zitto kabwe'
Majibu yangu Kwa HOJA za Nape Nnauye kuhusu muswada wa Huduma za habari, 2016
Ndugu yangu Nape Nnauye amejibu andiko langu nililolitoa
Jana kuhusu muswada tajwa.
Kama ilivyo ada ya Siasa za kijinga jinga
Nape amejibu andiko langu Kwa kunishambulia binafsi na kuweka Hoja zake
mbalimbali. Mimi sitamjibu Nape namna yake maana wenye busara
wametufunza ' when they go low go high '. Nitajibu Hoja za Nape Na
sitamjibu Nape.
Hata kwenye andiko langu sikutamka neno Nape Nnauye
kwani Siasa zangu sio Siasa za mtu bali za masuala. Sitahangaika Na mtu
bali Hoja ili kujenga.
#1 Hoja ya Kushirikishwa wadau: Nape anasema
" utungaji wa mswaada kuna hatua mbili za kutoa maoni.
Hatua ya kwanza ni pale ambapo serikali inapokuwa
inatengeneza mswaada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya
kiserikali kwa hatua za kuupitisha wadau HUSHIRIKISHWA ili kutoa maoni
yao. Na kwa mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari ,2016 WADAU
wameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni
yao UPO.
Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya mswaada
kusomwa mara ya KWANZA bungeni, Mswaada husika hukabidhiwa kwa Kamati
husika ya Bunge, na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma
na kutoa maoni yao( public document) kwa Kamati ya Bunge.
Hili pia limefanyika mpaka hatua ya wadau kuitwa na kuja
Dodoma ambapo waliomba mbele ya Kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya
kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati Ndg. Peter
Serukamba(mb) kwa uamuzi wa Kamati ya kudumu ya Bunge wakaamua
kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli
inayoendelea sasa."
Majibu ya Hoja hii
Kanuni za Bunge ( kanuni ya 84 ) zinataka kwamba Muswada
ukishasomwa Kwa mara ya kwanza Bunge lifanye MATANGAZO Kwa umma ili
kuhakikisha kuwa umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha Wananchi
kutoa maoni Yao.
Muswada huu kwanza Bunge halikutoa matangazo yeyote (
Kwa Taarifa tu Ni kwamba Hata Kamati ya Bunge ilishindwa kutoa photocopy
nakala za uchambuzi wa muswada kutoka Kwa wanasheria wa Bunge Kwa
sababu Bunge halina Fedha. Bunge halina Fedha kutoa photocopy ya nyaraka
za Wabunge kufanyia Kazi ).
Wadau wote waliokuja mbele ya Kamati ya
Bunge walitamka dhahiri kwamba wamepewa Taarifa ya kutokea mbele ya
Kamati Siku 2 kabla ya vikao Na hivyo wameomba muda zaidi wa kutoa maoni
Yao. Labda Ni kutokana Na uchanga wa shughuli za Bunge, Waziri anajenga
Hoja kwamba Ushiriki ulianzia kabla. Mtu yeyote anayejua namna Bunge
linafanya Kazi atakwambia muswada Ni muswada pale ambapo umechapishwa
kwenye gazeti la Serikali Na kusomwa mara ya kwanza Bungeni.
Wadau wote
waliiambia Kamati kwamba Kwa muswada huu Ndio walikuwa wanashirikishwa
Kwa mara ya kwanza pale mbele ya Kamati. Hivyo wadau hawakushirikishwa
kwenye muswada huu tangu umesomwa Kwa Mara ya kwanza Bungeni. Kama
Serikali ina ushahidi wowote ule kwamba kati ya Septemba Na sasa muswada
huu umehusisha mdau yeyote waweke wazi uthibitisho huo. Nyaraka
zinazoonyeshwa Na Serikali Ni za miaka ya nyuma kabla ya muswada kuwa
muswada. Ushirikishaji unaanza rasmi pale muswada upo gazetted Na
umesomwa Bungeni.
#2. Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC:-
"Mosi hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu; pili,
hakuna dhamira hiyo kwenye muswada huu; na tatu, serikali haina hata
wazo hilo."
Majibu ya Hoja
Itakumbukwa kuwa muswada wa awali ulikuwa Na kifungu hiki
Na wadau wakapiga kelele sana kukataa. Ukisoma muswada huu Kwa juu juu
utaweza kuona kuwa kifungu hiki hakipo. Mtu mwenye dhamira ovu huficha
huficha mambo yake. Kwenye muswada huu mambo mengi yaliyokataliwa Na
wadau sasa yamewekwa kiujanja Kwa kuweka Mamlaka hayo Kwa Waziri mwenye
dhamana ya Habari. Serikali inaposea hakuna kifungu hicho haisemi kuna
kifungu gani.
Nitawaeleza kifungu kilichowekwa ambacho ndicho kitatumika
na Waziri kufanya haya bila kuhojiwa Na mtu yeyote yule, kupitia
kanuni.
Sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari Fulani au masuala Fulani yenye umuhimu kwa Taifa.
Sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari Fulani au masuala Fulani yenye umuhimu kwa Taifa.
Serikali itatumia kifungu hiki kutekeleza jambo lile lile ambalo wadau walikataa kuwekwa sheria Siku za nyuma. Serikali italiweka Kwa mlango wa nyuma. Mbaya zaidi muswada unatamka wazi kwamba Waziri mwenye dhamana ataweka TERMS and CONDITIONS Kwa uendeshaji wa ' media houses'.
Hivyo
Hata wakifuta kifungu Hicho cha 7, bado Waziri kapewa Mamlaka makubwa
sana ya kuamua Chombo cha habari kinaendeshwaji. Ni dhahiri kwamba
Waziri ama anajua haya au kawekewa vifungu ambavyo yeye binafsi hajui
tafsiri zake lakini atashangazwa katika utekelezaji wa sheria. Kifungu
cha 60(2)(a) ( Minister to make regulations for TERMS and CONDITIONS for
OPERATIONS of licensed media house) inampa Mamlaka hayo Waziri kiasi
ambacho ataweza kuendesha vyombo vya habari atakavyo yeye. Muswada huu
unamfanya Waziri wa Habari kuwa Mhariri Mkuu wa Taifa.
#3. Mitandao ya kijamii:
"muswada huu unakusudia kuzibana blogs na kutaja mitandao
ya kijamii kama jamiiforums kuwa nayo itatakiwa kusajiliwa. Mtu huyu ni
wa kumwonea huruma. Bahati mbaya muswada huo hauna mamlaka wala nia
hiyo. Kifungu cha 3 cha Sheria kiko wazi kuwa usajili utahusu magazeti
na majarida na machapisho yao ya mitandaoni (magazeti mtandao ya
magazeti hayo rasmi na sio mitandao yote au mingine ya kijamii kama
anavyopotosha)."
Majibu ya Hoja
Muswada uliopo mbele ya kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana
sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya Muswada inatamka chombo cha
habari ni pamoja na gazeti, kituo cha radio na televisheni ikiwemo
mitandao ya kijamii ( online platforms).
Napenda umma wa Watanzania ufahamu kwamba muswada Ni wa
Kiingereza. Muswada wa Kiswahili Ni Kwa ajili tu ya kuwezesha Wabunge
wasiojua kiingereza kuweza kuelewa vifungu vya muswada. Muswada Ni wa
Kiingereza, Ndio rasmi. Mahakamani hawatatumia muswada wa Kiswahili Bali
muswada rasmi.
Tafsiri ya online platforms haikuwekwa kwenye muswada. Tafsiri ya media Ndio imeweka Hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote aende Google Na kuandika online platform atapata tafsiri Ni Nini. Nitsaidia kidogo hapa
Tafsiri ya online platforms haikuwekwa kwenye muswada. Tafsiri ya media Ndio imeweka Hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote aende Google Na kuandika online platform atapata tafsiri Ni Nini. Nitsaidia kidogo hapa
”Social media is defined as “online interactions among people in which they create, share, and exchange information and ideas in virtual communities, networks and their associated platform”. Serikali itatumia tafsiri hii ya kwenye muswada kubana mitandao ya kijamii. Hivi Watanzania mmesahau kesi ambazo Wananchi wanapewa kupitia sheria ya cyber crime? Hivi mnasahau kuwa Rais alisema anatamani mitandao ya kijamii Malaika washuke waizime? Malaika watashuka Kwa kupitia muswada huu. Muswada huu una nia ovu kabisa ya kukandamiza uhuru wa habari.
#4. "Ipo hoja ya Waziri kupewa mamlaka kuagiza chombo
chochote kutangaza jambo lenye umuhimu kwa umma: Katika hili pia
tumsamehe kwa sababu hahudhurii vikao vya Kamati wakati wa mijadala hii.
Hili limejadiliwa kwa kina na wahusika kuelewana. Hakuna kifungu
kinachompa mamlaka hayo Waziri.
Bali kifungu kilichopo kinaipa fursa Serikali
kuvishauri/kuvielekeza(Govt MAY) vyombo vya habari kuungana pamoja
kulinda maslahi ya Taifa kunapokuwa na jambo la muhimu kama vile nchi
kuwa VITANI au majanga makubwa. Zitto kama kijana wa Kitanzania kama
haoni umuhimu wa hili basi hakuna namna nyingine ya kumsaidia."
Majibu
Msomaji utaona dhahiri kuwa hakuna Hoja ya kujibu hapo.
Hivi CNN inaagizwa kisheria Na Serikali ya Marekani kuhusu kulinda Nchi
Yao? Hivi hapa Tanzania kuna Chombo cha habari binafsi ambacho kinaweza
kwenda kinyume Na Nchi wakati wa vita? Muswada umetaja vita? Maelezo ya
Waziri yanaonyesha dhahiri kuwa Serikali haina Hoja bali inahangaika
kuokoteza Hoja. Kwenye hili Sina la kujibu majibu yamo ndani ya maelezo
Yao.
#4 Kwamba muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa
masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti
lichapishwe habari aitakayo.
Majibu
Nimeeleza huko juu kuhusu Mamlaka haya ya Waziri wa Habari. Kifungu cha 60 kipo wazi sana.
#5Zitto anasema muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini.
Ni kweli muswada umetoa mamlaka hayo lakini Zitto ameamua kutosema ukweli wote.
Muswada unampa Waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au
kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku
yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu
majarida yanayotaka kuhamamsisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue
hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo.
Majibu
Nadhani wenye uelewa wanaelewa maana ya hili. Sina maelezo
ya kujibu hili kwani linajitosheleza. Nani anatafsiri maslahi ya umma?
Nani atafsiri kuwa sheria za Nchi zimevunjwa Kama sio mahakama? Kwanini
kabla ya Waziri kufungia vitabu au magazeti asipate amri ya mahakama?
Yeye Waziri Ni Nani Mpaka atoe tafsiri ya kitabu Fulani au gazeti Fulani
limevunja sheria?
#6. Zitto anazungumzia kuwepo kwa vifungu vya uchochezi
akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa. Kwanza katika hili
lazima ijulikane kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ukiwemo
Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966,
masuala yote yanayohusu kusababisha athari kwa usalama wa taifa ni ukomo
unaokubalika wa uhuru wa habari (allowable restriction to press
freedom).
Majibu
Sina maelezo katika hili. Wenye uelewa wanaelewa namna Hoja
za namna hii hutumika. Kiufupi masuala yote ya uchochezi yaliyokuwa
kwenye sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 yamerudishwa kwenye
sheria hii mpya. Sheria hii inakwenda mbali Na kusema " Hata ukitamka
jambo ambalo linaweza kujenga chuki ya Wananchi dhidi ya Serikali Ni
uchochezi ".
Mwisho
Napenda kutoa ushauri wa bure Kwa ndg. Nape Nnauye, kwamba
kujadiliana Kwa Hoja kuna Maslahi Kwa Nchi. Wote waliosoma andiko langu
wataweza kutofautisha vijembe, dharau, kulewa madaraka Na matusi kwenye
majibu ya Nape Na Hoja kwenye andiko langu. Katika andiko langu
sikumtaja Nape Kwa jina Kwa sababu najua anatimiza wajibu wake Kama
Waziri. Katika majibu yake kuanzia mwanzo Mpaka mwisho Ni vijembe tu.
Hii inaonyesha uwezo wetu mdogo wa kuhimili mijadala. Hii Ndio
inayofanya Watanzania tuonekane watu ambao hatukusoma au tulikwenda
shule lakini hatukuelimika.
Haiwezekani kwamba mtu yeyote ambaye ana Hoja tofauti Na wewe atakuwa ametumwa. Kwamba hatuna uhuru wa mawazo binafsi Na hivyo lazima tutumwe. Hii Ni hulka mbaya sana ambao sikutegemea Kama wanasiasa vijana wanaweza kuiendeleza. Lakini Kama kuna mtu ambaye amezoea kutumwa Hoja Ni dhahiri kwamba anaona mwengine yeyote mwenye Hoja nyengine katumwa Pia.
Ninaamini muswada huu Ni mbaya Na unadidimiza uhuru wa
habari. Ninaamini kuwa muswada huu Kama ulivyo haupaswi kujadiliwa Na
Bunge Kwa sababu unapaswa kuandikwa upya.
Muswada huu ukipitishwa hakuna
mchapishaji ( printer ) wa magazeti atakayekubali kuchapisha magazeti
Kwa sababu Kwa mujibu wa muswada Mkurugenzi wa Maelezo anaweza kuingia
kwenye mtambo wowote akiwa Na Polisi Na kuung'oa. Haya sio kwamba
hayajaanza kufanyika, yamefanyika. Wakati wa masuala ya UKUTA kuna
wachapishaji walikataa kuchapisha gazeti lolote lililokuwa na neno
UKUTA. Watu wa magazeti wanajua hili Na wanaweza kuthibitisha Kwa namna
wanayoona inafaa.
Mimi nimeandika. Nimetahadharisha. Nimetimiza wajibu wangu.
Zitto Kabwe
Njiani kwenda Maputo
21/10/2016
Njiani kwenda Maputo
21/10/2016
No comments:
Post a Comment