Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles
Mwijage ameipongeza na kuishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa jitihada za kuendelea kuelimisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kulipa kodi utakaoiwezesha Serikali kusonga mbele katika suala zima na ukuzaji wa viwanda vya ndani hapa nchini.Mhe. Mwijage aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa mwaka wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa Msimbomilia (Barcode) za bidhaa (GS1); uliofanyika tarehe 29 Novemba 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya GS1 na TRA kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wadau wao, kujadili mambo muhimu ya kodi yanayohusu umuhimu wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika kuweza kupata msimbomilia (barcodes 620) na kuweza kuzitambulisha bidhaa za Tanzania kimataifa pamoja na kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage wa tatu kulia akikata keki kuadhimisha mwaka wa nne wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa Msimbomilia 620 (Barcode) za bidhaa (GS1) uliofanyika jijini Dar es salaam. Wa kwanza kushoto ni mwakilishi kutoka TRA ambaye ni Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi Bi. Rose Mahendeka na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya GS1 Bw. Gideon Mazara wakishuhudia tukio hilo.
Waziri Mwijage aliliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha kila mfanyabiashara anayemiliki viwanda vidogo na vya kati kuhakikisha anakuwa na TIN na namba ya msimbomilia 620 inayotolewa na GS1 Tanzania kabla ya kuhuisha vyeti vyao vya biashara.
Aidha Waziri Mwijage amesema kuwa uchumi wa viwanda
unatakiwa kukua nchini ili kuweza kuzalisha bidhaa bora
zitakazouzwa ndani na nje ya nchi na kukusanya kodi stahiki
itakayoiwezesha Serikali kutoa huduma bora za kijamii kwa
maendeleo ya wananchi wa Tanzania .
“Ifike wakati wafanyabiashara muwaelewe vizuri TRA na kulipa
kodi stahiki ya Serikali, ili nchi iweze kusonga mbele” alisema
Mhe. Mwijage.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (katikati) akielezea na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Shear Illusions Bi. Shekha Nasser (aliyeshika zawadi) kwa kulipa kodi stahiki ya Serikali ya kati ya Milioni 9 na 12 kila mwezi kupitia kampuni yake ambayo pia imeweza kutoa ajira kwa vijana zaidi ya12. Pongezi hizo alizitoa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa nne wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa msimbomilia (Barcode) za bidhaa (GS1) uliofanyika jijini dar es salaam.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bi. Rose Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka msimbomilia (Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kabla ya kwenda kupata huduma ya msimbomilia 620.
Bi. Mahendeka aliwasisitiza wadau hao kuhakikisha wanajisajili na TIN na wale waliojisajili kuhakikisha wanahakiki taarifa zao ili kurahisisha upatikanaji wa Msimbomilia 620 na kuiwezesha TRA kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara wazalishaji na wanaouza bidhaa zao nje ya nchi.
Baadhi ya wadau wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa Msimbomilia (Barcode 620) za bidhaa (GS1) wakimsikiliza kwa makini Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Rose Mahendeka akitoa elimu ya kodi wakati wa mkutano wa nne wa mwaka wa Taasisi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Wafanyabiashara wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka Msimbomilia(Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi(TIN) kabla ya kwenda kupata huduma” alisisitiza Bi. Mahendeka.
Aidha Bi. Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara ambao wanahitaji kuuza bidhaa zao kwa kutumia msimbomilia wanapaswa kulipa kodi bila ya kukwepa ili kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kufikia uchumi wa viwanda na vilevile kuweza kutoa huduma bora kwa maendeleo ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya GS1 Bw. Gideon Mazara alitoa rai kwa wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa kutumia Msimbomilia 620 wa Tanzania na kuweza kutangaza bidhaa za hapa nchini ili kupata soko la kimataifa litakalowezesha nchi kufikia uchumi wa kati .
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akiwa katika picha ya pamoja na baadi ya wadau wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa msimbomilia (Barcode 620) za bidhaa (GS1) mara baada ya kuhitimisha mkutano mkuu wanne wa Taasisi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment