WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Monday, January 16, 2017

JAMII INAPASWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUANDAA MAZINGIRA MAZURI KWA WATOTO WA MITAANI.



Na, SABRINA MNZAVA

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgfecdgSWAKOmc_uufduqKhZ7eReiKlMjqhIKDjiomPO8rOTUdzwey4GHyU_EAfV6cOKxeDBo9BetPn2WNYdXicPnRmohVYdVOB4LytrFZcnIFOR8FrWotlsVFOUyMq4CXbEf39X84VKMgJ/s1600/4.jpg
Watoto wa mitaani kwa sasa tatizo linalokua kwa kasi kubwa hasa maeneo mengi ya mjini. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya na ustawi wa jamii kupitia idara ya Ustawi wa jamii zinaonyesha kuwa kwa jiji la Dar es salaam pekee lina zaidi ya watoto wa mitaani zaidi ya 5600. Hizi zikiwa ni takwimu za mwaka 2012 (Rapid Assessment 2012).

Kwa idadi hiyo inaonyesha jinsi tatizo hili linavyokuwa kwa kasi kubwa, lakini pamoja na kuwepo kwa vituo mbalimbali vya kulelea watoto hawa ikiwemo Dogodogo Center, Kihowede, Child in the Sun na vingenevyo vingi . Lakini bado tatizo la watoto hawa wadogo kuzurura mitaani huku wakiishi kwa kuomba omba, kuosha magari, na kulala mitaroni yakiwa maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wa jiji la Dar es salaam watoto hawa wamekuwa wakipatikana kwa wingi katika maeneo ya mwenge, morocco, posta, ubungo, maeneo karibu na daraja la Sarender na maeneo mengine. Itakumbukwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kwa wakati wa nyuma alipiga marufuku ombaomba wote kutoonekana barabarani katika mkoa wake lakini halikutekelezeka hata kidogo.

Sababu kubwa za kuongezeka kwa watoto hawa ambao kimsingi walistahili wawe shuleni wakipata elimu zimekuwa zikiongezeka kila kukicha. Lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Child in the Sun ikisaidiana na kituo cha Dogodogo Center zimeonyesha sababu kadhaa zikiwemo za uwepo wa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi ya ubungo, kuvunjika mfumo wa malezi katika familia. Nyingine ni vifo vya wazazi au walezi, ongezeko la watu wanaohamia Dar es salaam kutoka mikoani na maeneo mengine ya vijijini kuja kutafuta ajira na nyingine watoto kufuata misukumo ya watoto wenzao au ushauri mbaya wa watu waonaamua kuwatumikisha kwa faida zao.

Mbali na kuwepo kwa watoto hawa mara nyingi kumekuwa kukiripotiwa kwa matukio mengi ya kiuharifu yakiwahusisha watoto hawa. Mfano mzuri ni lile kundi linalosumbua jiji la Dar es salaam likijulikana kama Panya Road. Ambalo limekuwa likitumia silaha za jadi kufanya uharifu na unyang’anyi wa mali za watu. Na muda mwingine kukata watu mapanga na kuwasababishia maumivu na majeraha makubwa.

Mbali na matukio wanayoyatenda muda mwingi watoto hawa wamekuwa wakitendewa matendo maovu ikiwemo kubakwa, kulawitiwa na wengine kutendewa kinyume na maumbile pamoja na kupigwa na kutumikishwa huku kwa malipo kiduchu au kusaidiwa eneo la kulala au chakula. Matatizo haya ndiyo yamenifanya niandike makala hii ili kama jamii ione kuna haja kubwa ya kuwaokoa watoto hawa waishio mazingira hatarishi.

Nafahamu fika kuwa serikali imefanya jitihada mbalimbali kuwasaidia watoto hawa ikisaidiana na mashirika mabalimbali likiwemo lile la UNESCO, IMF, IOM, AMREF, Family Health International na mengineyo mengi. Lakini bado tatito liko palepale na wengine upelekwa kwenye vituo vya kulelea watoto waishio kwenye mazingira magumu lakini wengi wao hutoroka huku sababu kubwa wanayodai ni manyanyaso wayapatayo huko kwenye vituo hivyo.

Pia miradi mbalimbali imefanyika ikiwemo ile ya Rapid Assesment na mradi wa pamoja tuwalee, ili kusaidia kupunguza watoto waishio mitaani na walio katika mazingira hatarini lakini bado tatizo lipo. Kama jamii tunapaswa kujiuliza tumekosea wapi ili tuweze kujinusuru katika janga ili.

Watoto hawa walipaswa kuwa shuleni wakipata elimu itakayowasaidia kuwakomboa kimaisha na hapo mbeleni baadhi yao wangeweza kuwa hata viongozi wa taifa ili na kuwa tegemeo kubwa kwa taifa.Lakini cha kusitisha jamii imekaa kimya na kuliona hili si tatizo kubwa la kuifanya jamii ishituke.

Baadhi ya watoto hawa wameanza kujiingiza katika matendo ambayo hayafai katika jamii ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya huku wangali wadogo. Tujiulize kama jamii leo hii mtoto mdogo wa miaka kati ya 10 na 15 anatumia madawa ya kulevya tunatengeneza taifa gani?, Tunajenga taifa la watu wa aina gani?.

Na hapo hapo utawasikia watu wakisema watoto wa siku hizi wameharibika na kusahau kuwa tuna jukuma la kuilinda, kuielimisha jamii na kutunza maadili ya jamii ili tuweze kuwa na taifa lililo imara na bora kwa hapo mbeleni.  Nakumbuka kauli moja aliyowahi kuitoa mama Salma Kikwete kuwa mtoto wa mwenzio ni wako hivyo kama jamii inapaswa kujiweka tayari kusaidiana na serikali kuwasaidia watoto hawa watoke mitaani na kwenda kupata elimu shuleni itakayao wasaidia kujikomboa kimaisha na kujipatia maarifa.

Hivyo basi ni jukumu la jamii kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kuunganisha nguvu ili kuikomboa jamii katika janga hili ambalo linakuwa kwa kasi kubwa. Pia ni wakati wa taasisi na Asasi za kiraia kushirikiana na jamii ili kuwasaidia watoto hawa ili tuweze kujenga jamii isiyo na watoto wa mitaani.

0718156595.

No comments:

Post a Comment