Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Wanafunzi wakiwa darasani kwenye shule ya Youth for Technology Foundation mjini Nairobi
Katika kile kinachoonekana kama jitihada za kutimiza na kutekeleza
ahadi zake kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao, Serikali ya Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya, imetangaza rasmi kuanza kuwapa wanafunzi wote wa
shule za msingi za umma nchini humo vipakatalishi, yaani laptop kuanzia
Ijumaa Septemba 30 na litakamilika katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mara tu baada ya kuchaguliwa mwaka 2013, Rais Kenyatta aliahidi
kuyafanya masomo kuwa kwenye mfumo wa kidigitali kwa kuwapa wanafunzi
wote wa shule za umma nchini humo vipakatalishi hivyo.
Likiwa ni zoezi lililotarajiwa kwa hamu kubwa kote nchini, serikali
hatimaye imeanza mchakato wa kuwapa wanafunzi wa shule za msingi za umma
vipakatalishi vitakavyowawezesha kufuatilia masomo katika mfumo wa
kidigitali. Japo zoezi hili halijafika wakati alioutangaza Rais,
serikali yake imekuwa mbioni kuhakikisha kuwa ahadi muhimu alizozitoa
mara tu baada ya kuchaguliwa kwake zinatimizwa.
Waziri wa Elimu nchini humo, Fred Matiang’i anasema kuwa
vipakatalishi hivyo vimeundwa kwa mtaala wa kisasa na hivyo basi
utawawezesha wanafunzi na shule za umma kuukumbatia mfumo wa kidigitali
unaokumbatiwa na mataifa yaliyoendelea. Bwana Matiang’i akiahidi kutoa
tangazo la kuidhinishwa kwa mtaala mpya wa mafunzo kwa walimu kote
nchini.
Naye waziri wa Sayansi na Teknolojia, Joe Mucheru aanasema kuwa
serikali tayari imewapa mafunzo ya kutosha walimu watakaobeba jukumu la
kuwaongoza wanafunzi kote nchini kupata mafunzo muhimu jinsi ilivyo
katika mtaala.
Suala ambalo limeonekana kuwa tete ni iwapo shule za msingi za umma
takriban milioni moja nukta mbili zimejengewa miundo msingi inayofaa
kama vile umeme. Waziri wa Kawi Charles Keter anaeleza kuwa shule zote
zitakuwa na umeme kabla ya mwaka huu kumalizika.
Zaidi ya vipakatalishi 1,060 tayari vimepokelewa nchini na nyingine zipatao 22,000 zikitarajiwa kufika nchini kila wiki.
No comments:
Post a Comment