Zitto Kabwe Adai Kuna Uhaba Mkubwa wa Chakula Nchini.........Waziri wa Kilimo Ampinga
Wakati Mbunge wa
Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akidai kuwa hali ya chakula
nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya, Serikali imesema hali ni
shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za wastani.
Zitto alidai
jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya chakula
kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na chakula
cha kutosha miezi miwili.
Kwa mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) ya Novemba inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya
Chakula (NFRA), imebaki na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni
cha kutosholeza siku nane.
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dk Charles Tizeba alijibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina
chakula cha kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali
zaidi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi.
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi.
“NFRA inanunua chakula
kwa kuangalia mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu wakivuna sana maghala
yao yanakuwa yamejaa na mahitaji ya chakula yanakuwa madogo ndiyo maana
Serikali hainunui chakula kingi. Miaka miwili iliyopita Serikali
ilinunua mahindi kwa wingi lakini yaliishia kuharibika,” alisema Dk
Tizeba.
Aliongeza kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga ghala jingine
lenye uwezo wa kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa lenye
uwezo wa tani 246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya
500,000.
“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko
watavuna kama kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje
ya nchi bila vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo
siwezi kutaja kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila
kinatosha siyo kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” alisema Tizeba.
Juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani
katika kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema
kauli ya Rais John Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba
Serikali haina shamba ni kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa
akiba ya chakula ya kutosha.
Alidai kuwa hali ya chakula nchini si
nzuri, wananchi wanashuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku
akidai kuwa bei ya sembe na mchele zimekuwa juu na gharama za maisha
zitaendelea kupanda kutokana na uhaba wa chakula kuwa mkubwa.
“Hali ya chakula inazidi kuwa
mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali kuhusu hifadhi ya
chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula
cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni,
hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula,”
alisema Zitto.
Aliongeza kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za
chakula wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa
na tani 459,561.
Takwimu alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika ripoti
ya BoT ya Novemba mwaka jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016
hadi Julai 2016, akiba ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi
49,632, lakini hadi Oktoba mwaka huo iliongezeka hadi 90,476.
Ripoti
hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa chakula kwa mwaka jana na miaka
mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014 Januari, kulikuwa na tani
235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka 2015 Januari kukiwa na
tani 459,561 na Desemba 180,746.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa
Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga alisema hali
halisi kwa wakulima siyo nzuri kwa kuwa mvua zilinyesha chini ya
kiwango, hivyo kuna hofu ya ukosefu wa chakula cha kutosha baadaye.
“Sasa hivi nipo Kiteto na kwa kawaida mahindi yalipaswa kuwa tayari
yameinuka kufikia walau mabega ya mtu mzima, lakini nikiyatizama sasa
bado yako chini.
"Mwaka huu kuna hatari ya ukosefu wa chakula na
naishukuru Serikali kwa kuwa imeanza kuchukua hatua katika maeneo yenye
uhitaji,” alisema Ruvuga.
No comments:
Post a Comment