Maalim Seif Sharrif Hamad .
'' Maalim Seif naye aliitwa msaliti wa Wazanzibari kwa madai
kuwa mwaka 1984 ndiye aliyepika maneno kwenda kwa Mwalimu Nyerere dhidi
ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi. Kwamba ni maneno hayo
yaliyosababisha Jumbe aondolewe urais wa Zanzibar na kunyang’anywa vyeo
vyote alivyokuwa navyo kwenye chama cha CCM na Serikali.''
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alimuita rafiki yake
wa harakati za kisiasa aliyegeuka hasimu wake, Oscar Kambona kuwa
msaliti akisema kuwa alitumiwa na Wazungu kufitini Serikali ya
Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kambona naye kwa maelezo yake ni kwamba Mwalimu Nyerere
alimsaliti kwa sababu walishirikiana kudai uhuru wa nchi baada ya kuwa
rais, alimfanya aishi kama mkimbizi nchini Uingereza.
Usaliti katika siasa ni jicho la mtu. Kama mlikuwa pamoja kisha mkatofautiana, neno msaliti lazima lipewe nafasi.
Oscar Kambona.
Mwalimu Nyerere alimuita Bibi Titi Mohamed ni msaliti, vilevile mwanamke huyo wa shoka alidai kusalitiwa na Mwalimu Nyerere.
Usaliti kwenye kamusi ya kisiasa ni kutofautiana. Mnapokuwa
kwenye chama kimoja cha siasa kisha mkawa hamuendani na mambo fulani
fulani, lazima atokee mtu wa kumuita mwenzake msaliti.
Wanasiasa hulitamka neno msaliti wakijua kabisa ni baya. Usaliti kwa maana yake ni kitendo cha kwenda kinyume na makubaliano.
Tafsiri hiyo haipo kwenye kamusi ya wanasiasa. Wao ndani ya
chama kimoja wanapotofautiana mitazamo huo huitwa usaliti. Anayeanza
kumtamka mwenzake mara nyingi ndiye hufanikiwa.
Bibi Titi Mohamed katika moja ya matukio ya kihistoria.
Neno usaliti linavunja heshima, linachafua, kwa hiyo
ukishaitwa hivyo, unakuwa kama vile umemwagiwa takataka ngumu, popote
unapopita watu watanyoosheana vidole kuwa wewe ni msaliti.
Usaliti ni ‘ukutiukuti’
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad alimsema aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika
Bunge la Tisa, Hamad Rashid Mohamed kuwa ni msaliti aliyehongwa fedha
ili awagawe Wazanzibari katika kudai haki zao ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Maalim Seif naye aliitwa msaliti wa Wazanzibari kwa madai
kuwa mwaka 1984 ndiye aliyepika maneno kwenda kwa Mwalimu Nyerere dhidi
ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi. Kwamba ni maneno hayo
yaliyosababisha Jumbe aondolewe urais wa Zanzibar na kunyang’anywa vyeo
vyote alivyokuwa navyo kwenye chama cha CCM na Serikali.
Hata sasa, Maalim Seif anamuita Profesa Ibrahim Lipumba
msaliti ni kama ambavyo Lipumba naye alivyosimama kidete kumshughulikia
Hamad Rashid kwa hoja ya usaliti. Kimsingi usaliti kwenye siasa ni kama
mchezo wa watoto kuzunguka kwa mduara ambao unaitwa ukutiukuti.
Seif aliitwa msaliti wa Wazanzibari kipindi cha Jumbe, naye
sasa anawaita Rashid na Lipumba jina hilo. Akina Lipumba pia hoja yao
ni kwamba Maalim Seif ni msaliti. Ni kutuhumiana na kuchafuana.
Mgogoro wa Rashid CUF ulitokana na dhamira yake ya kuwania
Ukatibu Mkuu, cheo ambacho kipo kwenye mikono ya Maalim Seif. Rashid
katika kutetea dhamira yake alisema kuwa Maalim Seif baada ya kupata
Umakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alikidhoofisha chama.
Rashid alitaka Maalim Seif aache Ukatibu Mkuu wa CUF ili
yeye ashike nafasi hiyo apate kukijenga chama. Ni hapo ndipo usaliti wa
Rashid ulisemwa kila upande. Kashfa mbaya zaidi aliitwa msaliti wa
Wazanzibari.
Ipo hoja inayozungumzwa dhidi ya Maalim Seif. Vinazungumzwa
vipindi ambavyo moto uliwaka kati ya CUF na polisi, haipo mara moja
ambayo Maalim Seif alisimama mstari wa mbele, mara zote haonekani.
Upande wa Lipumba hivi sasa wanasema kuwa zipo picha
zinazomuonyesha akiwa chini ya ulinzi wa polisi na zile ambazo amepigwa
na kuumizwa. Wanahoji zilipo picha Maalim Seif akiwa CUF zenye
kumuonyesha akipambana na polisi, kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi
au za kupigwa japo mara moja.
Machafuko makubwa ya kisiasa kuwahi kutokea nchini ya
Januari 26 na 27, 2001, Zanzibar na Dar es Salaam, wanasema Lipumba
alipigwa, kuvunjwa mkono na kuwekwa mahabusu pamoja na wafuasi wengine
wengi wa CUF. Wanahoji Seif alikuwa wapi? Hitimisho lao ni kuwa Seif
ndiye msaliti.
Kikwete na Lowassa
Kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, aliyetumika katika Serikali
ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa ni kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete
alimsaliti kwa sababu walikubaliana kushirikiana kisha kuachiana
uongozi.
Siri hii iliyotoka kwa Lowassa ni kuwa katika Uchaguzi Mkuu
mwaka 2005, hakuchukua fomu ya kugombea urais kwa sababu alimuunga
mkono JK na makubaliano yakawa baada ya JK kumaliza muda wake, alipaswa
kumsaidia Lowassa.
Edward Lowassa Mjumbe wa Kamati kuu CHADEMA.
Vilevile, Lowassa naye anaitwa msaliti, aliyejaribu
kumzunguka JK alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mwenyekiti wa CCM. Zipo fitina ambazo Lowassa anatuhumiwa kuzitengeneza
ili kumdhoofisha JK.
Katika siasa unapomuona mtu anaitwa msaliti, usikimbilie
kumhukumu, maana ukimuuliza naye atakutajia wasaliti wake. Anayeita
wenzake wasaliti, ukifuatilia upande wa pili naye jina hilo linakuwa
linamhusu.
Usaliti kwenye siasa ni vita ya masilahi. Ukionekana
unaingilia masilahi yake lazima akuite msaliti. Katika siasa kama
mtatofautiana bila kuathiri masilahi ya kila upande ni vigumu neno
usaliti kusikika.
waheshimiwa Edward Lowassa na Jakaya Kikwete wakiwa jukwaani.
Popote utakaposikia mwanasiasa ameitwa msaliti, ujue kuna
masilahi ya watu kaingilia. Na ukisikia mwanasiasa anamuita mwenzake
msaliti, tambua masilahi yake yameguswa.
Profesa Abdallah Safari alitofautiana na Lipumba CUF,
lakini hakuitwa msaliti kwa sababu hakuonekana kugusa masilahi ya
Lipumba. Safari hakuwa na madhara kwa uenyekiti wa Lipumba.
Rashid aligusa masilahi ya watu alipotaka kushika nafasi ya katibu mkuu ndiyo maana vita ilikuwa kubwa.
Usaliti Chadema
Kote wanaweza kuitana wasaliti, lakini Chadema
wamenyoosheana zaidi vidole. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho
Tanzania Bara ambaye sasa ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kabwe ana rekodi pana ya kuitwa jina hilo.
Dkt. Slaa akiwa na Zitto Kabwe.
Zitto aliitwa msaliti kwa sababu ya kutofautiana na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk
Willibrod Slaa. Hoja kuu iliyojengwa ni kuwa Zitto alikuwa anapokea
fedha nyingi kutoka CCM na Serikali yake na kuzitumia kukivuruga chama.
Kabla ya Zitto, aliyeitwa msaliti ni aliyekuwa Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Chacha Wangwe baada ya mzunguko huo, Dk Slaa
naye akawa msaliti kuanzia mwaka jana mpaka sasa.
Usaliti hata Urusi
Usaliti ni vita ya masilahi; Katika Chama cha Ujamaa wa
Kidemokrasia cha Urusi na baadaye Chama cha Kikomunisti, kulikuwa na
vijana wanne wenye maono na itikadi za kikomunisti ambao ni Leon
Trotsky, Joseph Stalin, Grigory Zinoviev na Lev Kamenev. Hapo ni kuanzia
mwishoni mwa Karne ya 19 mpaka katikati ya Karne ya 20.
Mwaka 1917, Urusi na Dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti
vikiwa chini ya uongozi wa nembo ya ukomunisti, Vladimir Lenin, vijana
hao wanne waliingizwa kwenye chombo kikuu cha uamuzi katika chama na
Serikali (Politburo) kama sehemu ya wajumbe saba waanzilishi.
Trotsky alimuunga mkono Lenin waziwazi na alionekana ni
kijana mwenye akili nyingi maana baadhi ya dhana zake za kiuongozi
zilitumiwa pia na kiongozi huyo. Watu wengi Urusi wakati huo, waliamini
mwisho wa Trotsky ungekuwa kuongoza Dola ya Kisovieti.
Stalin hakumpenda Trotsky na alimuona ni mtu hatari kwa
masilahi yake ya kisiasa, kwa hiyo akawashawishi Zinoviev na Kamenev,
wakaunda utatu wa kisiasa na kidola ambao waliuita Triumvirate,
wakijilinganisha na utatu wa Julius Caesar, Pompey na Crassus
waliounganisha nguvu ili kuitawala Roma miaka 60 Kabla ya Kristo.
Trotsky akajikuta kwenye mapambano na Triumvirate. Stalin
hakuwa na ushawishi mkubwa, hivyo aliwatumia Zinoviev na Kamenev
kumshughulikia Trotsky kwenye chama na serikalini. Trotsky akaitwa
msaliti jina likakua.
Baada ya Trotsky kupungua nguvu, Stalin aliwageuka Zinoviev
na Kamenev akawachachafya kuwa nao ni wasaliti. Alifanikiwa maana
Aprili 3, 1922, Stalin alikamata mamlaka ya chama na Dola ya Kisovieti.
Hata baada ya kukamata nafasi hiyo, Stalin alimhofia
Trotsky, hivyo ili kuzidi kumchafua alihakikisha anatambulika rasmi
serikalini kama msaliti kwa jina la Yuda Trotsky, yaani Msaliti Trotsky.
Oktoba 23, 1926, Stalin alitumia mamlaka yake kushawishi na kumfukuza
Trotsky kwenye chama na kumuondoa kwenye vyeo vyote.
Mwaka 1940, Trotsky aliuawa na ikaaminika kuwa Stalin
alihusika na mpango huo wa mauaji. Upande mwingine, Zinoviev na Kamenev
walimuona Stalin ni msaliti na mtu hatari, maana walishirikiana kwa
utatu wao kumshughulikia Trotsky baada ya kufanikiwa aliwageuka.
Mwandishi wa makala haya ni Luqman Maloto, mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa.
Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao
No comments:
Post a Comment