WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Thursday, September 29, 2016

NI MTIKISIKO



 ·     


           Katika kila watu 10 , 7 kati yao wanalalamika njaa
·        Kampuni zafunga Ofisi, zapunguza wafanyakazi
·        Vijana sasa wageukia Kilimo, Ufugaji
·        Serikali yasisitiza hali ni  shwari

Na. mwandishi wetu,
Mabadiliko makubwa ya kimfumo wa utawala katika serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli yanayoendana na kubana matumizi, kurudisha nidhamu serikalini, kufuta na kuondoa wafanyakazi hewa na kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda yenye uchumi wa kati yanaonyesha kuambatana na maumivu makali kwa wananchi wa kada mbalimbali yanayotokana na kinachoitwa kukaukiwa fedha mifukoni kunakotokana na kubanwa matumizi huko.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti unaonyesha kwamba, tangu mkakati wa kubana matumizi ushike kasi, hali ya maisha ya watu mmoja mmoja imekuwa ikibadilika kwa kasi kubwa huku nidhamu ya fedha ikionekana kutamalaki tofauti na hapo awali.
Sambamba na malalamiko hayo, taarifa zinaonyesha kupungua ama kudorora kwa mzunguko wa fedha katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani jijini Dar es salaam kunakotokana na watu wengi wenye kipato kikubwa kijihami na kuamua kubana matumizi huku wakisikilizia hali ya uchumi kutengemaa, sambamba na kubana huko matumizi kwa kutokutumia pesa na kuiondoa katika mzunguko, pia wafanyabiashara wengi waliokuwa wametoa ajira kwa vijana na watu wazima wamepunguza idadi ya wafanyakazi kati ya asilimia 40 mpaka 60 ya wafanyakazi waliokuwa wamewaajiri ili kuendana na mabadiliko hayo ya kiuchumi.
Mmoja wa wamiliki wa kampuni inayojihusisha na huduma za hoteli hapa nchini ambaye ameombwa jina lake lisitajwe Gazetini, amesema kampuni  yake haina namna zaidi ya kupunguza wafanyakazi na kuitaka serikali iangalie upya na haraka njia bora ya kubadili mfumo wa kiuchumi bila kuathiri shughuli na maisha ya kila siku ya wananchi wake.
‘’kwa sasa ninaedesha kampuni kwa hasara kubwa, tena hasara imekuwa ikiongezeka kila siku tangu mwezi wa tatu, kiasi kwamba hata wafanyakazi ninawalipa Mishahara kutoka kwenye vyanzo vingine vya mapato ambavyo navyo vimekata kwa sasa, hivyo hakuna jinsi ndio maana nimeamua kuwapunguza tu ndugu yangu’’. Alisema
‘’wewe mwenyewe fikiria, tunalipa Ankara za maji, umeme, usafi na mishahara kwa gharama kubwa sana tofauti na tunachokipata, hali hii inatuumiza sana’’. Aliongeza
Utafiti zaidi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa katika kila watu 10 waliohojiwa juu ya hali ya sasa ya kimaisha na kiuchumi, watu saba kati yao wamekuwa wakilalamika mabadiliko haya kuwakuta kabla ya wao kujiandaa na kwamba wanalia njaa.
‘’kwa hali hii, bora nichukue zangu malipo yangu ya pensheni nikajiajiri kwa kilimo aisee, nikifuga zangu kuku wa nyama na mayai hata wa milioni tatu naamini ipo siku watanilip tu’’. Alisema Godwin Mnyembela wa kinyerezi Dar es salaam.
Mwengine aliyepata kuzungumza na gazeti hili bwana Gilbert Mgube amesema kuwa kwa hali hii inavyokwenda inawahitaji vijana kutuliza akili zaidi kuliko kupapatika na sehemu sahihi ya kutulizia akili wakati wa kuangalia namna bora zaidi ya kuendana na kasi hii ni kilimo.
‘’wapo wanaolalamika kuhusu kilimo kutokulipa, lakini sio sawa na kutokupata kabisa, uzurinwa kilimo hakikukati moja kwa moja, utakosa kikubwa lakini kidogo utapata, na ikiwa utazingatia matakwa ya ukulima wa kisasa haiwezi kukukata kabisa na lazima ikulipe, japo changamoto ya soko imezidi kuwa kubwa kwa sasa, lakini hakuna kukata tamaa’’. Alisema Mgube
Hivi karibuni kumeripotiwa kufanyiwa mabadiliko kwa makampuni kadhaa ya hoteli na kufungwa, kuuzwa ama kubadili matumizi ili kuendana na hali ya sasa ya ubanaji wa matumizi.
Hoteli maarufu jijini arusha za Snow Crest na Mount Meru zilizokuwa zikisifika kwa ubora na uendeshaji wake sasa zimetangazwa kuuzwa huku jijini Dar es Salaam hotel maarufu ya land mark iliyopo ubungo riverside ikibadili matumizi kutoka kuwa hotel mpaka hostel kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Hali hii inakuja huku kukiwa na  taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba - Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 umepungua kwa 4%.
Taarifa hizo zinaonyesha kuwa  Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita, sambamba na hayo, Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
 Taarifa hizo zinaonyesha zaidi kuwa Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporomoka kwa 7%.
Taarifa hizi  za kushuka kwa uchumi zinaenda sambamba na malalamiko ya kupungua kwa shehena ya mizigo katika bandari ya Dar es salaam kunakodaiwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za tozo za kodi tofauti na hapo awali.
Tofauti na malalamiko hayo ya kupungua kwa mizigo kunakodaiwa na serikali kupitia mamlaka ya mapato nchini  Tra kupandisha tozo hizo, taarifa iliyosambazwa na viongozi wa Tra mitandaoni inawaondoa hofu watanzania na kwamba kodi sio sababu ya mizigo kupungua.
Taarifa hiyo inakiri kuwa ni ukweli uliowazi kuwa kwa kiasi fulani mizigo imepungua kwa wastani wa asilimia 9-30 kutegemea na nchi, ambapo  mizigo mingi iliyokuwa inapita bandari ya Dar kwa kisingizio inaenda Kongo siyo kweli ilikuwa inaenda Kongo badala yake ilikuwa wana itumia  humu nchini.
Taarifa hiyo inazitaja sababu nyingine kuwa ni Kudorora kwa bei ya shaba Zambia,Uchaguzi mkuu wa  Zambia na kuimarika kwa  Msumbuji kiasi kwamba bandari ya Beira imeanza kufanyakazi vizuri.
Sababu nyingine ni Kuanza kutumika kwa utaratibu wa Single Custom Territory ambapo mizigo inalipiwa ktk bandari ya Dar kabla ya kusafirishwa kwenda Kongo ambapo inawanyima wafanyabiashara kule Kongo kukwepa kodi .

Sambamba na hayo sehemu ya taarifa hiyo inaonyesha kwamba hata katika  utafiti tulioufanya hata Bandari ya Mombasa mizigo imepungua, na kusema kuwa kupungua kwa mizigo katika bandari ya Dar hakujazuia kuongezeka kwa mapato na badala yake mapato yanayotokana na bandari yameongezeka maradufu tofauti na hapo awali
‘’Wakati meli zikiwa zimepingua katika bandari ya  Dar,  Mapato yatokanayo na Forodha mwaka 2015 yalikuwa wastani wa Shilingi Bilioni 200-300  kwa mwezi. Lakini tangu Disemba 2015 - August 2016 wastani wa mapato ya Forodha kwa mwezi ni Kati ya shilingi bilioni 400-550. Facts hizi zipo Mwananchi yeyote anaweza kuzipata kwenye tovuti yetu ya TRA Taarifa za Mapato kila mwezi.’’ Inasema taarifa ya mamlaka hiyo ya serikali
Wakati TRA wakisema hayo, hivi karibuni Gavana wa benki kuu ya Tanzania Professa Beno Ndulu ameuhakikishia umma kwamba hali ya uchumi wan chi ni shwari na kwamba kila kitu kipo sawa na kinachotokea sasa kiuchumi ni kuondoka ama kupungua kwa fedha za ujanaujanja mitaani na kubaki kwa fedha zinazotokana na shughuli rasmi.



No comments:

Post a Comment