- L CUF Zanzibar watofautiana
- L Habib Mnyaa apongeza uamuzi wa msajili
Na Meshack Katunzi.- JAMVI LA HABARI
SHILINGI milioni 369 zilizodaiwa kutoroshwa kutoka hazina na
kwenda katika akaunti ya Chama cha CUF wilaya ya Temeke, Januari 5 na baadae kugawanywa kwa watu mbalimbali, zinaelezwa ziliingizwa
kihalali kwa kufuata sheria na taratibu zote za kiofisi kama ilivyoelekezwa na
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jamvi la Habari linaweza kuthibitisha.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya chama cha
wananchi CUF ambaye ofisi ya msajili wa
vyama vya siasa haimtambui, Julius Mtatiro alikaririwa na vyombo kadhaa vya
habari akilalamikia juu ya alichokiita kuchotwa kwa fedha za ruzuku za chama
hicho kitendo alichokiita kupewa baraka na msajili wa vyama vya siasa Jaji
Francis Mutungi.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata,
zinaonyesha kuwa hakukuwa na tatizo lolote la kisheria, kimaadili wala kikanuni
katika utoaji wa fedha hizo ambazo ni sehemu ya fedha za ruzuku ambazo CUF
wanastahili kupata kutoka serikali kuu kwa shughuli za uendeshaji wa chama
hicho.
Taarifa hizo zinasema zaidi kuwa sio kweli fedha hizo
ziliingizwa katika akaunti ya wilaya ya Temeke isipokuwa kwa sasa, Temeke ni
jina tu la akaunti hiyo kama ambavyo akaunti nyingine zinaitwa Holland, Vijana,
Kijitonyama na kadharika, na kwamba akaunti hiyo ni halali na imehuishwa kwa
kubadilishwa matumizi yake kutoka kuwa akaunti ya wilaya mpaka kuwa akaunti
maalum ya taifa kwa kufuata vikao halali vya mashauriano ya chama hicho.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu aliye ndani ya serikali,
anasema ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ilipata uthibitisho pasi na shaka
kwamba akaunti hiyo ni halali kwa
kukipatia chama hicho ruzuku yao kama walivyoomba viongozi waandamizi
wanaofahamika na kutambulika na msajili wa vyama.
‘’Unajua msajili hajajiingizia tu zile fedha, CUF wenyewe
walileta maombi kuwa fedha zao kwa sasa ziingizwe katika akaunti namba fulani inayopatikana
sehemu fulani, ndipo msajili alipofuatilia na kuwataka watimize masharti yote
ya kikatiba ikiwemo kufuata vikao halali vya chama chao na kuwaingizia fedha
hizo baada ya kuombwa muda mrefu kufanya hivyo’’. Kilisema chanzo chetu
‘’Ukweli ni kwamba Msajili anaifahamu CUF moja tu, msajili yeye haifahamu kamati inayoongozwa na
Mtatiro na wenzake, anachofahamu msajili wa vyama vya siasa kuwa kuna CUF,
ambacho Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu wake, Maalim
Seif Sharrif Hamad, na manaibu wake Magdalena Sakaya na Nassoro Mazrui kila
mmoja’’ kiliongeza chanzo chetu.
Julius Mtatiro
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili linazo zinaonyesha
kuwa kitendo cha Profesa Lipumba
kumtambua na kuwa tayari kufanya kazi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kimempa moyo msajili kuwa
akuwapatia ruzuku kina Lipumba kutapelekea kazi za chama kizima kufanyika kwa
kuwa mara kadhaa Lipumba amekaririwa na vyombo vya habari akimuita ofisini
katibu mkuu wake kumpangia kazi za kufanya.
Tofauti na Katibu mkuu wa CUF Maalim Seif ambaye ameendelea kusisitiza kutomtambua Mwenyekiti
wake Lipumba bila kujali ukweli kwamba mamlaka iliyomchagua haikuwahi kurudhia
kujiudhulu kwake.
‘’katika akili tu ya kawaida, mwenyekiti wa chama ndio
kiongozi mkuu wa shughuli za kichama katika CUF, yeye anathibitisha anamtambua
Katibu Mkuu wake na yupo tayari kushirikiana naye kufanya kazi, Katibu Mkuu
yeye hataki kumtambua na anaendelea kuing’ang’ania Kamati ya Uongozi ambayo
kisheria haitambuliki, unafikiri ili chama kiendelee kupewa ruzuku na kijiendeshe,
nani angepewa ruzuku kama si Lipumba’’. Alisema
Chumi Kisyabo aliyeombwa na gazeti hili kutoa maoni yake.
‘’Kwa maoni yangu, kumpa ruzuku Lipumba ni kukifanya chama
chao kiende mbele kwa kuwa Lipumba ndio kiongozi mkuu wa chama na anawatambua
wasaidizi wake wote halali akiwemo Maalim Seif, na kumpa ruzuku Maalim Seif ni
kukidumaza chama na kuchochea mgogoro
kutokana na msimamo wa wake wa kutomtambua, kwa hili namuona msajili wa vyama
kama mtu aliyetumia akili nyingi sana kuutatua mgogoro huu’’. Alisema.
Maalim Seif Sharrif Hamad
Sakata la ruzuku la chama hicho kimeendelea kuchukua nafasi
katika vichwa vya habari mbalimbali ambapo jumapili ya Januari 15, 2017
anayejiita Mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa chama hicho, Mtatiro alishiriki kwa
njia ya simu mjadala kuhusu jambo hilo na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano
kwa Umma, Abdul aliyekuwepo studio katika
kituo cha Star Tv jijini Mwanza na wawili hao kushindana kwa hoja, katiba na
uzoefu wao ndani ya chama hicho huku kambaya akimtuhumu mtatiro kuwa ni mpiga
madili mzoefu.
‘’Namshangaa Julius(Mtatiro) leo analalamika sisi
kuingiza fedha hizi kwenye akaunti ya
diwani wetu na anasema ni wizi, wakati yeye mwaka 2011 aliingiziwa milioni mia
moja na nane (108) katika akaunti yake binafsi , sasa leo analalamika nini nay
eye mwenyewe aliwahi kumuingizia diwani huyo huyo milioni 46’’?. Alisema Kambaya.
Katika majibu yake, Mtatiro
alikiri kuingiziwa na kusema ziliingizwa kwababu ya kampeni za uchaguzi mdogo
igunga, japo akaunti ya wilaya hiyo ya igunga ilkikuwepo.
Katika hatua nyingine kiongozi mwandamizi wa chama hicho na
mbunge maarufu mstaafu wa Mkanyageni,
Habib Mnyaa alipiga simu studio hizo na kusema yeye kama mwanachama na kiongozi
mwandamizi wa chama hicho haoni shida kwa wao kuingiziwa fedha kwenye akaunti
hiyo kwa kuwa ni akaunti halali ya chama na kwamba kuziingiza kwenye akaunti
binafsi ya mtu ni jambo la chama ambalo halihusiani na msajili wa vyama.
‘’msajili hajaingiza fedha kwenye akaunti ya mtu binafsi,
msajili ameingiza fedha kwenye akaunti ya chama, na kwa hivyo hakuna tatizo
lolote kisheria, chama kimetumiaje hizo fedha ndio swala linaloweza kuibua
mjadala, na hata hivyo mamlaka ya ubadhilifu sio ya mtatiro ni mamlaka ya CAG,
hivyo hatuna haja ya kuwa na papara, tusubiri tuone matokeo ya msajili, kwenye
hili Msajili hana makosa na ninampongeza sana kwa kweli’’. Alisikika Mnyaa.
No comments:
Post a Comment