WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Friday, October 21, 2016

WAZIRI NAPE NAUYE AMVAA ZITTO KABWE

ZITTO ACHA UNAFIKI

Na
Nape Nnauye (MB)
NAZIONA juhudi kubwa za Mbunge wa Kigoma Mjini Ndg. Zitto Kabwe kujaribu kupotosha jamii kwa kutosema ukweli kuhusu masuala kadhaa yahusianayo na Muswada wa Huduma za Habari, 2016.
Kwa kawaida mimi huwa sio mtu wa kujibu hoja zinazotolewa kinafiki na kioga kama alivyofanya rafikiangu Zitto Zuberi Kabwe. Kwa hali ya kawaida ningeweza kumpuuza kabisa, lakini kwa hili uvumilivu wangu kwa kiwango hichi cha unafiki umefikia ukingoni. Hivyo nitalazimika kujibu baadhi ya hoja.

Nimesoma kwa masikitiko sana sana, makala ndefu kidogo aliyoisambaza ndugu yangu na mwanasiasa kijana mwenzangu Ndg. Zitto Zuberi Kabwe kuhusiana na alichodai ni hatari ya Mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari 2016.

Muswada huu uliochapishwa na kuwekwa hadharani tangu Septemba, 2016, pamoja na mambo mengine unakwenda kuhitimisha safari ya zaidi ya miaka 20 ya wadau wa habari nchini kuwa si tu na sheria nzuri itakayoratibu kazi na kulinda maslahi yao, bali sheria inayoitangaza rasmi kazi hii kuwa taaluma kamili.

Hata hivyo, akiyatumikia maslahi yasiyo wazi kwa sasa, akiongozwa na unafiki wa hali ya juu kabisa kupata kuushuhudia kwake, na baada ya kujaribu kuzuia muswada huu kwenye Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na juhudi zake hizo kushindwa vibaya. Mbunge mwenzangu Zitto Kabwe ameanza kupayuka mitandaoni akieneza uzushi na kila aina ya uongo na upotoshaji kuhusu muswada huu. 

Inahitaji ujasiri wa kinafiki kuandika aliyoyaandika mwanasiasa mwenzangu kijana Zitto Zuberi Kabwe. Licha ya kuwa nimekuwa nikimheshimu kwa muda mrefu, na bado namheshimu na kumpenda kama kijana mwenzangu, unafiki huu wa kutumikia masilahi binafsi umenistua sana. 

Kama nilivyosema nitayajibu baadhi ya madai yake kama ifuatavyo:-

#1 Hoja ya Kushirikishwa wadau:
Zitto anajaribu kujenga picha kuwa muswada huu haukushirikisha wadau. Ndugu yangu huyu, huku akiwa anajua kuwa katika utungaji wa mswaada kuna hatua mbili za kutoa maoni. 

Hatua ya kwanza ni pale ambapo serikali inapokuwa inatengeneza mswaada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya kiserikali kwa hatua za kuupitisha wadau HUSHIRIKISHWA ili kutoa maoni yao. Na kwa mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari ,2016 WADAU wameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni yao UPO.

Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya mswaada kusomwa mara ya KWANZA bungeni, Mswaada husika hukabidhiwa kwa Kamati husika ya Bunge, na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma na kutoa maoni yao( public document) kwa Kamati ya Bunge. 

Hili pia limefanyika mpaka hatua ya wadau kuitwa na kuja Dodoma ambapo waliomba mbele ya Kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati Ndg. Peter Serukamba(mb) kwa uamuzi wa Kamati ya kudumu ya Bunge wakaamua kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli inayoendelea sasa.

Ndg Zito kwa makusudi aliamua kujaribu kuzuia hatua hii ya pili isifanyike bila mafaniko.
Hoja yake hiyo ilianguka mbele ya Kamati tulipoonesha ushahidi wa wazi na wa nyaraka kuwa wadau wakuu wote si tu walishiriki katika hatua za ndani ya Serikali kutoa maoni na sasa watashiriki zaidi katika hatua hizi za Bunge bali sehemu kubwa ya maoni yao yaliingizwa katika muswada wa sasa. Zaidi ya asilimia 90+% ya maoni ya wadau yamezingatiwa katika Mswaada huu. 

Alipoona kashindwa kabisa akaamua kuondoka Dodoma akasafiri na kusambaza waraka wa kizushi ili kufurahisha waliomtuma badala ya kuchangia kuboresha mswaada husika.

#2. Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC:-
Zitto pia anaeneza uongo kwamba muswada huu unadhamiria kuvifanya vyombo vya habari hususani TV kulazimishwa kujiunga na TBC kwenye vipindi vyake. 

Kwanza nina wasiwasi kama ameusoma muswada huu na kama ameusoma naanza kuamini hana muswada sahihi. Au ndio kaamua kutoa maoni akiongozwa na unafiki.
Hata hivyo hili tumelifafanua katika Kamati, kwa bahati mbaya hakuhudhuria ili kupata uelewa mpana. Mosi hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu; pili, hakuna dhamira hiyo kwenye muswada huu; na tatu, serikali haina hata wazo hilo.

#3. Mitandao ya kijamii:
Zitto katika kutimiza malengo na maslahi yake, anapotosha kuwa muswada huu unakusudia kuzibana blogs na kutaja mitandao ya kijamii kama jamiiforums kuwa nayo itatakiwa kusajiliwa. Mtu huyu ni wa kumwonea huruma. Bahati mbaya muswada huo hauna mamlaka wala nia hiyo. Kifungu cha 3 cha Sheria kiko wazi kuwa usajili utahusu magazeti na majarida na machapisho yao ya mitandaoni (magazeti mtandao ya magazeti hayo rasmi na sio mitandao yote au mingine ya kijamii kama anavyopotosha). 

Na kwakuwa nakala ya Mswaada huu ina tafsiri ya kiingereza na Kiswahili sitaki kuamini kuwa Zitto hakusoma hili, au waliomtuma hawakusoma vizuri hili.
Zitto anakwenda mbali kudai wachangiaji kama wa jamiiforums watatakiwa wafanyiwe ithibati! Bila shaka mwenzetu huyu anajadili muswada mwingine kabisa. 

Muswada huu hauhusu wala hakujapata kuwa na fikra za kudhibiti au kuratibu mitandao ya kijamii na kuwataka watumiaji wa mitandao hiyo eti wasajiliwe. Huu ni upuuzi mwingine wa kupuuzwa.

#4. Ipo hoja ya Waziri kupewa mamlaka kuagiza chombo chochote kutangaza jambo lenye umuhimu kwa umma: Katika hili pia tumsamehe kwa sababu hahudhurii vikao vya Kamati wakati wa mijadala hii. Hili limejadiliwa kwa kina na wahusika kuelewana. Hakuna kifungu kinachompa mamlaka hayo Waziri.
Bali kifungu kilichopo kinaipa fursa Serikali kuvishauri/kuvielekeza(Govt MAY) vyombo vya habari kuungana pamoja kulinda maslahi ya Taifa kunapokuwa na jambo la muhimu kama vile nchi kuwa VITANI au majanga makubwa. Zitto kama kijana wa Kitanzania kama haoni umuhimu wa hili basi hakuna namna nyingine ya kumsaidia.

#4 Kwamba muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti lichapishwe habari aitakayo.

Hili ni eneo lingine linalothibitisha kuwa hapa tunajihusisha na mtu mwenye malengo ya hatari sana na anayejaribu kuweka matazamio yake katika jambo la muhimu kama hili. Muswada huu hauna kifungu hicho zaidi ya Waziri kupewa uwezo wa kisheria, kama ilivyo katika sheria nyingine, kutunga kanuni za kutekeleza sheria hii. Hili nalo Zito hataki!!!!

#5Zitto anasema muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini. 

Ni kweli muswada umetoa mamlaka hayo lakini Zitto ameamua kutosema ukweli wote.

Muswada unampa Waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu majarida yanayotaka kuhamamsisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo.
#6. Zitto anazungumzia kuwepo kwa vifungu vya uchochezi akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa. Kwanza katika hili lazima ijulikane kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, masuala yote yanayohusu kusababisha athari kwa usalama wa taifa ni ukomo unaokubalika wa uhuru wa habari (allowable restriction to press freedom).

Uandishi wa habari kama taaluma nyingine unabeba haki na wajibu. Moja ya masuala ambayo waandishi wanapaswa kubeba wajibu kwayo ni kutosababisha hatari kwa usalama wa Taifa kwa kusababisha vurugu, chuki katika jamii (uchochezi). Hivyo katika kuweka vifungu hivi muswada umezingatia ukweli huo wa sheria za kimataifa.

Hata hivyo ieleweke, tofauti na Zitto anavyopotosha, sheria hii imekwenda mbali zaidi kwa ruhusu wananchi na watu wengine kuikosoa Serikali na utekelezaji wa sera zake.
Sheria inasema haitakuwa uchochezi kama mtu atatoa maoni yake kwa minajili ya kukosoa makosa katika Serikali, makosa katika utekelezaji wa sera (kifungu cha 49[2]). Huu ni uhuru mkubwa sana kuwahi kutamkwa na sheria.

Mwisho, namshauri Ndugu Zitto Kabwe apunguze kuishi kinafiki. Akasome tena muswada huu na alete hoja zake kwenye Kamati ya Bungeni zijadiliwe, aache kupotosha umma mitandaoni na aache kujiweka karibu zaidi na vibaraka.

Muswada huu, narudia tena, unakwenda kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma inayoheshimika. Ni muswada unaokwenda kuipa heshima taaluma hii na kila mmoja wetu awe tayari kwa mageuzi haya.
Katika kuifanya fani hii kuwa taaluma tunafahamu kuwa wapo waliozoea mambo ya kale na yale yale na kwamba watapinga; tunafahamu wapo watakaoona wanahabari waliowaajiri watadai maslahi zaidi na wapo watakaoona fani hii kuwa taaluma kamili watashindwa kuitumia kwa maslahi yao- wanahabari na wananchi tuungane kuwakataa wenye maslahi binafsi katika hili.

Tuungane kutoa maoni ili tuwe na muswada bora zaidi na utakaoifanya sekta ya habari kuwa na mchango mzuri zaidi kwa nchi yetu.

Kwasasa niishie hapa , lakini nitaendelea na awamu ya pili hata ya tatu ya ufafanuzi ikibidi. Uzalendo katika hili utashinda unafiki na utumwa wa kubeba mawazo ya watwana wachache walizoea vya kunyonga ambavyo kuchinja kwao msamiati!

No comments:

Post a Comment