''Mhe rais, chukuwa hatua. Sitisha fedha za malipo hayo
haramu tuonawalipa PAP kila mwezi. Fumua shirika letu la umeme kwa
kuondoa matapeli wote hasa wale ambao wapo kwenye eneo la sheria. Hawa
wana undugu wa damu na matapeli''.
Harbinder Singh Sethi kushoto na Joseph Makandege Kulia.
MHE RAIS, KATIKA HILI LA IPTL, BORA LAWAMA KULIKO FEDHEHA!
------------------------------
------------------------------
Mhe Rais, pole na majukumu mazito ya kuiongoza nchi katika
mazingira magumu. Natambua pia kazi kubwa uliyonayo hasa ya utekelezaji
wa ahadi zako kwa wananchi hasa ile ya kulinda fedha za umma.
Mhe Rais, nchi yetu kwasasa inapitia wakati mgumu hasa wa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Inasikitisha kwamba, bado nchi hii inakabiliwa na upungufu
mkubwa wa dawa mahospitalini na wanafunzi wengi ambao uliwaahidi kuwa
wangepata mikopo kwajili ya elimu zao za juu, wengi wao wamekosa mikopo
hiyo.
Mhe rais, lengo langu sio kuainisha ugumu ambao tunapitia
kama taifa, kwasababu nikifanya hivyo, huenda andiko hili likawa refu
sana au kuitwa la kichochezi. Muhimu nimelenga kukuonesha au kukumbusha,
eneo ambalo linakutia doa sana au kukupa sifa mbaya katika vita ya
kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na aina zote za uhujumu uchumi
wa nchi yetu. Matarajio ya wengi ni kukuona ukiwa na 'ZERO TOLERANCE'
kwenye eneo hili.
Swala la IPTL ni tatizo kubwa kwa nchi yetu kwasababu sio
tu kwamba linatutia hasara kama nchi, bali linakufedhehesha kama
kiongozi wa nchi.
Wengi wetu tumeshindwa kuelewa hasa ni kipi ambacho
kimepelekea matapeli hawa kuendelea kuturudisha nyuma kama taifa na
wakati tunaye rais ambaye anaonekana kujipambanua kushughulika na wezi,
wahujumu uchumi na wala rushwa?
Tunajiuliza, hivi kiongozi wetu wa nchi ambaye ameonesha
nia ya kubana matumizi ya serikali na kupunguza anasa katika utumishi wa
umma, anaweza vipi kushuhudia utapeli wa mchana kweupe uliofanywa na
unaoendelea kufanywa na matapeli wa ndani na wa nje bila kuchukuwa hatua
yoyote? Binafsi siamini kama umeshindwa kuchukuwa hatua dhidi ya
matapeli hawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombr Magufuli.
Mhe Rais, hukumu ya ICSID inatutaka tuwalipe SCB HK ambao ndio wamiliki halali wa IPTL kiasi cha shilingi bilioni 320($148m).
Mwaka 2013 tuliwalipa PAP(matapeli) zaidi ya bilioni 300.
Hii ni baada ya matapeli hao na ndugu zao kutoka shirika letu la umeme
kwa baraka za baadhi ya viongozi wa serikali kukutana pale Kunduchi
Beach Hotel & Resort October 3, 2013 kuanzia saa 17:00-02:38 kwajili
ya kupanga namna ya kutupiga bila sisi kujua.
Kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 6 na ajenda 6, pamoja na
mambo mengine, kilifanikiwa kubadilisha hukumu halali kwa kuamua fedha
za kwenye A/C ya Tageta Escrow pamoja na mitambo ya uzalishaji umeme,
vyote vikabidhiwe kwa PAP.
Mhe rais, pamoja na BOT kuiandikia wizara ya nishati na madini barua ya kutowaruhusu PAP kutoa fedha kwenye A/C(Nov 28 & 05 Dec 2014),matapeli hao walifanikiwa kutoa fedha hizo na kuanza kugawana kama peremende.
Mhe rais, matapeli hao hasa wale ambao wako kwenye shirika
letu hodhi na wale wa wizara husika licha ya kwamba mpaka leo wapo
salama kabisa, watu hao na wengineo ambao ni ndugu wa damu na tabia,
wamezoea kutubia.
Ni hisia zangu kwamba swala kwamba tunaibiwa huwenda
unalifahamu.
Utakuwa na kumbukumbu kwamba 2012 tuliwalipa isivyo rasmi
Dowans zaidi ya bilioni 140 ambazo hadi leo hazipo kwenye vitabu vya
bajeti.
Hata tukiwalipa SCB HK hizo dola 148m hiyo haitakuwa mwisho
wa kuibiwa na matapeli hao kwakuwa tayari tunalo deni la kulipa katika
siku za usoni ambalo chimbuko lake ni utapeli uliofanyika dhidi ya
kampuni ya Symbion kwa sisi kuvunja mkataba nao wa miaka 15 baada ya
kugundua ulikuwa wa kitapeli. Business as usual!
Mhe rais, licha ya serikali yako kukosa bilioni 42.5 sawa
na 68% za kuipa MSD kwajili ya dawa hospitalini mwezi July mpaka
September, kila mwezi tunawalipa IPTL zaidi ya bilioni 7 kila mwezi
kwajili ya mitambo inayotokana na mkataba huo wakitapeli. Inauma sana
kwasababu hatupaswi kuwalipa fedha zinazotokana na kitu haramu.
Mhe rais, chukuwa hatua. Sitisha fedha za malipo hayo
haramu tuonawalipa PAP kila mwezi. Fumua shirika letu la umeme kwa
kuondoa matapeli wote hasa wale ambao wapo kwenye eneo la sheria. Hawa
wana undugu wa damu na matapeli. Hawa wanatuhujumu.
Hawana tofauti na
vibaka wa Kariakoo wanaojifanya wanamfukuza mwizi kumbe ni ndugu yao.
Bila kufanya hivyo, hatua yoyote utakayochukuwa, Matapeli hao kwa kujua
ndugu zao ndio wako kwenye safu ya ulinzi, watakimbilia mahakamani na
watatushinda vizuri tu.
Mhe rais, kwasababu chimbuko la utapeli mwingi hutokana na
upungufu wa nishati ya umeme, ruhusu mashirika na makampuni binafsi
kuzalisha nishati hiyo. Hii itaongeza ufanisi utakaotokana na ushindani
baina yao.
Wananchi tunahitaji Nishati ya umeme sio nishati ya umeme
inayotokana na la shirika la umma. Tunahitaji iwe kama kwenye
huduma za usafiri wa anga ambapo ATCL inashindana na mashirika binafsi.
Mhe rais, washughulikie wote ambao wametuumiza na
wanaoendelea kutuumiza.
Kwa kufanya hivyo, utakuwa umeweka precedent
sahihi na hisia kwamba unawalinda mafisadi na matapeli Hawa
hazitakuwepo. Najua wapo wakubwa, washughulikie tu utakumbukwa kwa hilo
na hapa ndipo nia yako ya kupambana na ufisadi itakapodhihirika kwa
usahihi wake.
Bora lawama kuliko fedheha!
Matarajio ya watanzania ni kusikia kishindo kizito katika
siku za hivi karibuni cheenye baraka zako au ukimya wenye baraka zote
kutoka kwako.
Mungu ibariki Tanzania.
IMEANDIKWA
Na. Bob Chacha Wangwe
October 16, 2016
October 16, 2016
No comments:
Post a Comment