WADHAMINI WETU

WADHAMINI WETU

Wednesday, December 7, 2016

Msaidizi wa Trump Michael Flynn Jnr apoteza kazi

Michael Flynn Jnr (kushoto) na babake, Luteni Jenerali Mstaafu Michael Flynn Snr wakiwaTrump Tower in New YorkMichael Flynn Jnr (kushoto) na babake, Luteni Jenerali Mstaafu Michael Flynn Snr wakiwaTrump Tower in New York.

Mmoja wa wasaidizi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump amepoteza kazi kwa kuendeleza uvumi ambao ulifikia kilele chake katika ufyatuaji wa risasi katika mgahawa mmoja wa pizza wikendi.
Michael Flynn, 33, aliacha kazi katika kundi la mpito la Bw Trump Jumanne kwa sababu ya ujumbe alioandika kwenye Twitter kuhusu habari za uongo.

Sakata hiyo sasa inafahamika kama Pizzagate.
Babake, Michael Flynn Snr, ambaye ameteuliwa na Bw Trump kuwa mshauri mkuu wa usalama wa taifa, pia alisambaza habari za uongo.

 

Uvumi huo wa Pizzagate ulisababisha mtu mwenye bunduki kufyatua risasi mgahawani Jumapili.
Hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea katika mgahawa wa Comet Ping Pong mjini Washington DC.

Mshukiwa huyo aliwaambia polisi kwamba alikuwa amefika eneo hilo "kuchunguza mwenyewe" uvumi ulioenezwa mtandaoni kwamba mgahawa huo ulikuwa ngome ya kundi la watu wanaowadhulumu watoto ambalo lilihusisha Hillary Clinton na mmoja wa wasaidizi wake, John Podesta.
 Edgar Maddison Welch, 28, akijisalimisha kwa polisi Jumapili
Uvumi huo ulikuwa umeenezwa na blogu za makundi yanayoegemea siasa za mrengo wa kulia.
Madai hayo pia yalienezwa na Bw Flynn Jr, ambaye Jumapili, baada ya ufyatuaji wa risasi kutokea katika mgahawa huo, alisema habari hizo zitasalia kuwa za kweli "hadi zithibitishwe kuwa za uongo."

Gazeti la New York Times linasema alifutwa kutoka kwenye kundi la mpito la Bw Trump Jumanne, lakini kwa mujibu wa CBS News, alijiuzulu kabla ya kufutwa.

Maafisa wa Trump wamethibitisha kuondoka kwa Bw Flynn, ambaye tayari alikuwa amepewa anwani ya barua pepe ya serikali inayoisha na .gov, lakini hawakusema iwapo kuondoka kwake kunahusiana na ujumbe wake katika Twitter.

 Tweet: Until #Pizzagate proven to be false, it'll remain a story. The left seems to forget #PodestaEmails and the many
Makamu wa rais mteule Mike Pence amekiri kwamba Bw Flynn Jnr alikuwa anamsaidia babake katika masuala ya ratiba na kiutawala kipindi hiki cha mpito lakini sasa hana tena majukumu hayo.
Babake, Bw Flynn Snr, 57, pia amewahi kusambaza kwenye Twitter uvumi wa kudai Bi Clinton na wasaidizi wake, walihusika katika ulanguzi wa watoto.
Luteni jenerali huyo mstaafu pia amewahi kudai kwamba Rais Barack Obama ni "mwanajihadi" ambaye "analangua na kutakasa" pesa kwa niaba ya magaidi.
Katika kisa cha Jumapili, mshukiwa Edgar Maddison Welch, 28, anayetoka North Carolina, aliingia Comet Ping Pong na kumwelekezea mfanyakazi mmoja bunduki lakini baadaye akafyatua risasi sakafuni.
Ameshtakiwa kwa kumshambulia mtu akitumia silaha hatari.

Kashfa ya Pizzagate ilianzaje?

Uvumi wa Pizzagate ulianza kwenye mtandao wa 4chan, kwa kutumia habari kuhusu barua pepe za chama cha Democratic ambazo zilikuwa zimefichuliwa na Wikileaks.
Mmiliki wa mgahawa huo, James Alefantis, ambaye ni mfadhili wa Democratic, alitajwa kwenye barua pepe hizo kuhusiana na hafla ya kuchangisha pesa za kampeni za Democratic.
Watu wanaotumia 4chan na mtandao mwingine wa Reddit, walianza kudai maneno kama vile jibini, hot dog na pizza yalikuwa maneno ya siri ya kuwarejelea watoto na ngono.
BBC.

No comments:

Post a Comment