Baadhi ya
wasichana wakitoka kukeketwa wilayani Tarime mkoani Mara, kumbuka mwezi
Disemba, kila baada ya miaka miwili, ni msimu wa ukeketaji na tohara
kwa baadhi ya Koo za Wakurya.
Pamoja na
juhudi za Serikali, Wanaharakati na Watetezi wa haki za binadamu
(Wanawake na Wasichana) katika kuhakikisha kwamba suala la ukeketaji
linatokomezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Mara na
Arusha, bado suala hilo ni pasua kichwa kwani linafanyika, iwe kwa uwazi
ama usiri.
Mtandao
wa Binagi Media Group umeshuhudia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tarime
wakisherehekea msimu huu wa ukeketaji (Mwezi Disemba kwa baadhi ya koo,
ikiwemo Watimbaru) ambapo wasichana wadogo wanafanyiwa ukeketaji.
Shamra
shamra zinafanyika hadharani licha ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious
Luoga, kuonya kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na ukeketaji
atachukuliwa hatua za kisheria.
Baadhi
huamini kwamba msichana akikeketwa huleta heshima kwake na kwa familia
na huwa tayari kwa ajili ya kuolewa na hivyo kuwapatia wazazi mahari
(ng'ombe). Hatua hii husababisha baadhi ya mabinti kukosa fursa ya
kuhitimu masomo yako na kujikuta wakiolewa, Aidha kwa kupenda ama
kulazimishwa na wazazi/walezi wao. Suala la unyanyapaa miongoni mwa
wasichana waliokeketwa na ambayo hawajakeketwa ni jambo ambalo pia
huongeza msukumo wa wasichana kutaka kukeketwa. Mbaya zaidi, unyanyapaa
huo huenda hadi kwa baadhi ya wanaume kukataa kuwaoa wale ambao
hawajakeketwa na hivyo kusababisha ugumu wa kutokomeza suala hilo.
Tayari
Ngariba mmoja aitwaye Angelina ppCharles (50) amehukumiwa kifungo cha
miaka miwili gerezaji kwa kosa la kumfanyia ukeketaji mmoja wa wasichana
wilayani humo huku wengine wawili wakidaiwa kukabiliwa na kesi ya aina
hiyo. Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya
ya Tarime, Mhe.Martha Mpaze.
Wakati
hayo yakiendelea, zipo kauli mbalimbali wilayani Tarime kwamba hivi sasa
wasichana hawakeketwi kama zamani bali wakifika eneo la tukio hupakwa
unga kwenye uso na maumbile yao na kufanyiwa matambiko ya kimila na
shughuli huishia hapo na kinachofuata ni shamra shamra za kucheza ngoma
ya ritungu na kurejea nyumbani.
Hata
hivyo utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana na Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja
wa Mataifa linalojihusisha na idadi ya watu duniani, UNFPA, kwenye mikoa
13 nchini ikiwemo Mara, umebaini kwamba katika maeneo mengi nchini,
wanajamii wanazo mbinu mpya za kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya
kukumbatia mila potofu ikiwemo ukeketaji. Utafiti huo ulibaini kuwa,
suala la kuwapaka unga usoni wasichana wilayani Tarime ni kuuficha tu
ukweli kwamba wasichana hao hawakeketwi wakati ukweli ni kwamba
hukeketwa.
Itoshe tu
kusema kwamba, elimu zaidi inahitajika ili kuwanusuru wasichana
wanaotoka kwenye makabila yanayojihusisha na ukeketaji kwani madhara
yake ni makubwa ikiwemo kupoteza damu nyingi, kupata madhara kabla na
baada ya kujifungua, kupoteza uwezo wa kufurahia tendo la ndoa,
uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa ikiwemo Virus vya Ukimwi na
wakati mwingine kupoteza maisha.
Inaelezwa
kwamba msichana anayekeketwa hulipia kiasi cha shilingi elfu 35 hadi 40
ambapo wazee wa kimila hugawana pesa hiyo na mangariba hivyo
inawezekana suala hili linakuwa na ugumu kutokomezwa maana ni sehemu ya
ujira kwa wazee na mangariba hao.
Inadhaniwa
kwamba zaidi ya wasichana 3,000 kwa Koo moja ya kabila la Wakurya
hukeketwa kwa kila msimu. Kabila la Wakurya lina Koo 13.
Wakazi wa
Wilaya ya Tarime wanasema, msukumo wa ukeketaji umepungua kwa kiasi
kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wanasema suala la elimu juu ya
madhara ya ukeketaji pamoja na mwingiliano wa makabila mbalimbali ya
ndani na nje ya mkoa wa Mara, umesaidia japo kwa kiasi kidogo kupunguza
ari ya ukeketaji.
Kataa
Ukeketaji, haina umuhimu kufurahia mila na tamaduni zenye athari katika
jamii. Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwakama na kuwafungulia
mashtaka.
Wakati
haya yanaendelea, zaidi ya wasichana 250 kutoka maeneo mbalimbali mkoani
Mara na Arusha, wamehifadhiwa katika kituo cha kuwahifadhi wasichana
waliokimbia ukeketaji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime.
KWA HISANI YA BMG
No comments:
Post a Comment