WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Wednesday, October 12, 2016

RAIS MAGUFULI ASITISHA VIONGOZI WA MIKOA KWENDA SIMIYU

 
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Eng. John Kijazi akitangaza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli kuhusiana na sherehe za kuzima mwenge mkoani Simiyu.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele
cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016
katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao
walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.


Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini
Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu
ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika
shughuli za maendeleo ya nchi.


Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda
Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi
wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri
za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao
wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.


Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17
iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika
maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.


Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya
vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao,
zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na
kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu
utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.


Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu
wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na
Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na
kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14
Oktoba, 2016.


Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed
Shein.


Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam          

12 Oktoba, 2016

No comments:

Post a Comment