Urusi inapeleka ndege zaidi nchini Syria kuimarisha operesheni zake za angani, limeripoti gazeti la nchini Urusi. Haya yanajiri Marekani ikisema juhudi za kidiplomasia kuumaliza mzozo wa Syria ziko katika 'hali mahtuti'.
Gazeti la Izvestia limeandika kwamba ndege kadhaa chapa Su-24 na Su-34 zimewasili katika kituo cha anga cha Hmeymin nchini Syria.
Wakati huo huo Urusi imekanusha taarifa kwamba operesheni zake ndani ya Syria ambazo sasa zimetimiza mwaka mmoja, zimewauwa watu 10,000. Taarifa hiyo ilitolewa jana na shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lililo na makao yake nchini Uingereza.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov, amesema hawaichukulii taarifa ya ofisi zake nchini Uingereza kuwa ya kuaminika. Kwa mujibu wa shirika hilo la uchunguzi, watoto 900 ni miongoni mwa wahanga wa mashambulizi ya Urusi.
Mabomu yazidi kurindima Aleppo
Mapigano yanaendelea katika kampeni ya wiki nzima ya serikali ya Syria inayosaidiwa na Urusi, ikilenga kuwatimua wapinzani Mashariki mwa mji huo, eneo la mwisho la mjini linaloshikiliwa na waasi wa serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Urusi na serikali ya Assad waliutupilia mbali mpango wa kusitisha mapigano uliokuwa umefikiwa kati ya Marekani na Urusi mwezi uliopita, na kuanzisha operesheni dhidi ya waasi Mashariki mwa Aleppo, inayoonekana kuwa kubwa zaidi tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wamefanya mazungumzo ya simu kwa siku ya tatu mfululizo. Baadaye Lavrov amesema nchi yake ingekuwa tayari kufikiria njia zaidi ya moja ya kurejesha utulivu mjini Aleppo.
Lavrov hata hivyo ameikosoa Marekani kwa kushindwa kuwatenganisha waasi wenye misimamo laini na wale ambao Urusi inawaita magaidi, hali ambayo Urusi inasema ililiwezesha kundi ambalo siku za nyuma lilijulikana kama al-Nusra Front kuyakiuka makubaliano ya kusitisha uhasama yaliyofikiwa kati ya Marekani na Urusi tarehe 9 Septemba.
Msimamo wa Marekani njia panda
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi, John Kerry (kushoto) na Sergei Lavrov (kulia)
Ijumaa
Marekani ilisema bayana kuwa haijawa tayari kuitekeleza hatua ya
kusitisha ushirikiano na Urusi, iliyokuwa imeitangaza ikiwa Urusi
isingechukua hatua za haraka kusimamisha ghasia mjini Aleppo.Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Mark Toner amesema bado makubaliano ya amani hayajafa kabisa, na kuongeza kuwa wasingependa kuona mlango wa kidiplomasia ukifungwa kabisa.
Katika mazungumzo ya wanaharakati wa Syria pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, John Kerry aliwaambia wanaharakati hao kuwa utawala wa rais Obama umeshindwa kutoa kitisho chhochote cha kijeshi, ambacho kingezipa nguvu hoja zake katika mazungumzo yake na Urusi.
''Nadhani kuna watu watatu au wanne ndani ya utawala huo wanaopigia debe matumizi ya nguvu za kijeshi, na nimeshindwa '', waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amenukuliwa na gazeti la New York Times akiwaambia wasyria hao.
No comments:
Post a Comment