ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza
imekataa wito wa kufutiliwa mbali kwa ziara ya kikazi ya Rais wa
Marekani Donald Trump nchini Uingereza kutokana na hatua yake ya kuzuia
wahamiaji kuingia nchini mwake.
Taarifa zinasema Downing Street imesema hatua kama hiyo itakuwa "ya kupendeza umma tu" bila kuzingatia mambo muhimu.Aidha, afisi hiyo imesema kwa sababu ombi la mwaliko tayari lilitumwa na likakubaliwa, kufuta ziara hiyo kunaweza "kufuta kila kitu".
Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn alikuwa amesema Waziri Mkuu Theresa May atakuwa anakosa kutekeleza wajibu wake kwa raia iwapo atakataa kuahirisha ziara hiyo ya Bw Trump.
Kuna ombi lililoanzishwa Jumamosi mtandaoni kutaka mkutano huo wa Trump ufutiliwe mbali.
Kufikia sasa, watu zaidi ya 900,000 wameidhinisha kuunga mkono pendekezo hilo.
Maombi ama hayo huhitaji saini 100,000 pekee kuhakikisha ombi kama hilo linajadiliwa na Bunge.
Ziara hiyo ya Bw Trump Uingereza ilitangazwa wakati wa ziara ya Bi May nchini Marekani.
Hata hivyo, hakuna tarehe maalum iliyotengwa ingawa ziara hiyo inatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, Ijumaa, Bw Trump alitia saini agizo rasmi la rais na kusitisha mpango wa Marekani wa kupokea wakimbizi kwa siku 120.
Alipiga marufuku wakimbizi wa Syria kuingia Marekani kwa muda usiojulikana na pia akapiga marufuku watu kutoka nchi saba zenye Waislamu wengi kuingia Marekani.
Hatua hiyo imeshutumiwa vikali na viongozi mbalimbali duniani.
Afisa mmoja wa Downing Street ameambia BBC: "Marekani ni mshirika muhimu sana. Lazima tufikirie kuhusu muda mrefu ujao."
Mwanasheria mkuu wa upinzani Uingereza Shami Chakrabarti amesema msimamo wa serikali ni kama "wa kumridhisha" Bw Trump.
Bw Corbyn ametoa wito kwa wafuasi wa chama chake kuunga mkono ombi la kufutwa kwa mkutano huo.
Kiongozi wa chama cha Liberal Democrat Tim Farron pia ameunga mkono wito huo.
"Ziara yoyote ya Bw Trump nchini Uingereza inafaa kuahirishwa hadi marufuku hii iondolewe," alisema.
Meya wa London Sadiq Khan amesema ziara hiyo haifai kufanyika iwapo marufuku hiyo itaendelea kuwepo.
No comments:
Post a Comment