WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Thursday, September 29, 2016

MAKALA : Ukodishaji wa Ndege Usiokuwa na Faida - RIPOTI YA CAG



Ukaguzi umebaini kuwa tarehe 9 Oktoba, 2007, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ilisaini mkataba wa ukodishaji wa ndege (Airbus namba A320-214 yenye usajili namba MSN630) kutoka Kampuni ya Wallis Trading Co. Ltd. Hata hivyo, mkataba wa kukodi haukufuata utaratibu muhimu na rasmi wa uendeshaji wa kampuni. 

Kwa mujibu wa taratibu hizi, Kitengo cha Ufundi ndani ya Kampuni kinawajibika kufanya uchunguzi wa ubora na kupata maelezo yote ya ndege kabla ya kuingia katika makubaliano yoyote ya kukodisha. Kwa upande mwingine, 

TCAA pia ni inawajibika kuchunguza na kukagua ndege ilikuhakikisha kwamba inaendana na viwango vya sayansi na ufundi wa vyombo vya anga vya kimataifa kabla ya kusajili ndege husika katika nchi. 

Nilibaini kuwa vitengo vyote viwili vya ufundi cha Kampuni ya Ndege Tanzania na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania lifanya uchunguzi wao kati ya tarehe 14 na 22 Januari, 2008 wakati mkataba wa kukodi ulikuwa umekwisha kusainiwa. 

Matokeo ya ukaguzi yalionyesha kuwa ndege haikufikia viwango vinavyohitajika hivyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga ilimpa maelekezo mkodishaji kurekebisha mapungufu yaliyoonekana kabla ya kukabidhi ndege hiyo kwa Kampuni ya Ndege Tanzania. 

Aidha, nilibaini kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo tarehe 8 Oktoba, 2007 aliishauri Kampuni kupitia barua yake yenye kumbukumbu no.JC/I.30/308/3 lakini ushauri wake haukuzingatiwa wakati mkataba wa kukodi ndege unasainiwa. 

Ili kutimiza matakwa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga kufuatia ukaguzi wao waliofanya, kampuni ya Wallis Trading Co LTD ilifanya matengenezo yaliyoelekezwa mwezi Februari, mwaka 2008. Hata hivyo, Mkodishaji hakukabidhi ndege kwa Kampuni ya Ndege Tanzania mpaka ilipofika mwezi Mei, mwaka 2008 baada tu ya Serikali kutoa barua ya dhamana ya thamani ya Dola za Marekani milioni 60 tarehe 2 Aprili mwaka 2008. 

ATCL ilikuwa ikigharamika kodi ya mwezi ya Dola za Marekani 370,000 kiasi kwamba kati ya Oktoba mwaka 2007 na Mei mwaka 2008 Kampuni ilikuwa ikidaiwa limbikizo la kodi la kiasi cha Dola za Marekani 2,590,000 kabla ya ndege kukabidhiwa rasmi kwa Kampuni ya Ndege Tanzania. Ndege ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita hadi mwezi Novemba mwaka 2008. 

Ilipofika mwezi Disemba mwaka 2008 ndege ilitupelekwa katika Kampuni ya Ndege ya Mauritius kwa uchunguzi mkubwa wa kiufundi ambapo ilikaa hadi mwezi wa Juni mwaka 2009. Mwezi Julai mwaka 2009 ndege ilihamishiwa kwenye Kampuni ya Ndege ya Ufaransa kwa uchunguzi wa C+12. 

Makadirio za matengenezo yaliyofanyika yalikuwa Dola za Marekani 593,560 dhidi ya gharama halisi ambapo iliongezeka kufikia Dola za Marekani 3,099,495 baada ya matengenezo ya kina kufanyika. Mmiliki alitoa dhamana ya kuchangia Dola za Marekani 300,000 tu na gharama nyingine kubebwa na Kampuni ya Ndege Tanzania. 

Matengenezo yalikamilika mwezi Oktoba mwaka 2010 lakini ndege haikuweza kurudishwa Tanzania kutokana na Kampuni ya Ndege Tanzania kushindwa kulipa gharama husika. Ndege ilikaa Ufaransa kwa kipindi chote cha mkataba wa kukodi hadi tarehe 17 Oktoba 2011 mpaka mkataba ulipositishwa. 

Wakati mkataba wa kukodi unasitishwa, gharama za kukodi kwa muda wa miezi 43 ambayo ndege hiyo ilikuwa chini ya matengenezo zilifikia Dola za Marekani 15,910,000. 

Jumla ya gharama ikijumuishwa na ada ya kila mwezi ya kukodi na gharama nyingine kama vile riba ilifikia Dola za Marekani 42,459,316. (sawa na Bilioni 90)

No comments:

Post a Comment