda Kongo siyo kweli ilikuwa inaenda Kongo
badala yake ilikuwa wana itumia humu
nchini.
Taarifa hiyo inazitaja sababu nyingine kuwa ni Kudorora kwa
bei ya shaba Zambia,Uchaguzi mkuu wa
Zambia na kuimarika kwa Msumbuji
kiasi kwamba bandari ya Beira imeanza kufanyakazi vizuri.
Sababu nyingine ni Kuanza kutumika kwa utaratibu wa Single
Custom Territory ambapo mizigo inalipiwa ktk bandari ya Dar kabla ya
kusafirishwa kwenda Kongo ambapo inawanyima wafanyabiashara kule Kongo kukwepa
kodi .
Sambamba na hayo sehemu ya taarifa hiyo inaonyesha kwamba
hata katika utafiti tulioufanya hata
Bandari ya Mombasa mizigo imepungua, na kusema kuwa kupungua kwa mizigo katika
bandari ya Dar hakujazuia kuongezeka kwa mapato na badala yake mapato
yanayotokana na bandari yameongezeka maradufu tofauti na hapo awali
‘’Wakati meli zikiwa zimepingua katika bandari ya Dar,
Mapato yatokanayo na Forodha mwaka 2015 yalikuwa wastani wa Shilingi
Bilioni 200-300 kwa mwezi. Lakini tangu
Disemba 2015 - August 2016 wastani wa mapato ya Forodha kwa mwezi ni Kati ya
shilingi bilioni 400-550. Facts hizi zipo Mwananchi yeyote anaweza kuzipata kwenye
tovuti yetu ya TRA Taarifa za Mapato kila mwezi.’’ Inasema taarifa ya mamlaka
hiyo ya serikali
Wakati TRA wakisema hayo, hivi karibuni Gavana wa benki kuu
ya Tanzania Professa Beno Ndulu ameuhakikishia umma kwamba hali ya uchumi wan
chi ni shwari na kwamba kila kitu kipo sawa na kinachotokea sasa kiuchumi ni
kuondoka ama kupungua kwa fedha za ujanaujanja mitaani na kubaki kwa fedha
zinazotokana na shughuli rasmi.