WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Wednesday, December 7, 2016

HIVI NDIVYO RAIS MAGUFULI ALIVYOUNGURUMA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la
kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika Jiji la
Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya maeneo
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.


Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es
Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo
hilo aachie ngazi.


"Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi
wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata
kwa kufanya biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo
.

"Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza  madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na
Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho"
 amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga walioondolewa katika maeneo yao Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.

"Narudia na hii ni mara ya mwisho. Kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri. Kigamboni hapa palikuwa na Wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini
Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa"
 amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe. 

"Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu."Na hizi
ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda
kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini"
 amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2016.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwakaribisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo aliyeambatana na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe  kabla ya kuanza kwa kikao chao cha pamoja na Makamu wa Rais  Samia Suluhu Hassan.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika kikao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na  Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe.
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na  Makamu wa Rais Samia Suluhu mara baada ya kutoka kwenye kikao cha pamoja kilicho wahusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na  Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe Ikulu jijini Dar es Salaam

  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kumaliza kikao chao kilicho wahusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na  Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

No comments:

Post a Comment