Zitto Kabwe Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT WAZALENDO
Ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto juu ya kuwasilisha Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2016
Dodoma ,
Jumanne 18 Oktoba 2016,
Ndugu Wanahabari na Watanzania kwa Ujumla
Oktoba 8 mwaka huu, chama chetu cha ACT Wazalendo kilifanya
Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia (MMK) nchini, mkutano ambao ulifanyika
katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es salaam. Lengo la
mkutano husika lilikuwa ni kuwapa fursa Wanachama, Wafuasi, Wapenzi wa
chama chetu, Wanaharakati, Wanahabari pamoja na Wananchi wa kawaida
(ambao si wanachama wa ACT Wazalendo) ya kujadiliana kwa upana na
Viongozi mbalimbali wa chama chetu juu ya masuala mbalimbali yahusuyo
nchi yetu, ikiwa ni utaratibu mpya wa kisiasa nchini.
Baada ya hotuba kutoka kwa viopngozi na wageni mbalimbali,
pamoja na mijadala mipana kutoka kwa wanachama na wananchi mbalimbali,
Mkutano Mkuu wa wa Kidemokrasia (MMK) ulitoa MAAZIMIO Kadhaa ya Kisera
juu ya chama chetu na taifa kwa ujumla, maazimio ambayo ACT Wazalendo
tuliahidi kuyabeba Na kuyapeleka kwenye Vikao vya Maamuzi ili yajadiliwe
na kupitisho kuwa maamuzi rasmi ya chama. Mojawapo ya maazimio hayo ni
suala la kuibua upya Mchakato wa Katiba Mpya nchini kwa kuanzia
ilipoishia Tume ya Jaji Warioba.
Suala jengine lililoibuka ni juu ya Sheria Mpya ya
“Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Na Gesi Asilia” iliyotungwa
na Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ili
kuanzisha kampuni ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia Zanzibar ZPDC
ambayo itashiriki katika shughuli za utafutaji na uendelazaji wa Mafuta
na kesi asilia kwa niaba ya serikali ya Zanzibar. Sheria husika
ilitungwa na kupitishwa mwezi huu na Baraza hilo la kutunga sheria
Zanzibar katika vikao vyake vilivyomalizika karibuni.
Mjadala mpana katika Mkutano wetu Mkuu wa Kidemokrasia
(MMK) ulionyesha kwa dhahiri kuwa pamoja na Baraza la Wawakilishi la
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutunga Sheria hiyo, bado Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) haipati “Uhalali wa Kisheria na Kikatiba”
juu ya usimamizi, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa
upande wa Zanzibar.
Wanasheria mbalimbali walieleza kuwa vikwazo vya Kisheria na Kikatiba vitawafanya hata Wawekezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia kutothubutu kufanya uwekezaji Zanzibar, na hivyo kuwanyima fursa Wazanzibari ya kufaidika na rasilimali za Taifa letu.
Wanasheria mbalimbali walieleza kuwa vikwazo vya Kisheria na Kikatiba vitawafanya hata Wawekezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia kutothubutu kufanya uwekezaji Zanzibar, na hivyo kuwanyima fursa Wazanzibari ya kufaidika na rasilimali za Taifa letu.
Sekretarieti ya chama cha ACT Wazalendo ilikaa na kufanya9
uchambuzi juu ya masuala yote ya Kisera ambayo yaliibuliwa katika
Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia (MMK). Na Miongoni mwa mambo ambayo chama
chetu kupitia vikao vyake halali kimeamua kuyabeba ni hilo la “Sheria ya
Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia”, ambayo
baada ya mjadala mpana wa Kisheria ilionekana ni dhahiri kuwa Sheria
husika ni batili kwakuwa inakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kamati ya Katiba na Sheria ya Chama cha ACT Wazalendo
kupitia mimi Mbunge wake imeonelea ni vema kuwasilisha Bungeni “Mswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Tano (15) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2016” (juu ya masuala ya Mafuta na Gesi
Asilia Zanzibar). Lengo la mabadiliko hayo likiwa ni “Kuiwezesha
Zanzibar Kupata Uhalali wa Kisheria na Kiakatiba juu ya Uendelazwaji wa
Sekta ya Mafuta Na Gesi Asilia”.
Na hivyo kuondoa vikwazo vya Kikatiba na Kisheria vilivyoko
sasa ambapo mamalaka hayo ya Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa
Mafuta na Gesi Asilia bado Kisheria na Kikatiba yako chini ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hata mara baada ya kupitishwa kwa
Sheria hii ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
Pamoja na kwamba ACT Wazalendo tumeamua kupigania kuufufua
upya Mchakato wa Katiba Mpya lakini bado tumeonelea umuhimu mkubwa wa
kuleta Bungeni mabadiliko haya ya 15 ya Katiba tuliyonayo sasa,
mabadiliko ambayo yatanusuru uvunjwaji wa Katiba tuliyonayo sasa ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kusubiri Katiba Mpya hakuhalalishi Katiba ya Mwaka 1977 tuliyonayo sasa kuvunjwa. Kwa kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya umekwama bila Kauli ya Serikali wala Muafaka wa Kitaifa juu ya lini mchakato huo utaendelea, "Muswada huu Binafsi" ni hoja ya lazima kwa sasa katika kuhalalisha hatua ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya kutunga sheria juu ya Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Upande wa Zanzibar.
Ni imani yangu, pamoja na changu kuwa Bunge litaona busara
iliyoko mbele ya Mswada huu, na kwa Uharaka itaona umuhimu wa kuruhusu
mjadala wake Bungeni ili kutoifanya Sheria hii ya Baraza la Wawakilishi
Zanzibar kuwa kero Mpya ya Muungano wetu.
Naamini, nitaweza kushirikiana na Wabunge wenzangu Bungeni,
pindi mswada huu utakapopangiwa tarehe ya kuletwa kwaajili ya mjadala,
kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu wa kizalendo wa kuhakikisha
Watanzania Wote, kutoka pande zote mbili za Muungano, wanafaidika na
Rasilimali za Taifa letu.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment