Na, BARAKA NGOFIRA
0763580901
waziri Jenista Mhagama akiwa na Mwenyekiti wa kamati ya maafa mkoani kagera mkuu wa mkoa huo Mustafa Kijuu.
Septemba kumi mwaka huu tetemeko la
ardhi lilikumba mikoa ya kanda ya ziwa huku janga kubwa likiwa limeachwa mkoani
Kagera ambapo zaidi ya watu 17 walipoteza maisha papo hapo. Mbali na maafa hayo
nyumba zaidi ya 2000 zilibomoka na kuharibiwa vibaya na kuwaacha wakazi wengi
wa mkoa huo wakiwa hawana makazi.
Serikali na wadau mbalimbali walifanya
kila liwezekanalo ili kupeleka misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula na
mablanketi kwa waathirika ili waweze kujihifadhi. Huku serikali na wadau
wengine wakikusanya nguvu ili kuwasaidia wanakagera kurudi kwenye hali yao
waliyokuwa wameizoea kabla ya kukubwa na tetemeko la ardhi.
Miundombinu ikiwemo barabara, umeme,
maji, shule na mingi iliharibiwa vibaya na tetemeko hilo. Shule kongwe za
Ihungo na Nyakato ni moja ya taasisi ambazo ziliharibiwa vibaya sana na
tetemeko la ardhi. Hali iliyosababibisha serikali kuwahamisha wanafunzi katika
shule nyingine ili waweze kuendelea na masomo huku juhudi mbalimbali zikifanywa
na serikali kurudisha shule hizo katika hali yake ya kawaida.
Salamu za pole kutoka kwa viongozi wan
chi mbalimbali zilitumwa nchini, na msaada kidogo kama kifuta machozi kwa
waathirika wa Kagera. Mashirika mbalimbali ya ndani ya nchi, taasisi za umma na
watu binafsi walitoa misaada mbalimbali ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko
la Ardhi.
sehemu ya madhara ya tetemeko la kagera.
Mbali na juhudi zote hizo vyombo vya habari
havikuwa nyuma kuuhabarisha umma kwa kila hatua iliyokuwa inaendelea juu ya
makusanyo mbalimbali ya kuchangia waathirika wa tetemeko la Kagera. Viongozi
mbalimbali hasa kutoka Ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa, walipewa muda
mwingi na vyombo vya habari ili Kutoa tathmini yao na wapi walipofikia bila
kusahau Kutoa msisitizo kwa raia watanzania na wadau mbalimbali wajitokeze
kuchangia janga hili.
Kwa kufanya hivyo jamii na mashirika
mbalimbali yalijitokeza kwa wingi huku baadhi ya wadau na wataalam wakiwemo
wale kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na vyuo mbalimbali walijitolea kufanya
tathimini bure kabisa. Ambapo walitumia pesa zao wenyewe kutathimini na kutoa
ushauri kwa serikali juu ya nini kifanyike ili kuirudisha Kagera na wakazi wake
katika hali ambayo waliizoa.
Wakati hayo yote yakiendelea mwanzoni
kabisa mwa zoezi hili kasoro iliingia kwa baadhi ya watumishi wa umma ambao
hawakuwa waamini ambao walitaka janga hili kwa ajili ya kujishibisha. Ambapo
baada ya kugundulika kufungua akaunti feki iliyokuwa na jina sawa na ile ya
kupokea misaada ya Kagera walitumbuliwa mara moja na kupelekwa mahakamani ili
kupambana na sheria.
Mbali na hao kutumbuliwa lawama nyingi
zilisikika kuwalalamikia viongozi hao kugawa misaada hiyo kwa watu kulingana na
itikadi za vyama. Ambapo wafuasi wa chama tawala walionekana kupewa upendeleo
huku wenzao wa vyama vya upinzani wakibaki kula kwa macho. Jambo ambalo
lilikemewa mara moja na viongozi wa ngazi ya juu ya serikali japo sina uhakika
kama lilikisha au la!
Huku hayo yote yakiendelea serikali
iliwatangazia wakazi wa Kagera kuwa wajijengee nyumba kwani serikali haina pesa
za kujenga nyumba kwani tetemeko halikuletwa na serikali. Kauli hii iliibua
maswali mengi miongoni mwa wadau na wakazi wa Kagera ambao walikuwa ni walengwa
wa kauli hiyo. Lakini wajipa moyo na kupiga moyo konde na kuendelea na ujenzi
japo wana hali mbaya. Ambapo mpaka leo wengi bado wanasubiri usiku uishe ndo
waanze kujenga huku hawana mbele wala nyuma na kukaa pasipo kujua wapi
wataanzia kujenga na chakula kubaki kukisikia
na kukiona kwa majirani.
Huku wakiwa wanaendelea na shughuli zao
za kujijenga kisaikolojia, mwanzoni mwa mwezi huu serikali kupitia mkuu wa mkoa
huo ilipigilia msumari wa moto kwenye donda ambalo halijapona. Baada ya
kuutangazia umma kuwa misaada iliyotolea na wadau na nchi wahisani zitatumika
kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya mkoa huo. Ambapo alikaririwa akisema
kuwa ni maamuzi ambayo yamefikiwa kwenye kikao cha kamati ya maafa ya Mkoa huo.
Lakini pia Rais wa Jamhuri ya muungano
wa Tanzania alilibariki jambo hilo na kusema kuwa pesa hiyo ya maafa itatumika
kujenga maghorofa mkoani humo ambayo anaamini kuwa hayatabomoka hata tetemeko
la aina gani lipite. Jambo ambalo lilizua maswali mengi miongoni mwa watanzania na kuzua gumzo kubwa
mitandaoni ndani na nchi za jirani. Swali kubwa likiwa ni kwa nini serikali
imeamua kuimarisha miundombinu ya mkoa huo huku watu wengi walioathirika wakiwa
hawana chakula na malazi.
Ambapo wadau mbalimbali waliona ni
uonevu na utapeli wa wazi wazi na kutojali wanyonge ambako kunafanywa na
serikali ya Tanzania nchini ya Rais Magufuli. Itakumbukwa kuwa misaada yote
iliamuliwa ikusanywe kwa mkuu wa mkoa wa Kagera ili iwe rahisi kugawanywa kwa
wananchi lakini hali imekuwa tofauti na matarajio ya wengi. Kwani serikali
imeamua kutumia nguvu na kuaamua kutumia nguvu na kubadilisha matumizi ya misaada
ya kibinadamu kwenda kwenye matumizi ya maendeleo.
Jambo ambalo lingeweza kungoja bajeti ya
mwaka mpya wa fedha au miradi ambao nchi wahisani wangeweza kusaidia nchi kama
wanavyosaidia miradi mingine ya maendeleo. Kilichofanywa na serikali na sawa na
msemo usemao aliyeshiba hamujui mwenye njaa, maana hata nguvu za kumsumbua
hana.
Sikatai kuwa kilichofanywa na serikali
ni kibaya la hasha bali naweza kusema ni kupungukiwa kwa ubinadamu na kuangalia
ni nini kifanyike kwanza, maisha ya wakazi wanao lala nje na kukosa chakula au
kuwajengea barabara na maghorofa ambayo wenye hela zao ndiyo watayafaidi na
kupitisha magari yao. Huku maskini wanaotembea kwa miguu au wenye baiskeli zao
wakiwa hawana mbele wala nyuma.
Hivyo basi ni vyema serikali ikatazama
upya kuhusu misaada hiyo na kutoa misaada ya kibinadamu kwanza ikiwemo chakula
na malazi kwa familia ambazo hazina uwezo au zina uwezo duni wa kipato cha
kumudu kujenga nyumba na kununua chakula.
Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa
mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza ya mawasiliano kwa Umma katika Chuo kikuu
cha Dar es salaam. Anapatikana kwa barua pepe ya barakangofira@gmail.com au simu
0763580901
No comments:
Post a Comment